Wakulima wa ufuta Namtumbo watabasamu

NA MWANDISHI WETU

WAKULIMA wa Kata ya Limamu wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma wameibua shangwe kwenye mnada wa zao la ufuta kutokana na kuridhishwa na bei ya ununuzi wa zao hilo iliyopitishwa na wakulima wenyewe katika mnada huo.

Wakiongea baada ya kufanyika kwa mnada huo mkulima wa Kijiji cha Limamu, Otumali Njovu alisema haijawahi kutokea kwa zao la ufuta kumpata mnunuzi kwa bei nzuri ya shilingi 3614 kwa kilo ambayo anaipokea mkulima baada ya kutoa gharama za uendeshaji.

Njovu alidai, bei hiyo itamhamishia shambani ili kujipanga kuzalisha kwa wingi ili mwakani aweze kupata ufuta mwingi utakaompatia fedha za kutosha na kuweza kuhudumia familia yake na kuwasomesha watoto wake sekondari bila wasiwasi wowote.

Naye Adam Daniel Mbunda mkulima wa Kijiji cha Mtakuja katika kata hiyo ya Limamu alianza na kuishukuru Serikali kwa kuwa kidete kuwasimamia wakulima ili waweze kunufaika na mfumo wa stakabadhi ghalani ili kuepukana na madalali waliozoea kuneemeka kupitia nguvu za wakulima.
 
Mbunda alidai mfumo wa stakabadhi ghalani unamsaidia sana mkulima, lakini unapigwa vita na wafanyabiashara waliokuwa wakinunua ufuta kwa bei ya chini na wao kunufaika kupitia nguvu za wakulima,hivyo akaiomba serikali ya wilaya na Taifa kwa ujumla kuusimamia mfumo huo, kwani wakulima wanafurahia mfumo huo kwa kuwa unawasaidia kwa kiasi kikubwa na wanaopinga mfumo huo sio wakulima bali ni wafanyabiashara.
Awali akifungua mnada huo, Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Ngollo Ng’waniduhu Malenya aliwaambia wakulima kuwa katika mnada huo kampuni 17 zmeijitokeza kununua ufuta huo na baada ya mkuu wa wilaya huyo kufungua bahasha ya kila kampuni na kusoma bei ya kununulia ufuta kwa kila kampuni,wakulima hao walizitaka kampuni tatu ya African Harmony’s Trader ambayo iliomba kununua ufuta tani 60 kwa bei ya shilingi 3710,kampuni ya Agro Pulses Export kwa bei ya shilingi 3700 tani zote na kampuni ya Hiyaikery Hyseas tani zote kwa bei ya shilingi 3700 walizitaka kununua ufuta huo.

Mkuu wa wilaya alifafanua kuwa, kutokana na kuzipitisha kampuni hizo za kununua ufuta katika mnada huo aliwaambia wakulima hao kuwa baada ya kutoa gharama za uendeshaji mkulima atapokea kwenye akaunti yake shilingi 3614 kwa kilo na kuibua shangwe na nderemo kwa wakulima hao.

Malenya aliwasisitiza wakulima kutumia fedha watakazopata kujenga nyumba bora,kusomesha watoto shule, kununua mavazi ili kubadilisha taswira ya maisha yao ili kuimarisha familia kuanzia ngazi ya familia alisema mkuu wa wilaya huyo

Hata Hivyo, mkuu wa wilaya huyo aliwataka wakulima hao kutorubuniwa na wafanyabiashara bali wauze mazao yao kupitia stakabadhi ghalani ili wanufaike kwa kupata bei nzuri na serikali inasimamia kupatikana kwa wanunuzi badala ya kuwaachia madalali ambao huwanyonya wakulima.

Zamakanaly Komba, Afisa Masoko wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Songea na Namtumbo (SONAMCU) aliwataka wakulima kuwa makini wakati wa mnada kwa kuangalia bei itakayowafaa katika kuuza zao lao.

Komba alidai minada yote kwa msimu huu wa 2022/2023 na 2023/2024 zitafuata maoni ya wakulima wenyewe waliyoyaomba kupitia vikao halali vya kisheria kuwa minada yote ifanyike maeneo ya wakulima na chama kikuu kimezingatia hilo na kulisimamia ili kuhakikisha minada hiyo inafanyika maeneo ya wakulima wenyewe alisema Komba.

Wilaya ya Namtumbo kwa msimu wa mwaka jana ilipitisha jumla ya minada 12 ambayo kwa bei isiyozidi 2900 mpaka 2800 kwa msimu huo na mwaka huu bei ya mnada wa kwanza umeanza na shilingi 3700 na mkulima kulipwa shilingi 3614 baada ya makato ya uendeshaji hali iliyoibua shangwe na nderemo kwa wananchi wa Kijiji cha Limamu ulipofanyika mnada huo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news