TANZANIA, BORA KUISHANGILIA-6: Hapa Geita, mali kubwa ya Dunia imejaa

NA LWAGA MWAMBANDE

HISTORIA inaonesha kuwa, Mkoa wa Geita ulianzishwa rasmi kwa Tangazo la Serikali namba 72 la Machi 2, 2012, na kuzinduliwa Novemba 8, 2013 na Mheshimiwa Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete, Rais mstaafu wa Awamu ya Nne ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, mkoa huo ulitokana na sehemu ya mikoa ya Mwanza, Kagera na Shinyanga ambapo upande wa Magharibi na Kusini unapakana na Mkoa wa Kagera, upande wa Kusini na Kusini Mashariki unapakana na Mkoa wa Shinyanga na Mwanza kwa upande wa Kaskazini unapakana na Ziwa Victoria.

Geita una eneo au ukubwa wa kilometa za mraba 21,879 (Geita 6,375 km2, Bukombe 6,798 km2, Chato 3,572 km2, Mbogwe 3,684 km2, na Nyang`hwale 1,450 km2), kati ya hizo kilomita za mraba 19,933 ni za nchi kavu na kilomita za mraba 1,946 ni za maji.

Mkoa una wilaya tano,majimbo saba ya uchaguzi,halmashauri sita, mji mdogo mmoja,tarafa 23, kata 122, vijiji 474, vitongoji 2,219 na mitaa 65. Wilaya hizo ni Geita, Nyang‟hwale,Chato, Bukombe na Mbogwe.

Pia, mkoa una jumuisha Halmashauri ya Mji Geita, Halmashauri za Wilaya za Geita, Nyang’hwale, Chato, Bukombe na Mbogwe. Kuanzishwa kwa mkoa huu kumesaidia kuharakisha upelekaji wa huduma za kijamii, kiuchumi na maendeleo kwa wananchi.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, mkoa una wakazi wapatao 2,977,608 ambapo wanaume ni 1,463,764 na wanawake ni 1,513,844

Wakati huo huo, mkoa unapata mvua za kutosha kuanzia milimita 900 hadi 1200 na joto la wastani la nyuzi 22 hadi 30 kwa mwaka.

Vile vile, mkoa umekuwa ukipata mvua za vuli katika kipindi cha kuanzia Septemba hadi Desemba na mvua za masika kuanzia mwishoni mwa mwezi Februari hadi Mei.

Pia, kipindi cha kiangazi huanza mwanzoni mwa mwezi Juni hadi Septemba kila mwaka na unyevu wa kati ya asilimia 35 na 60.

Wakazi wa Mkoa wa Geita wanajishughulisha na shughuli mbalimbali za uzalishaji mali ikiwa ni pamoja na kilimo, ufugaji wa mifugo mbalimbali na nyuki, uvuvi, uchimbaji madini pamoja na biashara ndogo ndogo.

Sekta ya kilimo inachangia takribani asilimia 70 ya pato la mkoa wa kati shughuli nyingine za kiuchumi zinachangia asilimia 30.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mwaka 2013 zinaonesha kuwa, mchango wa Mkoa wa Geita katika pato la taifa umefikia shilingi bilioni 1,584 wakati pato la mwananchi ni shilingi 910,824 huku kukiwa na fursa mbalimbali za uwekezaji. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anakupitisha Geita kwa njia ya ushairi ili kuweza kufahamu mengi. Endelea;


1. Geita mkoa pia,
Mpya umeibukia,
Kilimo mifugo pia,
Huko mingi yasheheni.

2. Rais wa tano pia,
Ndiko kwake asilia,
Mengi alitufanyia,
Magufuli huyu Johni.

3. Pamba wanajilimia,
Pesa wanajipatia,
Na mifugo mingi pia,
Imejaa mabandani.

4. Mali kubwa ya dunia,
Mifugo tunatambia,
Geita tajipatia,
Kwa kilo hata kwa tani.

5. Dhahabu imejazia,
Kuichimba kwasalia,
Makampuni ya dunia,
Yamejazana nchini.

6. Nyingine wajipatia,
Juu juu nakwambia,
Na pia wajichimbia,
Chini sana ardhini.

7. Kanda ya Ziwa sikia,
Ni wengi Watanzania,
Kabila zazidi mia,
Wasukuma namba wani.

8. Watu hao nakwambia,
Huko ndiko wajazia,
Hapa kwetu Tanzania,
Kabila kubwa amini.

9. Kipenda Mwanza anzia,
Mikoa ntakutajia,
Geita, Simiyu pia,
Shinyanga kwao nyumbani.

10. Hawa watu nakwambia,
Ukali sijasikia,
Upole wamezidia,
Ule wa kutoka ndani.

11. Kazi wachangamkia,
Kama ukiwapatia,
Ukitaka jisikia,
Nenda hadi vijijini.

12. Mke ukijipatia,
Baraka tajipatia,
Mume ukijipatia,
Ushafika kileleni.

13. Pale mnakutania,
Yenu kuzungumzia,
Ni wawazi nakwambia,
Hilo kwangu liamini.

14. Rafiki kijipatia,
Toka huko furahia,
Amani itazidia,
Hadi mwende kaburini.

15. Ukarimu mesikia,
Mali na chakula pia,
Hao tunajivunia,
Ni Wasukuma nchini.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news