NA DIRAMAKINI
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Mei 20, 2023 ameandika historia mpya ya Tanzania kwa kuzindua majengo mapya ya Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma huku akishuhudiwa na mamia ya watanzania pamoja na wageni mbalimbali kutoka nje ya Tanzania.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa na Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdalla pamoja na Rais mstaafu Mzee Ali Hassan Mwinyi na Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete wakati akikata utepe kuashiria ufunguzi wa jengo la Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma leo Mei 20, 2023.(Picha na Ikulu).
Katika hafla za uzinduzi huo Rais Dkt. Samia amesema jambo hilo ni la kihistoria kwa watanzania kwani kwa mara ya kwanza, wameweza kujenga Ikulu yao kwa kutumia rasilimali zao pamoja na wataalamu wa ndani.

Amesema, kukamilika kwa mradi huo ni jitihada za Serikali za Awamu zote Sita za uongozi aidha, Rais Samia amesema aliahidi kukamilisha miradi aliyoipokea kutoka kwa mtangulizi wake Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, hivyo kukamilika kwa mradi huu ni utekelezaji wa kauli yake.

“Nilipokabidhiwa hatamu za kuiongoza nchi yetu, niliahidi nitaendeleza mema yaliyopo, nitaboresha inapobidi na nitaleta mema mapya, ujenzi wa Ikulu hii ni moja ya miradi niliyorithi kutoka kwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli na ni mradi wa pili kuukamilisha, mradi wa kwanza ulikua daraja la Tanzanite – Dar es Salaam, namuomba Mungu anipe uwezo niikamilishe yote,” amesema Rais Dkt. Samia.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango wakati wakipiga ngoma kabla ya kuingia Rasmi katika Ofisi za Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 20 Mei, 2023.
Rais Dkt. Samia amesema ni takribani miaka 50 toka mchakato wa Serikali kuhamishia Makao Makuu ya nchi Dodoma kutangazwa rasmi mwaka 1973, ambapo Serikali ilianza utekelezaji kwa kujenga taasisi zake mbalimbali ikiwemo Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ofisi za Bunge, Wizara ya TAMISEMI, Chuo Kikuu cha Dodoma, Hospitali ya Benjamini Mkapa na Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete pamoja na kupanua eneo ilipojengwa Ikulu hiyo kutoka heka 66 mpaka 8473.
“Katika utekelezaji wa wazo la kuhamisha Makao Makuu ya Serikali Dodoma, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ameandika historia yake, hatutoweza kuandika historia ya shughuli hii bila ya kuwepo kwa tahariri ya mchango wake mkubwa, tuendelee kumuombea Mwenyezi Mungu ampumzishe kwa Amani,” amesema Rais Dkt.Samia.
Taswira ya Jengo jipya la Ikulu ya Chamwino kama linavyoonekana pichani ambalo limezinduliwa Rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan tarehe 20 Mei, 2023.





Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Tulia Ackson pamoja na Spika wa Baraza la Waakilishi Mhe. Zubeir Ally Maulid mara baada ya kufungua Jengo la Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 20 Mei, 2023.

Akiongelea hatua inayofuata baada ya kukamilika kwa majengo ya Ikulu hiyo Rais Samia alisema ni ujenzi wa jengo la kisasa litakaloitwa ‘Samia Complex’ ambapo litajumuisha ukumbi mkubwa wa mikutano utakaoweza kuchukua idadi ya watu 2000-3000, nyumba za viongozi, Zanzibar Lounge, East Afrika Lounge, njia ya ndege, sehemu ya historia ya viongozi pamoja na viwanja vya michezo mbalimbali.