NA YEREMIAS NGERANGERA
MKUU wa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma,Ngollo Ng’waniduhu Malenya amewasimamisha kazi wenyeviti watano wa vitongoji wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Lusewa kwa tuhuma ya kuhujumu zoezi la kuwaondoa wafugaji katika mamlaka hiyo.
Malenya alifikia uamuzi huo baada ya kusikiliza kero za wananchi wa Mamlaka ya mji mdogo wa Lusewa waliodai zoezi la kuwaondoa wafugaji katika maeneo ya mamlaka hiyo linakwamishwa na viongozi wa mamlaka .
Rajabu Sangana, Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Wilaya ya Namtumbo pamoja na kumpongeza Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo kwa kuanzisha kampeni ya kuwaondoa wafugaji wilayani Namtumbo, katika mamlaka ya mji mdogo wa Lusewa zoezi hilo linakwamishwa na viongozi wa mamlaka kwa kuwasiliana na wafugaji katika kila mpango unaopangwa na viongozi ngazi ya wilaya.
Sangana alimhakikishia mkuu wa wilaya huyo kuwa kila mipango inayofanyika ya kutaka kuwakamata wafugaji hao ,wafugaji hao wanakuwa wana taarifa na mipango yote inayofanyika viongozi hao huwasiliana nao na wafugaji hao hutoweka katika maeneo hayo na baadae hurudi katika maeneo hayo kupitia mawasiliano yanayofanyika na viongozi hao.
Kasmi Thabiti Halidi ambaye ni mkazi wa mamlaka ya mji mdogo wa Lusewa alimthibitishia mkuu wa wilaya huyo kuwa viongozi hao wa mamlaka sio waaminifu kutokana na kutosimamia maamuzi ya vikao na badala yake huwasiliana na wafugaji hatua kwa hatua na kuwathibitishia kuwa hawawezi kuondoka katika maeneo hayo ya Mamlaka na kuathiri maeneo ya kilimo ya wananchi.
Mkuu wa wilaya huyo baada ya kupokea kero za tuhuma hizo kutoka kwa wananchi wao, aliwataka viongozi hao mmoja mmoja kutoa maelezo yao kujibu tuhuma hizo zinazowakabili kutoka kwa wananchi wao.
Alphani Kanduru Ngurukuru, mwenyekiti wa kitongoji cha Zanziba na Shazari Abeid Chikwemba mwenyekiti wa kitongoji cha Ushirika wote kwa pamoja walimwambia mkuu wa wilaya huyo kuwa hawapo tayari kueleza tuhuma zilizoelekezwa kwao ,walimuomba mkuu wa wilaya kufanya uchunguzi ili wakibainika kuwa wenyeviti hao kuhusika na tuhuma hizo sheria ichukue mkondo wake.
‘’Nawasimamisha kazi kupisha uchunguzi,“alisema mkuu wa wilaya ya Namtumbo huku akiwataka viongozi hao kutoa ushirikiano kwa kamati ya uchunguzi atakayoiunda ili iweze kufanyakazi yake bila kumwonea mtu yoyote.
Wenyeviti wa vitongoji waliosimamishwa kazi ni mwenyekiti wa kitongoji cha Lusewa Juma Sandali,Muhamudu Matumbi mwenyekiti wa kitongoji cha Kwizombe,Adamu Kalela mwenyekiti wa kitongoji cha Mchajila ,Shadhari Chikwemba mwenyekiti wa kitongoji cha Ushirika na Alphan Ngurukuru Mwenyekiti wa kitongoji cha Zanziba.
Mkuu wa wilaya ya Namtumbo alianzisha zoezi la kuwaondoa wafugaji katika maeneo yasiyorasmi kwa kuunda kamati iliyowahusisha wananchi wa kijiji hicho ili kuwaondoa wafugaji hao lakini kamati hiyo kwa mujibu wa wananchi hao hawakufanya kazi yao ipasavyo kwa kuwa ilikuwa inahujumiwa katika mipango yake na viongozi hao kwa kuwasiliana na wafugaji katika kila hatua na kuwathibitishia kuwa watawasimamia kuhakikisha kuwa hawaondoki katika maeneo hayo.