TANZANIA, BORA KUISHANGILIA-5: Dodoma ni Tanzania,Dodoma nambari wani

NA LWAGA MWAMBANDE

WAKATI wa Uhuru, Mkoa wa Dodoma ulikuwa sehemu ya Jimbo la Kati. Mwaka 1963 Mkoa wa Dodoma ulianzishwa baada ya kutenganisha mikoa ya Singida na Dodoma (mikoa hiyo miwili ilikuwa sehemu ya lililokuwa Jimbo la Kati).

Aidha, wakati wa kuanzishwa kwake mkoa ulikuwa na wilaya tatu za Dodoma Vijijini, Kondoa na Mpwapwa. Baadaye, Wilaya ya Dodoma Mjini iliunda wilaya ya nne.

Pia, historia inaonesha kuwa mwaka 1995 Wilaya ya Mpwapwa iligawanywa na kuwa wilaya mbili ambazo ni Kongwa na Mpwapwa zilizounda wilaya ya tano katika mkoa huo.

Mwaka 2007 Wilaya ya Dodoma Vijijini iligawanywa katika wilaya mbili za Bahi na Chamwino. Hii iliunda wilaya ya sita, na mwaka 2012 Wilaya ya Kondoa iligawanywa katika wilaya mbili ambazo ni Kondoa na Chemba ambazo hatimaye ziliufanya mkoa kuwa na wilaya saba.

Mkoa huu ambao ni makao makuu ya nchi,imeundwa na halmashauri nane ikiwemo Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa, Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa na Halmashauri ya Mji Kondoa.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema licha ya Dodoma kuwa makao makuu ya nchi, mkoa huo una mambo mengi na historia ndefu ya kuvutia. Endelea;


1. Dodoma nafagilia,
Mji Mkuu wa nia,
Serikali metulia,
Watu wako ofisini.

2. Dodoma likoanzia,
Jina ninakutajia,
Ni tembo alizamia,
Akanasa matopeni.

3. Likuwa Idodomia,
Jina ndipo liingia,
Hapo limeshikilia,
Maarufu duniani.

4. Nyerere nakutajia,
Rais aloanzia,
Na wengi liazimia,
Dar es Saalam hameni.

5. Hao lijichagulia,
Dodoma kuitumia,
Hiyo ninakuambia,
Ni miaka ya sabini.

6. Awamu kwanza anzia,
Ya nne kimalizia,
Kidogo walichangia,
Kuweka nzuri ramani.

7. Bunge lilishahamia,
Vikao vyafanyikia,
Wizara nyingi salia,
Dasalamu ondokeni,

8. Magufuli kuingia,
Tamko likatujia,
Alipotutangazia,
Dodoma ndio jijini.

9. Wengi walifikiria,
Maneno ya kusikia,
Kumbe alidhamiria,
Dodoma pawe nyumbani.

10. Miaka likaribia,
Hamsini kufikia,
Toka lipoazimia,
Dodoma kuwa enzini.

11. Jinsi alishikilia,
Serikali kuhamia,
Kinyume hakurudia,
Hadi kufika mwishoni.

12. Sasa ndugu aminia,
Serikali shahamia,
Wizara zote sikia,
Dodoma ndiyo nyumbani.

13. Hilo nimewaambia,
Sifaze nawatajia,
Mkoa navyovutia,
Utajiri ni nishani.

14. Wagogo nawatajia,
Kabila ninaanzia,
Hawa ni Watanzania,
Usoamini amini.

15. Katikati Tanzania,
Ndiko kwao asilia,
Huwezi kuwasikia,
Wako nchi ya jirani.

16. Tofauti nakwambia,
Makabila twasikia,
Kenya hata Tanzania,
Huko ni kwao nyumbani.

17. Tena mwenzangu sikia,
Lugha yao asilia,
Huwezi kuisikia,
Nchi nyingine jirani.

18. Kigoma ukisikia,
Warundi takuambia,
Wanyarwanda nao pia,
Wanajuana kindani.

19. Warangi nao sikia,
Dodoma wanajazia,
Hawa ni Watanzania,
Wenye rangi ya thamani

20. Dodoma kwa asilia,
Ni heri kifwatilia,
Hawa wanajivunia,
Ni katikati nchini.

21. Mji mkuu sikia,
Rahisi kupafikia,
Bukoba ukianzia,
Kati piga darubini.

22. Mtwara ukipitia,
Na Kilimanjaro pia,
Dodoma panasalia,
Ni katikati nchini.

23. Mazao wajilimia,
Chakula kujipatia,
Mengine wajiuzia,
Yajaa tele sokoni.

24. Zabibu umesikia,
Tamu kijitafunia?
Mvinyo wazifanyia,
Dodoma nambari wani.

25. Fedha nyingi zaingia,
Zabibu kijilimia,
Hizo tunafurahia,
Shilingi na za kigeni.

26. Viwanda twavisikia,
Mvinyo watufanyia,
Na pia zabibu kavu,
Bora mapishi nyumbani.

24. Uwele tajipatia,
Na mtama kujilia,
Mifugo mingi sikia,
Mbuzi, ng’ombe tatamani.

25. Toka Iringa pitia,
Singida utaishia,
Moro kama waanzia,
Manyara barabarani,

26. Dodoma ni Tanzania,
Sote tunajivunia,
Hasa alotia nia,
Ikulu iwe nyumbani.

27. Malecela kisikia,
Jina kubwa Tanzania,
Urais linukia,
Dodoma ndiko nyumbani.

28. Mwinyi limsaidia,
Kuongoza Tanzania,
Mageuzi kuanzia,
Nchi ipae winguni.

29. Maarufu Tanzania,
Na hata kwenye dunia,
Busara amezidia,
Wamjua Marekani.

30. Lowassa kikutajia,
Kule alijifunzia,
Malecela takwambia,
Lipikwa kama mekoni.

31. PM wa Tanzania,
Wadhifa lishikilia,
Hata kwenye chama pia,
Likuwa juu enzini.

32. Kama ukimsikia,
Kitu akisimulia,
Yote yatakuingia,
Kutoka kwake kinywani.

33. Huyu alishikilia,
Nafasi nyingi sikia,
Hadi kule lifikia,
Hekima ya duniani.

34. Wakati lipofikia,
Mandela kumwachilia,
Kwenye timu ya dunia,
Malecela pia ndani.

35. Sauzi waliingia,
Kumtoa lichangia,
Huyu twamshangilia,
Ni maarufu nchini.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news