TANZANIA,BORA KUISHANGILIA-9: Migebuka kumbukia,Hakika huoni ndani

NA LWAGA MWAMBANDE

HISTORIA inaonesha kuwa, Mkoa wa Kigoma ni miongoni mwa mikoa ya Tanzania Bara yenye ardhi yenye rutuba ya kutosha, uoto wa asili na hali ya hewa ya kuvutia.

Pia, mkoa unayo bionuai adimu yenye kuvutia watalii kutoka ndani na nje ya nchi. Ipo milima, mabonde, mito na Ziwa Tanganyika ambalo linashika nafasi ya pili duniani kwa kuwa na kina kirefu cha maji.

Kwa ujumla jiografia ya Mkoa wa Kigoma inaufanya kuwa mkoa wa kimkakati kwa uwekezaji wa kitalii, kilimo, viwanda na biashara.

Aidha, shughuli za kiuchumi katika mkoa zimeendelea kuimarika kutokana na jitihada za Serikali za kuboresha huduma mbalimbali za kijamii, miundombinu ya barabara,reli, umeme na usafiri wa anga.

Kigoma una eneo la kilomita za mraba 45,075. Kati ya hizo, kilomita za mraba 36,523 ni nchi kavu na kilomita za mraba 8,552 ni eneo lililofunikwa na maji.

Mkoa unapakana na nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) upande wa Magharibi na Burundi upande wa Kaskazini Magharibi.

Ndani ya nchi, mkoa unapakana na mikoa ya Kagera upande wa Kaskazini, Shinyanga upande wa Kaskazini-Mashariki, Katavi na Rukwa upande wa Kusini na Tabora upande wa Mashariki.

Kwa kiasi kikubwa kuanzia Kaskazini Mashariki yote mpaka Kusini Mashariki Mkoa wa Kigoma umezungukwa na Ziwa Tanganyika.

Hali ya hewa ya Mkoa wa Kigoma ni ya joto kiasi na unyevunyevu. Joto linafikia nyuzi joto kati ya 17-33 ‘centigrade’ na unapata wastani wa mvua zenye ujazo wa mm 800-1200 kwa mwaka.

Kutokana na mvua za kuaminika, wakulima huweza kupanda baadhi ya mazao hadi mara mbili kwa mwaka. Mvua huanza mwezi Oktoba na kuishia mwezi Mei na kufuatiwa na kipindi kirefu cha jua yaani kiangazi.

Shughuli kuu za kiuchumi katika Mkoa wa Kigoma zimejikita katika kilimo, ufugaji,uvuvi, biashara na viwanda vidogovidogo.

Jitihada za uongozi wa mkoa na ongezeko la kibajeti, rasilimali watu na vitendea kazi uliofanywa na Serikali umewezesha changamoto nyingi kutatuliwa na hivyo kuwapa fursa wananchi kujikita katika uzalishaji mali.Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anakushirikisha mambo haya muhimu kutoka mkoani Kigoma. Endelea;


1.Kigoma meisikia?
Migebuka kumbukia,
Mkoa unavutia,
Umetanda ufukweni.

2. Waha ni Watanzania,
Kweli wanashikilia,
Kitu wakikubishia,
Hakika huoni ndani.

3. Huko mwanzo wa dunia,
Ya taifa Tanzania,
Machache nitagusia,
Ili uweze baini.

4. Kigoma nakuambia,
Rutuba naisifia,
Wenyewe wajilimia,
Mazao yenye thamani.

5. Sijawahi kusikia,
Njaa imewafikia,
Wakaanza kuwania,
Msaada kwa jirani.

6. Mambo waliyopitia,
Mengi sana nakwambia,
Wakimbizi kuhamia,
Wakajaa makambini.

7. Ujambazi wa jambia,
Na bunduki kutumia,
Wengi wameshaumia,
Lakini wafanye nini?

8. Vurugu zipotukia,
Waburundi litujia,
Congo nako kikalia.
Wote wakaja nchini.

9. Wengi walikoishia,
Ni Kigoma nakwambia,
Wengi metuharibia,
Huo ndio ujirani.

10. Utalii kisikia,
Kigoma wanatishia,
Huko ukikufikia,
Utafurahi moyoni.

11. Sokwe mtu mesikia,
Nenda kuwaangalia,
Elimu tajipatia,
Gombe ni kwao nyumbani.

12. Mbuga tunajivunia,
Hapa kwetu Tanzania,
Goddall twakumbukia,
Alivyoishi nchini.

13. Sokwe awaangalia,
Na wao anatulia,
Kama wamfahamia,
Ni ajabu duniani.

14. Mahale ni mbuga pia,
Tembelea yavutia,
Pesa zatuingizia,
Za kwetu na za kigeni.

15. Kile kwetu chasalia,
Mbuga ninokutajia,
Kuzidi kujitunzia,
Zizidi faa nchini.

16. Wale wanatuibia,
Wanyama kutuulia,
Na misitu kuishia,
Hawatufai nchini.

17. Vema kuwachukulia,
Hatua kuwafagia,
Mbuga zisijeishia,
Tubakie maskini.

18. Kigoma ukiingia,
Mwisho wa Reli sikia,
Ziwa utafurahia,
Kina bora duniani.

19. Tanganyika nakwambia,
Ziwa tunajivunia,
Samaki wa Tanzania,
Wamejaa protini.

20. Pengine umepania,
Kazi ya kujifanyia,
Biashara shamiria,
Kigoma utashaini.

21. Migebuka tajilia,
Na dagaa nakwambia,
Kongo Burundi sikia,
Wanafaidi amini.

22. Michikichiki twatambia,
Mawese yatupatia,
Chakula tunapikia,
Kigoma tuko rahani.

23. Uvinza waisikia,
Maarufu Tanzania,
Chumvi huko twachimbia,
Inatufaa mekoni.

24. Chumvi ukiangalia,
Ni bidhaa masalia,
Ila bila kutumia,
Chakula hutotamani.

25.Waimbaji wenye nia,
Kigoma tajipatia,
Wacheza mpira pia,
Kigoma kwao nyumbani.

26.Mkuu ametujia,
Kigoma twajivunia,
Mbele atutangulia,
Samia kiwa kitini.

27.Dokta nakutajia,
Wa uchumi Tanzania,
Makamu Rais pia,
Kwa sasa yuko kazini.

28.Mpango ameingia,
Buhigwe alianzia,
Kazi anatufanyia,
Nchini na duniani.

29. Zamani lijilimia,
Huko alikoanzia,
Shule akashikilia,
Sawa na utamaduni.

30.Wengi katufundishia,
Chuo Kikuu sikia,
Hata Benki ya Dunia,
Alikuwako kazini.

31.Tume Mipango sikia,
Mengi alitupangia,
Na hapo hakuishia,
Akaenda wizarani.

32. Myaka mitano sikia,
Pesa alitutunzia,
Ni sifa kubwa sikia,
Wasema serikalini.

33. Sasa hapa Tanzania,
Huyo amsaidia,
Rais kusimamia.
Maendeleo nchini.

34. MV Liemba pia,
Maarufu Tanzania,
Meli ya historia,
Toka kwa Wajerumani.

35. Karne imezidia,
Tangu ilipoingia,
Usafiri twatumia,
Hapa na kwa majirani.

36. Kumbukumbu zatwambia,
Kabla vita ya dunia,
Ziwani iliingia,
Hadi sasa i kazini.

37. Na tena cha kuvutia,
Hasa kwa historia,
Ni peke imesalia,
Ya wa kwanza wakoloni.

38. Kigoma ukifikia,
Tumia kusafiria,
Utajiri Tanzania,
Wa pekee duniani.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602


Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news