UDOM wafunguka kuhusu kifo cha mwanafunzi Nusura Hassan Abdallah

NA DIRAMAKINI

CHUO Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimeeleza kusitishwa na kifo cha mwanafunzi Nusura Hassan Abdallah ambaye alikuwa mwanafunzi wa Shahada ya Kwanza ya Sanaa katika Elimu (BA.Ed) katika Ndaki ya Insia na Sayansi za Jamii ya chuo hicho.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Mei 5, 2023 na Kitengo cha Masoko na Mawasiliano cha Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

"Katika mitandao ya kijamii kumekuwa na taarifa ambazo sio rasmi kuhusu aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Nusura Hassan Abdallah.Menejimenti ya Chuo inatoa taarifa rasmi kuhusu tukio hili.

"Nusura Hassan Abdallah alikuwa mwanafunzi wa Shahada ya Kwanza ya Sanaa katika Elimu (BA.Ed) katika Ndani ya Insia na Sayansi za Jamii ya Chuo Kikuu cha Dodoma.

"Taarifa zinaonesha kwamba hadi kufikia jioni ya Aprili 27, 2023, Nusura Hassan Abdallah alionekana chuoni akiendelea na masomo kama kawaida.

"Mei 3, 2023, Menejimenti ya Chuo ilipokea taarifa kutoka kwa mwanafunzi ambaye alikuwa anasoma naye kuwa, amepokea taarifa kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kuwa ni mjomba wake Nusura Hassan Abdallah, akimjulisha kuwa mwanafunzi Nusura Hassan Abdallah amefariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Faraja iliyopo Himo, Kilimanjaro.

"Tukizingatia kwamba, masomo yanaendelea, Menejimenti ya Chuo ilifanya juhudi za kutafuta taarifa za ziada na kufanikiwa kumpata dada yake Nusura Hassan Abdallah anayeishi Uchira mkoani Kilimanjaro ambaye alithibitisha kutokea kwa kifo cha mdogo wake.

"Taarifa zaidi zilieleza kuwa mwili wa marehemu ulisafirishwa Mei 3, 2023 kutoka Moshi hadi nyumbani kwao Iramba, Singida.

"Baada ya chuo kujiridhisha na taarifa hizo utaratibu ulifanyika kwa kushiriki kutoa salamu za pole kwa familia. Maziko ya Nusura Hassan Abdallah yalifanyika Mei 4, 2023 nyumbani kwao Iramba mkoani Singida.

"Menejimenti na Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Dodoma imesikitishwa sana na msiba huu na inatoa pole nyingi kwa familia ya marehemu Nusura Hassan Abdallah,"imefafanua kwa kina sehemu ya taarifa hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news