TaTrade, RCT wabisha hodi kwa wafanyabiashara wa mchele Mbarali

NA MWANDISHI WETU
Mbarali-Mbeya

MAMLAKA ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kwa kushirikiana na Baraza la Mchele Tanzania (RCT) wametoa semina kuhusu upatikanaji wa masoko pamoja na taratibu za mauzo nje (exports) kwa Wasindikaji na Wafanyabiashara wa Mchele katika eneo la Halmashauri ya Mbarali mkoani Mbeya.

Washiriki wa semina hii ni pamoja na viongozi waliowakilisha wafanyabiashara wa mchele kutoka Tandale (mwenyekiti mwakilishi wa wafanyabiashara 1,055), Tandika, Temeke, na Mbagala ambayo uhudumia masoko ya Mkuranga, Rufiji na Kilwa.

Wadau wengine waliohudhuria ni Mbeya Rice, KTC Kilombero Rice, MTC Morogoro wakiwakilisha vikundi vya wachakataji na wadau wa mchele wa Igawa na Ubaruku.

Lengo la semina hiyo lilikuwa kutoa uelewa kuhusu Biashara za Mchele katika Soko la Ndani na kuwaunganisha Wasindikaji na wadau wa Masoko yenye walaji wengi (ikiwemo DSM) ili waweze kuwa na mahusiano ya kibiashara na kutengeneza Biashara endelevu.

Akifungua semina hiyo Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Mhe. Col.Dennis Mwila amesisitiza Wasindikaji na wafanyabiashara wa mchele kujipanga kimkakati na kuhudumia fursa za Masoko ndani na nje badala ya kutulia na kulalamika kukosa Soko.

Naye, Mtaalam kutoka TanTrade Bw. Deo Shayo alibainisha maeneo ambayo Mchele na nafaka ya Tanzania kwa ujumla inafanya vizuri kuwa ni katika Masoko ya Miji ya kibiashara ikiwemo Dsm na Arusha na kwa upande wa Masoko ya Nje yanayoonekana zaidi kuwa ni Kenya, Burundi, Uganda, Congo DRC, Zambia na Rwanda. Akifafanua taratibu na nyaraka muhimu kwa Biashara za nje ( exports)

Bw. Shayo ametoa ushauri kwa wafanyabiashara kuchangamkia fursa mpya zinazoibuka za Biashara katika Soko Huru la Afrika (AfCFTA) ambapo wigo wa kuhudumia ni mkubwa zaidi wenye nchi zaidi ya 50 kwa unafuu wa Kodi ya forodha na pia walaji wengi zaidi. Pia wafanyabiashara wametakiwa kushiriki matukio ya Ukuzaji Biashara ya TanTrade ikiwemo Maonesho ya Sabasaba 28 Juni hadi 13 Julai 2023 ili kujitangaza.

Kwa upande wa Baraza la Mchele wameahidi kuendelea kuwasaidia wazalishaji wa mchele katika masuala ya kushauri sera rafiki kwa kushirikiana na serikali ili kuimarisha uzalishaji na Biashara za Mchele nchini.

Aidha, wafanyabiashara wameishukuru RCT kupitia wawakilishi wake Bw. Geofrey Rwiza na Leoncia Salakana na pia Serikali kwa ujumla kwa kuona umuhimu wa kuinua zaidi Biashara za Mchele kwani zimeajiri watu wengi na pia kuongoza katika mauzo ya nje hivi karibuni.Hivyo kuomba matatizo yao ya mara kwa mara ikiwemo tozo wanapovuka Halmashauri moja hadi nyingine zipunguzwe au kuondolewa kabisa.

Mpango huu wa mafunzo na kukutanisha wadau ni sehemu ya juhudi zinazofanywa na Baraza la Mchele Tanzania kwa kushirikiana na wafadhili na Mamlaka za Serikali ili kuboresha mnyororo wa thamani wa mpunga na bidhaa zinazohusiana.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news