TANZANIA, BORA KUISHANGILIA-7: Hodi! hodi! Iringa,Iringa twausifia sana

NA LWAGA MWAMBANDE

MKOA wa Iringa unapatikana katika Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania kati ya Latitudo 6.540 na 100 na Longitudo 33 na 370-000 Mashariki.

Iringa ni kati ya mikoa 26 ya Tanzania Bara na mikoa 31 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo upo katikati ya nchi, kidogo upande wa Kusini. Umepakana na mikoa ya jirani ya Morogoro, Njombe, Mbeya, Singida na Dodoma.

Mkoa huu una historia ndefu ya kuvutia na hapa ndipo unaweza kupata simulizi ya kusisimua kumuhusu Mkwawa ikiwa ni kifupisho cha Mukwava au Mukwavinyika lililokuwa jina lake la heshima likimaanisha "kiongozi aliyetwaa nchi nyingi".

Mkwawa alizaliwa mnamo mwaka 1855 mahali palipoitwa Luhota karibu na Iringa Mjini. Alikuwa mtoto wa Chifu Munyigumba aliyefariki mwaka 1879.

Wanahistoria wanasema, Baba yake Munyingumba aliwahi kuunganisha temi ndogo za Wahehe na makabila ya majirani kuwa dola moja.

Aliiga mfumo wa kijeshi wa Wasangu waliowahi kuwa kabila lenye nguvu kwa kujifunza mfumo huo kutoka kwa Wangoni na Shaka Zulu.Hadi miaka ya 1870 eneo la Wahehe lilipanuliwa mbali kuanzia Kusini hadi katikati ya Tanzania ya leo.

Baada ya kifo cha chifu mzee watoto wake walishindania urithi wake, na Mkwawa alishinda akawa kiongozi mpya. Aliendelea kupanua utawala wake. Hadi mwisho wa miaka ya 1880 alitawala sehemu muhimu za njia ya misafara kati ya Pwani na Ziwa Tanganyika

Ilikuwa mwaka 1894, Chifu wa Wahehe Mkwawa alijenga ngome yenye urefu wa kilomita 13 na urefu wa mita nne kwa ajili ya kujaribu kupigana na ukoloni wa Wajerumani.

Mwaka 1898, baada ya miaka tisa ya kuwanyanyasa Wajerumani katika mfululizo wa vita vya msituni, Mkwawa inaaminika kwamba alijitoa uhai mwenyewe. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, kwa ujumla Iringa kuna mambo mengi mazuri ambayo itakuchukua muda mrefu kuyafahamu kwa ufasaha. Endelea;


1. Iringa tunaringia,
Mkwawa kikumbukia,
Jinsi livyojipigia,
Mkoloni Jerumani.

2. Mkoloni kumjia,
Apate kumkalia,
Vema limfanyizia,
Anakumbukwa nchini.

3. Silaha lizotumia,
Kweli hazikutimia,
Vumbi limtimulia,
Aloleta ukoloni.

4. Nguvu zilipomwishia,
Mtego hakuingia,
Mbali alijiulia,
Katoweka duniani.

5. Darasa atupatia,
Ya kwamba hakutulia,
Nchi alipigania,
Kumpinga mkoloni.

6. Jinsi walivyofulia,
Mkwawa kijipigia,
Fuvu lijichukulia,
lisibakie nchini.

7. Juzijuzi nakwambia,
Walipoturudishia,
Shujaa anasalia,
Wa kutukuka nchini.

8. Fundisho linaingia,
Kwa hii historia,
Mababu ninakwambia,
Walipinga ukoloni.

9. Iringa twausifia,
Hapa kwetu Tanzania,
Mengi unatufanyia,
Tubakie furahani.

10. Kwa chakula nakwambia,
Ziada watupatia,
Mahindi hata bamia,
Wanalima makondeni.

11. Kuna Wahehe sikia,
Hawaogopi jambia,
Ujasiri wazidia,
Kwa makabila nchini.

12. Tunao Wabena pia,
Ni wa pole Tanzania,
Kazi wanajifanyia,
Wasiishi kwa madeni.

13. Ukarimu wazidia,
Kama ukiwafikia,
Kweli utafurahia,
Huko kwao malangoni.

14. Iringa twajivunia,
Misitu imetimia,
Mbao tunajipatia,
Viwandani majumbani.

15. Nyanya tunazotumia,
Nyingi watuzalishia,
Chai Mufindi sikia,
Iko nyingi mashambani.

16. Ajira jitafutia,
Kilimo kinachangia,
Misitu mazao pia,
Huko ni bora nchini.

17. Ulanzi ninakwambia,
Ni pombe yetu sikia,
Twagema twajipatia,
Kuburudika jioni.

18. Na wengine nakwambia,
Pesa unawapatia,
Kote wanajiuzia,
Wakiutoa shambani.

19. Ruaha twaisifia,
Mbuga kubwa Tanzania,
Wageni waifikia,
Na watalii wa ndani.

20. Wanyama na ndege pia,
Kwa wingi wametulia,
Hakika wanavutia,
Mkawaone nendeni.

21. Utajiri wetu pia,
Ni neema Tanzania,
Fedha yatuingizia,
Shilingi na za kigeni.

22. Baridi yapulizia,
Huko ninakuambia,
Kama joto lazidia,
Kapumzike mbugani.

23. Pareto wajilimia,
Madawa twajifanzia,
Na madola mia mia,
Yanaingia nchini.

24. Kitaka tajirikia,
Iringa kule ingia,
Miradi tajifanyia,
Kwa kipato mfukoni.

25. Shambani ninakwambia,
Utajiri wanukia,
Fanya kujiamulia,
Hata miti msituni.

26. Hivi sasa nakwambia,
Wengi huko wahamia,
Wawezwe kujipatia,
Maisha ya ugenini.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news