NA MWANDISHI WETU
WANANCHI mbalimbali kutoka ndani na nje ya Jiji la Arusha wameendelea kumiminika katika banda la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) ndani ya Maonesho ya Pili ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (TVET) kupata huduma na ushauri wa kujiunga na mafunzo ya elimu ya juu.
Maonesho hayo yanaratibiwa na Baraza la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) yanafanyika kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha kuanzia Mei 16 hadi Mei 22, 2023.
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kinaendelea kuwakaribisha wageni wote kutembelea banda la chuo hiki lililopo uwanja wa Sheikh Amri Abeid kupata huduma mbalimbali ikiwemo maelezo ya kukifahamu zaidi chuo, kozi zinazotolewa, udahili, mifumo ya ufundishaji na ujifunzaji, utafiti, huduma kwa jamii na ushauri wa Kitaalamu.
OUT ni nini?
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) ni Chuo Kikuu cha Umma chenye mamlaka kamili, kinachojiendesha na chenye ithibati, kilichoanzishwa kwa Sheria ya Bunge Namba 17 ya 1992.
Sheria hiyo ilianza kutumika Machi Mosi, 1993 kwa kuchapishwa kwa Tangazo la Serikali Na. 55 kwenye Gazeti rasmi la Serikali.
Kansela wa kwanza alisimikwa rasmi katika sherehe kamili Januari 19, 1994 na kundi la kwanza la wanafunzi lilidahiliwa Januari 1994.
Mnamo
Januari 2007, kufuatia kupitishwa kwa Sheria ya Vyuo Vikuu namba 7 ya
2005, OUT ilianza kutumia Mkataba na Kanuni za OUT (2007) kwa shughuli
zake.
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kinatoa kozi zake za cheti,
Stashahada, Shahada na Uzamili kupitia mfumo huria na masafa
unaojumuisha njia mbalimbali za mawasiliano kama ana kwa
ana,broadcasting, telecasting, correspondence, seminars, e-learning.
Programu za kitaaluma za OUT zimehakikishwa ubora na zinadhibitiwa na
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).
Makao Makuu ya OUT yapo kwa
muda nje ya Barabara ya Kawawa katika Manispaa ya Kinondoni, Dar es
Salaam. Makao makuu ya kudumu yanajengwa Bungo wilayani Kibaha, Barabara
ya Soga, takribani kilomita 4.0 kutoka barabara kuu ya Morogoro mkoani
Pwani.
OUT inafanya kazi kupitia mtandao wa Vituo vya Mikoa
vipatavyo 30; Vituo 10 vya Uratibu, ambapo kimoja kiko Unguja na kimoja
Pemba; viwili vipo Kenya (Egerton na Njoro), moja kipo Rwanda
(Kibungo),Namibia na nyingine Uganda.
Vituo vingine vya Uratibu
wa Ndani vya OUT ni African Council for Distance Education -Technical
Collaboration Committee (ACDE TCC),Centre for Economics and Community
Economic Development (CECED) na SADC Centre of Specialization in Teacher
Education (SADC ODL CoS TE). OUT pia ina Vituo 69 vya Utafiti
vilivyoenea katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Chuo Kikuu
Huria cha Tanzania kinatoa vyeti vyake, Stashahada za kawaida, Shahada,
Stashahada ya Uzamili na Uzamivu kupitia vitivo vyake vitano na taasisi
mbili.
Kitivo cha Sanaa na Sayansi ya Jamii
Kitivo cha Usimamizi wa Biashara
Kitivo cha Elimu
Kitivo cha Sheria
Kitivo cha Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Mazingira
Taasisi ya Teknolojia ya Elimu na Usimamizi
Taasisi ya Elimu Endelevu