TANZANIA, BORA KUISHANGILIA-3: Arusha ninaanzia, mengi sana ya kujivunia

NA LWAGA MWAMBANDE

MKOA wa Arusha ni moja kati ya mikoa 26 ya Tanzania Bara, wenye ukubwa wa kilomita za mraba 34,515.5. Aidha, kiutawala mkoa huo uliopo Kanda ya Kaskazini mwa Tanzania unao wilaya sita na halmashauri saba,tarafa 23,kata 33,vijiji 393,mitaa 154 na vitongoji 1471.

Wilaya hizo ni Arusha yenyewe,Arumeru, Monduli,Karatu,Longido na Ngorongoro. Huku kwa upande wa halmashauri ikiwa ni Halmashauri ya Jiji la Arusha,Halmashauri ya Arusha, Meru, Monduli, Karatu, Longido na Ngorongoro

Aidha, Mkoa wa Arusha umepakana na Mkoa wa Manyara kwa upande wa Kusini, upande wa Mashariki umepakana na Mkoa wa Kilimanjaro, kwa upande wa Kaskazini umepakana na nchi ya Kenya na kwa upande wa Magharibi umepakana na Mkoa wa Simiyu na Mara.

Picha na andbeyond.

Pia, Arusha ni miongoni mwa mikoa nchi yenye fursa nyingi za kiuchumi ikiwemo vivutio mbalimbali vya kitalii. Ikifahamika kama Geneva of Africa, Arusha kuna mengi ya kujifunza.

Katika mwendelezo wa kukueleza fursa na mazuri yanayopatikana kila kona ya nchi, mshairi wa kisasa leo anakupitisha kwa njia ya ushairi katika mkoa na Jiji la Arusha. Endelea:

1.Arusha ninaanzia,
Makao ya Jumuia,
Mashariki nakwambia,
Afrika kanda nyumbani.

2.Mkoa twausifia,
Mengi ya kujivunia,
Vivutio vyajazia,
Kwa watalii nchini.

3.Utamaduni sikia,
Wamasai fwatilia,
Mila wanashikilia,
Kuwaona tatamani.

4.Vivutio sikizia.
Vingi nikikutajia,
Kiuchumi aminia,
Mkoa u kileleni.

5.Hifadhi za Tanzania,
Nyingi nitakutajia,
Ngorongoro naanzia,
Mlima Meru oneni.

6.Hapa kwetu Tanzania,
Tafiti zatuambia,
Yule mtu asilia,
Fuvu lake li nchini.

7.Olduvai pitia,
Uweze kupafikia,
Makumbusho nako pia,
Mengi yako vitabuni.

8.Arusha wanaingia,
Manyara yawavutia,
Mara wanajikalia,
Tule pesa za kigeni.

9.Tarangire mesikia,
Mbuga yetu yatulia,
Wanyama wazungukia,
Ni utajiri nchini.

10.Kitu sijawatajia,
Ni cha ajabu sikia,
Hicho kwetu chatukia,
Ni ajabu duniani.

11.Mchanga umesikia,
Uko kiguu na njia,
Unahama nakwambia,
Kila siku safarini.

12.Huo haujatulia,
Tangu kuumbwa dunia,
Unahama wakimbia,
Maajabu ya dunia.

13.Hivyo utalii pia,
Mchanga unavutia,
Ukiweza kufikia,
Tafurahia moyoni.

14.Jinsi kunavyovutia,
Arusha kunanukia,
Watu wengi wakujia,
Toka nje na nchini.

15.Viwanda vikubwa pia,
Arusha vimetulia,
Kimoja ntakutajia,
Ni maarufu barani.

16.Nishati kinachangia,
Ili watu kufikia,
Hapa nje watumia,
Chaleta mamilioni.

17.Ni transfoma sikia,
Arusha waziundia,
Zinauzwa Tanzania,
Rwanda hadi Kameruni.

18.Azimio kisikia,
Arusha lilianzia,
Ujamaa kusifia,
Ubepari uwe duni.

19.Kwa sehemu lichangia,
Vijiji kuanzishia,
Hapa tulipofikia,
Mchango wake nchini.

20.Hii yetu Tanzania,
Umoja twajivunia,
Kujitegemea pia,
Azimio liko ndani.

21.Njiani liliishia,
Hali ilipotitia,
Sasa tunajivunia,
Uchumi huru nchini.

22.Arusha twaisifia,
Sura inatuuzia,
Mengi imetufanyia,
Twajivuna bila soni.

23.Majanga yalitukia,
Rwanda yakawazidia,
Arusha wakafikia,
Mazungumzo mezani.

24.Na Burundi angalia,
Ugomvi liwazidia,
Amani kujipatia,
Arusha ndio nyumbani.

25.Haki kuitafutia,
Mauaji kufidia,
Arusha liwapatia,
Korti liyosheheni.

26.Kesi zilifanyikia,
Mafaili kupitia,
Hukumu wakafikia,
Rwanda kwa sasa amani.

27.Arusha twaitumia,
Mahakama zakalia,
Kanda na Barani pia,
Majaji wako kazini.

28.Arusha twajivunia,
Watu maarufu pia,
Ambao walipitia,
Kufuatilia amani.

29.Mandela nakutajia,
Clinton naye pia,
Hata Bush nakwambia,
Maarufu duniani.

30.Arusha lipafikia,
Kazi wakijifanyia,
Na mbuga walifikia,
Tanzania ya amani.

31.Arusha kikutajia,
Kitu nakukumbushia,
Kitaifa twasifia,
Viongozi walo wini.

32.Sokoine angalia,
Lowassa nakutajia,
Uongozi Tanzania,
Walishika usukani

33.Hao twawashangilia,
Kuwajibika sawia,
Mambo walitufanyia,
Kusahau abadani.

34.Sokoine nakwambia,
Wahujumu walilia,
Walanguzi nao pia,
Liswekwa korokoroni.

35.Huyo hasa lizidia,
Nchi liwajibikia,
Waziri Mkuu pia,
Kwa mara mbili nchini.

36.Ajalini alifia,
Alipotutumikia,
Bado tunamuwazia,
Hatunaye duniani.

37.Wengi tulifikiria,
Dola alishikilia,
Pengine angeingia,
Ikulu ya Magogoni.

38.Ndoto hazikutumia,
Zile tulizowazia,
Njiani aliishia,
Akazikwa kaburini.

39.Vile tulimlilia,
Bado ninakumbukia,
Nadhani historia,
Wa kwanza kufa kitini.

40.Lowassa aliingia,
Nchi akatumikia,
Mengi ametufanyia,
Sote tunayathamini.

41.Jinsi alisimamia,
Walotaka kukalia,
Viwanja tunatumia,
Pale Mnazi amini.

42.Mabati walizuia,
Mradi wakianzia,
Yeye akaingilia,
Asiondoe kwa nini?

43.Citywater kumbushia,
Maji kutuhudumia,
Hovyo walitufanyia,
Na kutuleta shidani.

44.Yale walitufanyia,
Lowassa liangailia,
Mwishoni alifikia,
Kuwatimua jioni.

45.Kesi litufungulia,
Kisasi kutufanyia,
Lakini walifulia,
Tukashinda kortini.

46.Maji alifwatilia,
Kanda ya Ziwa sikia,
Maji wanajimwagia,
Mradi uko makini.

47.Lowassa hakusinzia,
Shule Kata kuanzia,
Sasa tunajivunia,
Wahitimu milioni.

48.Ukuu lipoishia,
Machache litufanyia,
Muda hakumalizia,
Kajikalisha pembeni.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news