TANZANIA, BORA KUISHANGILIA-8: Nyumba kwa nyumba sikia, Kagera pazuri

NA LWAGA MWAMBANDE

HISTORIA inaonesha kuwa, kabla ya Uhuru na hadi kufikia mwaka 1961, eneo la sasa la Mkoa wa Kagera lilikuwa ni moja ya maeneo yaliyounda jimbo lililoitwa Lake Province.

Jimbo hili lilijumuisha wilaya za Bukoba, Musoma, Shinyanga na Tabora. Baada ya Uhuru mwaka 1962 mkoa ulibadilishwa jina na kuitwa West Lake Region (Ziwa Magharibi) na kujumuisha wilaya nne za Ngara, Biharamuro, Karagwe na Bukoba.

Jina la Ziwa Magharibi lilidumu katika kipindi cha ukoloni na baada ya uhuru mwaka 1961 mpaka mwaka 1979 baada ya vita kati ya Tanzania na Uganda (Vita ya Kagera).

Mkoa ulipata jina la Kagera kutokana na Mto Kagera zamani ukijulikana kama Akagera ambao hutiririsha maji yake kutoka Rwanda kupitia Kaskazini na kumwaga maji yake katika Ziwa Victoria.

Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa 26 ya Tanzania na 31 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo unapatikana Kaskazini Magharibi mwa nchi ya Tanzania.

Makao Makuu ya Mkoa yapo katika mji wa Bukoba umbali wa kilometa 1500 kutoka Dar es Salaam. Mkoa huu unapakana na nchi ya Uganda kwa Kaskazini, Rwanda na Burundi kwa upande wa Magharibi.

Aidha, mikoa ya Geita na Kigoma kwa upande wa Kusini. Pia Mkoa wa Kagera unapakana na Ziwa Victoria kwa upande wa Mashariki ambapo kwa ndani ya ziwa hilo mkoa unapakana na mikoa ya Geita, Mwanza na Mara.

Vile vile Mkoa wa Kagera uko Kusini mwa Ikweta kati ya Latitude 1 “00” na 2”45”. Mashariki mwa ‘Greenwich' katika Longitudi 30”25” na 32”40”

Mkoa wa Kagera una jumla ya eneo la kilomita za mraba 35,686 kati ya hizo kilomita za mraba 25,513 ni eneo la nchi kavu ambalo ni sawa na asilimia 73 ya eneo lote la mkoa na kilomita za mraba 10,173 ni eneo la maji sawa na asilimia 27.

Mkoa una visiwa vikubwa katika Ziwa Victoria ambavyo ni Bumbire, Iroba, Kelebe, Goziba, Ikuuza na Mhutwe na visiwa vingine vidogo jumla vikiwa 27 vinavyokaliwa na watu na jumla ya visiwa 21 vidogo vidogo visivyokaliwa na watu.

Ukiacha mbali Wilaya ya Biharamulo ambayo ni tambarare, sehemu kubwa ya mkoa ni yenye milima na vilima vilivyogawanywa na mabonde yenye matingatinga.

Upande wa Magharibi wa mkoa mito mingi inamwaga maji yale katika Mto Kagera ambao nao humwaga maji yake katika Ziwa Victoria.

Mwinuko wa nchi (altitude) ni kati ya mita 1,100 na 1,800 juu ya usawa wa Bahari. Mchanganuo wa kilomita za mraba kwa kila halmashauri ni kama ifuatavyo Halmashauri ya Wilaya Biharamulo (5,627 km2), Halmashauri ya Wilaya Bukoba (5,071 km2), Bukoba Manispaa (80km2), Halmashauri ya Wilaya Karagwe (4,630 km2), Halmashauri ya Wilaya Kyerwa (3,086 km2), Halmashauri ya Wilaya Missenyi (2,709 km2), Halmashauri ya Wilaya Muleba (10,739 km2), na Halmashauri ya Wilaya Ngara (3,744 km2).

Kabla na baada ya kuja kwa wakoloni Mkoa wa Kagera ulikuwa na utawala wa Kimila (Chiefdoms) uliogawanyika katika himaya nane. Himaya hizo ni pamoja na Kyamutwara, Kihanja (Kanazi), Kiziba, Ihangiro, Bugabo, Karagwe, Biharamulo (Rusubi) na Maruku (Bukara).

Baadhi ya Watemi waliotawala himaya hizo ni pamoja na Emmanuel Rukamba (Kyamtwara), Rumanyika (Karagwe), Kasusura (Biharamulo), Lugomola (Bukara), Rutinwa (Kiziba), Kayo za (Bugabo), Kahigi (Kihanja) na Nyarubamba (Ihangiro). Kila mtemi alikuwa na walinzi wake walioitwa Warugaruga.

Makabila yanayopatikana hivi sasa katika mkoa wa Kagera ni pamoja na Wahaya ambao wanapatikana zaidi katika wilaya za Bukoba, Muleba na Missenyi.

Makabila mengine ni Wanyambo, wanaopatikana katika Wilaya za Karagwe na Kyerwa, Wasubi katika wilaya ya Biharamulo, Wahangaza wanaopatikana katika Wilaya ya Ngara. Pia kuna Waha, Wazinza and Warongo.

Baada ya kuja kwa wazungu waliongeza ulimaji wa kahawa kama zao la biashara lililowasaidia kujiongezea kipato. Wakazi wa asili ya Kagera ni wabantu na wengi wao wanaasili ya Bunyoro.

Wanaongea lugha sawa na ile ya Wanyoro, Wanyankole, Watoro na Wakiga. Busubi na Bugufi wana lugha na desturi sawa na Watusi, Wahutu na Waha. Lakini makabila hayo ni ya Wabantu wa Ziwa (Interlacustrine Bantu) na yanafanana mila na desturi.

Makundi hayo yaligawanyika katiya wachungaji (Bahima) ambao walitawala na wakulima (Bairu) ambao walitawaliwa na mara nyingi kudharauliwa.

Bahima (Balangira) walikuwa na koo chache zipatazo 20 na walitawaliwa na Wahinda, Wabito na Wankango Bairu walikuwa na koo kama 130 zenye mashina 24 ambayo kiasili walikuwa Bairu, lakini kwa kuoa katika Bahima au kufanya kazi kwa Watemi walipandishwa hadhi na kuwa Bahima (Batware).

Kila ukoo uliitwa jina la Baba mwanzilishi wake na kina ukoo ulikuwa na kitu walichokatazwa kula (Omuziro) na mnyama walioshirikishwa nae (Ekyerumono).

Wakati huo huo, hali ya hewa ya Mkoa wa Kagera kwa ujumla ni ya joto la wastani wa 26.02 sentigredi. Mvua zinanyesha kwa wastani wa milimita 800-1,100 kwa mwaka kati ya mwezi Septemba na Januari na kati ya mwezi Machi na Mei.

Mvua hizi ndizo zinazowezesha kuwepo kwa uoto wa asili wa kuvutia katika maeneo mengi ya mkoa. Kwa miaka ya kawaida mkoa hupata mvua za uhakika za vuli na masika ambazo ni muhium kwa shughuli za kilimo na ufugaji.

Uchumi wa wenyeji wa Mkoa wa Kagera ulijikita katika mashamba ya migomba na kahawa. Chakula chao kikuu ni ndizi katika aina zake mbalimbali. Katika mashamba yao hulima mazao mengine kufuatana na msimu. Mazao hayo ni pamoja na maharage, mihogo, mahindi na mboga. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema ndani ya Kagera utafurahia mengi. Endelea;

1.Kagera ni Tanzania,
Mkoa naupania,
Ni mzuri nakwambia,
Matoke tele amini.

2.Hali ya hewa sikia,
Kwa kweli inavutia,
Kwenda waweza salia,
Kwenu usipatamani.

3.Watu wa Kagera pia,
Wanajipenda sawia,
Mkazo wanatilia,
Maendeleo kichwani.

4.Wasomi wa kuzidia,
Watu wanajisikia,
Kwa hoja kuwazidia,
Ufanye kazi amini.

5.Samaki wanajilia,
Ziwani Victoria,
Wengine watuvulia,
Tule bara hadi pwani.

6.Kama unajisifia,
Shule umejipatia,
Kagera ukifikia,
Utajua wao nani.

7.Shahada zimezidia,
Nyumba kwa nyumba sikia,
Hata ukiwasikia,
Lugha ni changanyikeni.

8.Kama unajisikia,
Mara mbili fikiria,
Mhaya kimfikia,
Hapo ndipo kituoni.

9.Utajiri mwatambia,
Nyumba mmejifanyia,
Wenyewe wanatambia,
Umahiri wa kichwani.

10.Usije kufikiria,
Mjini wanasalia,
Vijijini kiingia,
Nyumba mjini mjini.

11.Miwa wanajilimia,
Sukari watupatia,
Matoke twayasikia,
Kagera i kileleni.

12.Kagera twakumbushia,
Kumbukumbu yasalia,
Vita vilipotujia,
Vya Nduli Idd Amini.

13.Amini lituvamia,
Vitisho kitufanyia,
Na vifo vikatujia,
Na hasara majumbani.

14.Kagera Mto sikia,
Daraja la Tanzania,
Alivyotushambulia,
Lisababisha madeni.

15.Daraja katuvunjia,
Shida zikatuzidia,
Makubwa tulipitia,
Kusahau asilani.

16.Vitani tukaingia,
Taifa kupigania,
Tukafanya yenye nia,
Akafia ugenini.

17.Mashujaa nakwambia,
Waliotupigania,
Hapa hawakuishia,
Wakaenda ugenini.

18.Uganda liwasaidia,
Mbali kumtimulia,
Amani ikaingia,
Pasipo Idd Amini.

19.Shida nyingi lipitia,
Toka vita kuingia,
Wengine ninakwambia,
Jambo bado li moyoni.

20.Jina tulilojulia,
Lile tulilitumia,
Ziwa Magharibi pia,
Sasa Kagera jueni.

21.Mto Kagera sikia,
Ni mkubwa nakwambia,
Ziwani unaingia
Samaki umesheheni.

22.Mkoa unachangia,
Uchumi wa Tanzania,
Biashara yazidia,
Na nchi za mpakani.

23.Uganda iko kulia,
Ngara Rwanda waingia,
Burundi yakaribia,
Zote ziko mpakani.

24.Kagera naisifia,
Muleba namalizia,
Wilaya metuzalia,
Kiongozi ni makini.

25.Inamjua dunia,
Hata yetu Tanzania,
Jinsi atutumikia,
Yabaki yake thamani.

26.Ni Anna jina sikia,
Mama twamfagilia,
Huyu Profesa pia,
Tibaijuka ubini.

27.Profesa twatambia,
Zao letu Tanzania,
Habitat kumbukia,
Alikalia kitini.

28.Makazi amechangia,
Kote alikopitia,
Hazina ya Tanzania,
Afrika duniani.

29.Kagera wanakwambia,
Usomi wajivunia,
Ukitaka hesabia,
Ni wengi sana jamani.

30.Wahaya ninakwambia,
Kweli wanajisikia,
Mambo wanajifanyia,
Kweli wanajiamini.

31.Kiwanda twajivunia,
Cha Kagera nakwambia,
Sukari tuzalishia,
Kwa matumizi nchini.

32.Tena ukikifikia,
Yake kuyaangalia,
Vizuri kinatumia,
Wataalamu nchini.

33.Tena chatupunguzia,
Nchi yetu Tanzania,
Sukari kuagizia,
Fedha zetu za Kigeni.

34.Ajira kiangalia,
Zote za Watanzania,
Mishahara yaingia,
Na hata kodi ghalani.

35.Kabanga umesikia?
Madini yalojazia?
Yale tutajichimbia?
Tuneemeke nchini?

36.Ni Nickel nakwambia,
Ambayo tunatambia,
Pesa itatupatia,
Kwa wingi sana jamani.

37.Ajira tajipatia,
Hata kodi kuingia,
Uchumi kuinulia,
Kwenda juu toka chini.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602


Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news