Waguswa na ombi la Prof.Muhongo serikalini kuhusu VETA

NA FRESHA KINASA

WANANCHI katika Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara wamepongeza hatua ya Mbunge wao, Prof.Sospeter Muhongo kuiomba Serikali kufanikisha ujenzi wa Chuo cha Veta jimboni humo kitakachojikita katika mambo ya kilimo, uvuvi na ufugaji.

Wameyasema hayo leo Mei 18, 2023 wakati wakizungumza na DIRAMAKINI ambapo wamesema kuwa, Prof.Muhongo anatekeleza vyema majukumu ya kuiomba Serikali mambo mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi na pia wameshukuru Serikali imekuwa ikifanya jambo ambalo linawapa furaha na matumaini chini ya uongozi thabiti wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Shabani Bwire mkazi wa Nyegina jimboni humo amesema kuwa, anashukuru Prof.Muhongo kumkumbusha Waziri wa Elimu juu ya Chuo cha VETA ambapo amesema iwapo chuo hicho kikijengwa kitasaidia kuleta mapinduzi jimboni humo.

"Prof Muhongo katika Mchango wake Bungeni Mei 17, 2023, alisema akipewa VETA yeye atataka ijikite katika mambo ya kilimo,uvuvi na ufugaji na sio mambo ya magari au hoteli. Mimi naungana naye kwa sababu atakuwa ameona mbali zaidi kuhusu rasimali zilizopo Musoma Vijijini na pia kupitia VETA na namna hiyo vijana wataandaliwa vyema katika mambo ya uvuvi, ufugaji na hivyo watakuwa wabobezi na watafanya mambo hayo kisasa na kisomi,"amesema Bwire.

Naye Naomy Justine mkazi wa Etaro amesema kuwa,"Kukiwa na chuo Cha VETA Musoma Vijijini kitajikita zaidi katika kilimo, ufugaji na uvuvi hivyo vijana wakaandaliwa vyema Musoma Vijijini na Mkoa wa Mara watakuwa wazalishaji wakubwa wa mazao ya kilimo na hata ufugaji, kwa mfano watafuga samaki kwa njia ya vizimba na watauzwa kwa bei nzuri na mazao ya kilimo yatachakatwa,"amesema na kuongeza kuwa.

"Pia, watafuga ng'ombe wa kisasa watazalisha maziwa kwa wingi, watafuga kuku kisasa zaidi na kwa tija kubwa, kumbe badala tu ya vijana kufundishwa magari, umeme, ujenzi wanapokwenda vyuo vya VETA kumbe tunaweza kuwa na VETA ambayo inaweza kujikita kuwafundisha vijana mambo ya kilimo na ufugaji kwa undani zaidi kama alivyobainisha Prof.Muhongo,"amesema Naomy.

Meshack Jaraba amesema kuwa, "nimekoshwa na mchango wa Prof.Muhongo alioutoa Bungeni wakati akichangia Wizara ya Elimu hasa upande wa shule zetu kuwa na maabara na maktaba, hili ni jambo muhimu sana. Vijana watasoma kwa vitendo kujua kwa uhalisia mambo muhimu na pia wataandaliwa kuja kuwa wana Sayansi wazuri katika Taifa hili kwa siku za usoni. Na ndio maana Prof.Muhongo anakampeni ya ujenzi wa maabara katika shule za Musoma Vijijini, hili lina faida kubwa sana lazima tuliunge mkono kwa dhati.

"Serikali yetu imekuwa sikivu sana, lazima tuishukuru miradi mingi imetekelezwa chini ya Mbunge wetu Prof.Mubongo na Rais wetu Dkt.Samia ipo miradi ya maji, na tunashukuru sana pia Serikali ikijenga Chuo cha VETA itakuwa neema sasa badala ya watoto kufundishwa magari, umeme wanaweza kufundishwa ufugaji bora na kikawa chuo tofauti kabisa ambacho kitasaidia kuleta mageuzi kwenye sekta hizo muhimu,"amesema Fabian Mafuru.
Mei 17, 2023 bungeni jijini Dodoma, Mbunge wa Musoma Vijijini, Prof. Muhongo akichangia katika bajeti ya Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia alimuomba Waziri wa Elimu, Prof.Adolf Mkenda kwa kusema, "Mimi natoa ushauri cha kwanza Profesa hebu ile Veta ya Musoma Vijijini na nilikueleza ukinipatia mimi VETA itakuwa ya mfano nchini kwa sababu, sitaki VETA ya mambo ya hoteli, mambo ya kutengeneza magari hapana. Mimi VETA yangu itakuwa ya mambo ya kilimo, uvuvi na ufugaji naomba hiyo home work profesa imalizie,"alisema Prof. Muhongo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news