Watakiwa kuhakikisha dawa za tiba zenye asili ya kulevya zinadhibitiwa

NA DENNIS GONDWE

WATUMISHI wa afya katika Mkoa wa Dodoma wametakiwa kuhakikisha dawa za tiba zenye asili ya kulevya zinadhibitiwa ili kuondoa mianya ya dawa hizo kutumika tofauti ya lengo lililokusudiwa na kusababisha uraibu wa dawa za kulevya katika jamii.
Rai hiyo ilitolewa na Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Nelson Buruku wakati akifungua mafunzo ya wasimamizi wa dawa za tiba zenye asili ya kulevya katika hospitali na vituo vya afya vinavyotumia dawa hizo mkoani Dodoma yaliyofanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu Huria Tanzania, Tawi la Dodoma.

Dkt. Buruku alisema “kwa kutambua kuwa ninyi watumishi wa afya ni watu wa awali mnaokutana na wagonjwa na kuwapa matibabu mna jukumu la kuhakikisha dawa za tiba zenye asili ya kulevya zinadhibitiwa ipasavyo ili kuondoa mianya ya matumizi yasiyo sahihi ya dawa hizo kwa jamii.

Hivyo basi, ninawaomba kupitia mafunzo haya ambayo wengine ni kwa mara ya kwanza lakini wapo ambao walishawahi kupata mafunzo haya siku za nyuma kuhakikisha mnayaishi katika utendaji kazi wenu ili kuwezesha matumizi sahihi ya dawa hizi”.

Alisema kuwa dawa hizo zinatumika katika kutibu na kupunguza maumivi. 
“Hivyo, pamoja na faida hiyo, dawa hizo zisipodhibitiwa vizuri huweza kuleta madhara kwa jamii hasa zikitua katika mikono isiyo sahihi. Natoa rai kwenu watumishi mnaosimamia dawa hizi kuepuka vishawishi vitakavyosababisha uchepushwaji wa dawa hizi na kupelekea mzigo kwa nchi kutibu waraibu wa dawa za kulevya,” alisema Dkt. Buruku.

Akiongelea matarajio yake kwa washiriki, alisema kuwa mafunzo hayo yatatoa uelewa wa pamoja.

Alisema kuwa, maazimio yatakayowekwa yatakuwa shirikishi na yatatekelezwa kwa ufanisi ili kulinda afya ya jamii na kulipunguzia taifa janga la matumizi yasiyo sahihi ya dawa za tiba zenye asili ya kulevya.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Dawa na vifaa tiba (TMDA) Kanda ya Kati, Benedict Brashi alisema kuwa mamlaka imetoa mafunzo kwa vituo vinavyotumia na kutunza za tiba zenye asili ya kulevya.

“Mafunzo haya yanahusisha vituo 47, yakijumuisha maeneo ya namna vituo vinavyoweza kununua dawa, kutunza na kutumia. Dawa hizi zinaleta madhara na utegemezi. Mafunzo haya tunapitishana kwenye muongozo wa TMDA unaoshughulikia udhibiti wa dawa hizi ili dawa hizi zisitumike ndivyo sivyo na zinawafikia walengwa” alisema Brashi.

Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Kanda ya Kati inahudumia mikoa minne ya Dodoma, Morogoro, Iringa na Singida ikiwa na jukumu la kudhibiti ubora, usalama na ufanisi wa bidhaa za dawa, vifaa tiba, vitendanishi, tumbaku na mazao yake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news