Wabunge wataka Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote

*Wasema ni ngumu kumudu gharama za matibabu

NA MWANDISHI WETU
Dodoma

WABUNGE wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamesema kuwa ni muda muafaka sasa kupitisha Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ili kuwezesha wananchi kumudu gharama za matibabu.

Wakichangia hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Wizara ya Afya, iliyowasilishwa jana, wamesema kwa sasa ni ngumu mwananchi wa kawaida kumudu gharama za matibabu wakiwa nje ya mfumo wa bima ya afya.

”Bima ya Afya kwa Wote inahitajika sana kwani usipokuwa na fedha ni ngumu sana kumudu gharama za matibabu, ni vyema sasa Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote ukaletwa kwa haraka,” alisema Mhe. Dkt. Christina Mzava.

Mbunge mwingine aliyesisitiza umuhimu wa Bima ya Afya kwa Wote ni Mhe. Hawa Mchafu ambaye alisema kuwa kutokana na ongezeko kubwa la magonjwa yasiyoambukiza ambayo yanahitaji fedha nyingi kujitibia ni vyema Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ikapitishwa ili kusaidia wananchi.

Akiwasilisha makadirio hayo, Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu alitoa rai kwa wananchi kujiunga na familia zao kwenye Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kabla ya kuugua ili waweze kunufaika na huduma za matibabu bila kikwazo chochote.

Amesema kuwa utamaduni uliojengeka wa wananchi kujiunga na NHIF baada ya kuugua ni kinyume na dhana ya bima ya afya hivyo ili kuendelea kuimarisha uhai na uendelevu wa Mfuko, Serikali kupitia NHIF imefanya tathmini ya wanufaika wake na msisitizo kwa sasa upo katika usajili kupitia Vifurushi vya bima ya afya ambavyo vina utaratibu wa kusajili katika ngazi ya familia.

Vifurushi hivi vijulikanavyo kama Najali Afya, Wekeza Afya na Timiza Afya vinatoa fursa kwa familia kusajiliwa kulingana na ukubwa wake, mahitaji pamoja na kipato na kwa utaratibu mwingine watoto wanaweza kusajiliwa kupitia shule wanazosoma, lengo ikiwa ni kusajili watoto wengi kwa umoja wao kulingana na misingi na dhana ya bima ya afya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news