NA DIRAMAKINI
WAKILI Harold Sungusia amechaguliwa kuwa Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) katika uchaguzi uliofanyika ljumaa Mei 12, 2023 kwenye Mkutano Mkuu wa Mwaka 2023 unaofanyika jijini Arusha.
Sungusia amechaguliwa kuwa Rais wa Tanganyika Law Society kwa mwaka 2023-2024 kwa kupata kura 748 kati ya kura 825.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha wanasheria Tanganyika,Wakili Charles Rwechungura ndiye aliyemtangaza Harold Sungusia kuwa rais mpya wa chama hicho baada ya matokeo ya uchaguzi, huku nafasi ya Makamu wa rais ikichukuliwa na Aisha Sinda.
Aidha,kati ya kura zilizopigwa 825 hakuna iliyoharibika ambapo Harold Sungusia alipatata kura 748 huku Reginald Shirima akipata kura 77.
Kwa upande wa nafasi ya Makamu wa Rais, Aisha Sinda alipata kura 527,Emmanuel Augostino kura 261 na Revocatus Kuuli kura 32.
Wakili Christopher Alex amechaguliwa kuwa MwekaHazina wa TLS kwa mwaka 2023-2024 kwa kupata kura 807 kati ya kura 825.
Naye Wakili Edward Heche amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Mawakili Vijana (AYL) wa TLS kwa mwaka 2023-2024.
Wakili Sungusia anachukua nafasi ya Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) anayemaliza muda wake,Profesa Edward Hoseah ambaye awali alikitetea kiti chake cha urais kwa kuibuka mshindi kwa kupata kura 621.
Akitangaza matokeo hayo Mei 27,2022 katika ukumbi wa mikutano wa AICC, Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi, Charles Rwechungura alisema kuwa, kura zilizopigwa zilikuwa 1,150 ambapo Profesa Hoseah aliibuka mshindi dhidi ya wagombea wenzake ambao ni Harold Sungusia (380) na Jeremiah Mtobesya (145).