Upuuzi haujibiwi, unapuuzwa-Rais Dkt.Mwinyi

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema, mara nyingi masuala ya kipuuzi ambayo yanalenga kupotosha kwa makusudi kuhusiana na mustakabali mwema wa nchi hayapaswi kujibiwa badala yake yanapaswa kupuuzwa.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo Mei 30, 2023 Ikulu jijini Zanzibar katika vikao vya kawaida vya kila mwezi na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu nchi.

"Kwanza nianze kuwashukuru waliotangulia kwa kuanza kuuliza maswali,kwa mengi ya maswali yaliyotangulia ni mengi yalitokana na mikutano iliyofanywa na Chama cha ACT Wazalendo na maneno yaliyokuwa yakizungumzwa na Balozi Karume katika mitandao.

"Labda na mimi nichukue fursa hii, kama nilivyosema siku za nyuma, kwamba upotoshaji lazima tuutolee ufafanuzi ili watu wasiendelee kupotoshwa, lakini masuala ambayo mimi ninayaita ya kipuuzi, upuuzi haujibiwi, unapuuzwa.

"Kwa hiyo mtanisamee yale ambayo mimi ninayahesabu ya kipuuzi, kwa sababu hayapaswi hata kusikilizwa, achilia mbali kujibiwa."

Bandari

"Leo ninataka nisema kuhusu maeneo ambayo watu wanajaribu kupotosha watu kwa makusudi,tuyatolee ufafanuzi watu waelewe.

"La kwanza, mradi wa ujenzi wa Bandari ya Mangapwani.Ujenzi wa Bandari ya Mangapwani kama tulivyosema siku za nyuma ni ujenzi wa bandari kubwa, ni ujenzi wa bandari jumuishi, ni ujenzi wa bandari ambayo itahudumia si Zanzibar tu,bali tunataka ihudumie kanda nzima hii ya Afrika.

"Na hili bandari (Mangapwani) hiyo ipatikane basi lazima utaratibu wake ukae sawa, ni kweli tulianza na watu wa Oman tukafanya feasibility study, tukafanya mazungumzo tukaishia sehemu ambayo si kwamba tumemalizana hata kidogo ni kwamba bado fursa ya kuendelea ipo pale ambapo watakuwa tayari kuendelea.

"Lakini haikuwa na maana kwamba tusizungumze na watu wengine,tukazungumza na watu wengine, tukazungumza na Abu Dhabi,na mazungumzo hayo yanafanywa na nani? Mazungumzo hayo yanafanywa na timu ya majadiliano ya Serikali (Government Negotiations Team), lengo letu ni nini?.

"Lengo letu ni kupata mkataba utakaokuwa na maslahi ya nchi, kwa hiyo hatuwezi tu kuingia katika mkataba wa haraka haraka, lazima tuhakikishe mkataba una maslahi ya nchi.

"Lazima tuhakikishe kwamba, bandari ile inajengwa kama tunavyotaka sisi. Bandari ile itakuwa ni sehemu ya makontena, itakuwa ni sehemu ya mafuta, itakuwa na sehemu ya nafaka, itakuwa na sehemu ya mafuta na gesi.

"Itakuwa na sehemu ya eneo huru kwa maana ya free zone ambapo ndani yake kutakuwa na logistics centre. Kwa hiyo, kama nilivyosema siku za nyuma ni mji wa bandari si bandari tu, Mangapwani-Bumbwini itakuwa miji ya bandari, mambo makubwa yanahitaji majadiliano ya uhakika, yanahitaji kuhakikisha kwamba Serikali yetu au nchi yetu inanufaika na mradi huo.

"Kwa hiyo, wakisema kwamba wamejiondoa si kweli, bado tupo katika mazungumzo, lengo ni kupata mkataba bora na yeyote ambaye yupo tayari kutoa maslahi bora kwa nchi yetu, huo ndio ukweli wa mambo na ninadhani kwamba wanafahamu, lakini wakisimama kwenye majukwaa wanafanya makusudi ili kupotosha umma,"amefafanu Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi.

Malindi

"La pili, kuhusu Bandari ya Malindi na mchakato wake, Bandari ya Malindi nimeshawahi kuizungumzia mara kadhaa hapa,kuwa haina ufanisi.

"Bandari ya Malindi inaathiri uchumi wetu wa Zanzibar,kwa sababu meli moja inashushwa na kupakiwa zaidi ya wiki, nilisema siku za nyuma, meli zikiwa 10 ile ya 10 itakaa siku sabini, kama meli moja ni siku saba.

"Miezi miwili hauwezi kuweka meli hapa,kuna tatizo la ufanisi katika bandari yetu. Ufanisi uliopo katika bandari yetu unasababisha biashara hapa Zanzibar zimekuwa ngumu kwa sababu watu hawana uhakika mzigo walioagiza utafika lini, lakini kukaa hapo kusubiri kushushwa kuna gharama kubwa,zile meli zinachaji kwa kila siku kwa nusu bili ya hapa.

"Kwa hiyo ilikuwa lazima tutafute njia mbadala na hili ninataka watu walielewe vizuri, hatuna maana tunatoa sisi watu wa nje watusaidie kuja kuendesha, kwa hiyo tunafanya hivyo pale ambapo inaonekana sisi tumeshindwa na ukweli ndio huo tupende tusipende hauwezi kuwa na bandari ambayo hauna uhakika mzigo wako utashuka lini, ni mbaya kwa biashara.

"Kwa hiyo tukasema tutafute watu wa kutusaidia kutuendeshea hii bandari kwa mkataba maalumu, tumetafuta hao watu na makampuni mengi yalijitokeza. Watu wa Oman walikuwa na utayari wa kufanya hivyo, watu wa Abu Dhabi walikuwa wanataka kuendesha Bandari ya Malindi kabla ya kuja Mangapwani.

"Ikaja kampuni nyingine inaitwa Bollore (Bolloré Transport & Logistics) hii ni kampuni ambayo ina bandari nyingi barani Afrika ambazo inazihudumia.

"Sasa hivi hii kampuni ya Bollore imenunuliwa na kampuni kubwa za meli duniani, ile kampuni ya MSc. Sasa hoja iliyopo hapa ni kwamba, sisi tukitaka kuitoa bandari yetu ili ipate ule ufanisi, lakini si ufanisi tu tupate na kipato ambacho ni bora kuliko tunachokipata sasa hivi, tukaangalia katika makampuni haya tukaona na majadiliano kwa maana ya Serikali yalifanywa na Government Negotiations Team.

"Kwa maana wamekaa wakajadiliana mpaka tukaona tuwape hii kampuni ambayo inaitwa Africa Logistics Group, hawa ni sehemu ya MSc na zamani walikuwa wanaitwa Bollore na kwa kweli tumekubaliana kwamba watabadilisha utendaji pale bandarini ili tuweze kupata ufanisi, moja katika vitu tulivyokubaliana ni kwamba badala ya meli kushushwa kwa siku saba, basi isivuke siku mbili.

"Huo ndio ufanisi tunautaka, lakini vile vile pale bandarini kwa taarifa zenu ni kwamba, bandari yetu inaendeshwa kizamani mno, hakuna system (mfumo) ya kompyuta, haijulikani mizigo mingapi, meli gani imeshusha makontena mangapi,wanafanya manually kila kitu ambapo ndani yake kuna kila sababu ya kuwa na wizi.

"Mnazungumza bwana nimeshashusha meli yangu, ninataka bili ulipe makontena mangapi, hayo mambo hayafai. Siku hizi kila kitu ni kidijitali, kompyuta inakuwezesha kufahamu meli haijafika hapa, idadi ya makontena imeshajulikana, bili yako imeshakuwa tayari ukifika hapa unapewa bili yako.

"Hayo ndiyo mambo yanakwenda kufanyika pale, kuna ujenzi wa ICD (bandari kavu) Maruhubi, hao mabwana watakwenda kujenga kule,Bandarini hapa Malindi itakuwa kupakia na kushusha,hakuna biashara nyingine pale, biashara zote za ushuru, biashara gani ni Maruhubi hapo ndipo utapatikana ufanisi.

"Kwa hiyo mtu akisimama kwenye jukwaa akadai, kwamba haya tunayoyafanya ni makosa kwa kweli ninashangaa sana, mnataka lini tuendelee na bandari isiyokuwa na ufanisi? Inaingiza gharama katika kila mzigo wa mfanyabiashara?.

"Baadhi ya meli zilikuwa zimeanza kukataa kuja Zanzibar kwa sababau zilikuwa zimechoka kusubiri sana ukuta, haya yote tunataka tuyatatue, njia ya kuyatatua ndiyo hizi, lakini hata kipato taarifa zilizopo ni kwamba mapto yaani ile revenue wanayoyapata sasa hivi, wakitoa gharama za uendeshaji, faida inayobaki ni asilimia 16 , mkataba wetu tuliokubaliana na hawa wanaoendesha bandari, faida ambayo Serikali itapata ni asilimia 30.

"Sasa ukisimama jukwaani lazima useme hoja yako ni nini. Kama ni mapato, tutapata zaidi kutoka asilimia 16 mpaka 30 kama ni ufanisi utaongezeka zaidi kutoka siku saba mpaka siku mbili unataka nini zaidi?. 
 
"Kwa hiyo mimi ninadhani, mambo mengine yanasemwa, lakini maadamu dhamira yetu ni safi, maadamu lengo letu ni kufanya biashara iwe rahisi, tupunguze gharama za kufanya biashara tutaendelea na hayo yanayoendelea kusemwa jukwaani waendelee kusema, wananchi wasipotoshwe, ukweli ni kwamba Serikali hii inataka kufanya mambo yawe bora zaidi si kinyume chake,"amefafanua Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news