Waziri Dkt.Gwajima afunguka mazito mahafali kidato cha sita St.Joseph Cathedral High School

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum,Mheshimiwa Dkt.Dorothy Gwajima amesema, ili kuweza kukabiliana na mmomonyoko wa maadili katika jamii nguvu ya pamoja kati ya wanajamii na Serikali inahitajika huku kipaumbele kikiwa ni kumshirikisha Mungu kwa kila jambo.
Mheshimiwa Waziri Dkt.Gwajima ameyasema hayo Mei 20,2023 katika Mahafali ya 12 ya Kidato cha Sita St.Joseph Cathedral High School yaliyofanyika shuleni hapo Kata ya Kivukoni,Posta jijini Dar es Salaam.

"Serikali inatambua kuna changamoto kuhusu maadili, nami niseme suala la mmomonyoko wa maadili linalopelekea ukatili dhidi ya watoto katika taifa letu na wanakatiliwa kuanzia majumbani, nje ya majumbani na katika mlolongo mzima wa maisha yao na hili linatuharibia watoto pamoja na vijana wa leo ambao ni tegemeo kwa taifa letu."

Sababu

Waziri Dkt.Gwajima amefafanua mbele ya wanafunzi na wazazi kuwa, zipo sababu nyingi ambazo zimekuwa zikichangia suala la mmomonyoko wa maadili.
"Na sababu za hali hiyo ziko nyingi tu baadhi ya sababu hizo ni kuwepo kwa maendeleo haya ya teknolojia. Teknolojia inakuja na mambo ya ajabu, sasa sisi wacha Mungu tujifiche kwenye teknolojia ya rohoni, moyoni maombi na kusali na kumjua Mungu.

"Na kutumia hiyo teknolojia ikusaidie kutumia neno la Mungu. Hiyo engineering ya kumjua Mungu ikikaa sawa moyoni hata upelekwe kuzimu katikati ya mashetani utatoka umesimama mmenielewa watoto?."

Aidha, Mheshimiwa Waziri Dkt.Gwajima amesema, "Inasikitisha sana, jana wakati napita pita huko kwenye mitandao nimekuta wameweka kitu bado nakifuatilia kama ni kweli, lakini kwa teknolojia ya leo huwezi kushangaa wanatengenezwa hata mabinti wazuri wa kimfumo wa roboti.

"Watatengenezwa na wanaume wa kimfumo wa roboti, hivi Sasa kama tunaanza kuoa maroboti tuiweke ndani, kama tunaona wengine wanafunga ndoa na wanyama muanze kuelewa kwamba shetani yupo na amejiandaa kuvuruga mpango wa Mungu.
"Ninyi mliotokea kwenye mpango wa Mungu shikeni neno hilo mkijua mmemaliza kusoma mnaachiwa kwenda kwenye vyuo vikuu kule nako (shetani) ameshaharibu ndio maana Serikali tunaweka madawati ya jinsia, madawati ya ulinzi wa mtoto.

"Mmeandaliwa kwenda kupambana kwenye maeneo mengine mnaweza kupambana na silaha pekee mnayoondoka nayo ni yale mliyofundishwa hapa, lakini roho yako na moyo wako ushikamane na Mungu huo ndio urithi pekee mnaoweza kuwauzia watoto wenu. Watoto wenu hoyeee..."

Mila na desturi

Waziri Dkt.Gwajima amesema, sababu nyingine ni kuwepo kwa changamoto ya mila na desturi zenye madhara katika jamii mbalimbali. 
"Lakini, kuna changamoto ya kuwepo kwa mila na desturi zenye madhara umaskini katika baadhi ya familia na migogoro isiyoisha katika familia yetu. 

"Hizi shetani anazitumia akishapiga familia ikawa na migogoro wale watoto neema ya malezi na makuzi inapotea unakuta wapo mitaaani wengine wanaanza majukumu makubwa kabla ya umri wao, umaskini tunapambana nao kwenye hotuba yangu ya bajeti Mei 18, 2023 niligusia programu za uwezeshaji wanawake kiuchumi kwa sababu ndio wanaokatiliwa na ukishamkatili mama moja kwa moja umemkatili mtoto.

"Na unapoona mtoto anakatiliwa ujue kuna mama katangulia kukatiliwa, kwa hiyo haya tunayoyaongea sasa lengo ni kuwakomboa wale wanaonyanyaswa kwa sababu ya umaskini ili wasiweze kunyanyaswa, lakini mila na desturi nimesikia mtangulizi wangu amesema sheria tukazifanyie kazi hakika tuna Waziri wetu wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndubaro yupo tayari kuingia na marekebisho ya sheria karibu 29.

"Na sheria nyingi kati ya hizo zinagusa masuala yanayojielekeza kumlinda mtoto na sheria yetu ya mtoto nayo imeshachukuliwa maoni tutayawasilisha bungeni ili tukayarekebishe, kwa hiyo Serikali inapambana na kwenda kuzifanyia kazi changamoto zote mtu kuyumba hadi mmomonyoko wa maadili unambeba na yeye.
"Pengine wazazi kushindwa kutoa huduma muhimu hata kwa watoto wa kike na kutelekeza familia ya watoto ni tatizo ambalo tunaungana na wenzetu wa masuala ya Ustawi wa Jamii, wanasaikolojia ili kuoana tunafikishaje hizi huduma karibu zaidi na jamii, kama ambavyo huduma za hospitali na nyingine zizidi karibu na jamii na hizi za msaada wa kisaikolojia kwa kushirikiana na viongozi wa dini.

"Wajue wanakimbilia kituo gani cha karibu kwa ajili ya kuongeza nguvu ya kutengamaa ile familia na mwisho kabisa ikishindikana tujue tuwaokoeje watoto na vituo vya kulelea watoto yatima na wengine ambao wanaishi mazingita hatarishi tunavyo.

"Tatizo hapa jamii haielewi hata kama wanaogombana ni baba na mama hawa jamii wanaozunguka familia hii na wemyewe wawe tayari kutoa taarifa.

"Lakini wakiona jambazi au kibaka mwizi kapita wanaungana mtaa mzima kutoka na silaha, hii tubadilishe mind set tukiona mtoto anatangatanga bila malezi nyumba hii wanagombana,nyumba hii wanayatima tutoe taarifa.
"Na taarifa zinatolewa wapi? Sasa hivi tuna namba 116 muda wowote unapiga saa 24 unapiga unasema nanusa harufu ya ukatili sehemu mtoto anakatiliwa sababu gani, yatima, hakuna matunzo,Ustawi wa Jamii wanafika lile eneo na tuna kamati za ulinzi wa mtoto na wanawake ambayo wajumbe wake ni viongozi wa dini tunakwenda kuimarisha hii mifumo vijijini, kwenye kata, mitaa.

"Kuwa na kamati ni suala jingine, lakini jamii je, inaelewa kimbilio kama imeshindikana kwenye ibada imeshindikana, huku kwenye ndugu ile kamati inatuambia hapo ndipo kuna jukumu la kuwabeba wale watoto inapoanzia sasa wakishagombana miaka mitano huwa wanarudi kutafuta watoto, baba anataka watoto, mama anataka watoto ulimwachia nani?.

''Kwa hiyo masuala haya ni kuendelea kuelimisha kwa kushirikiana na viongozi wetu wa dini ili watoto wetu wasiingie kwenye changamoto ya maadili, lakini vijana wanaingia wanaiga tamaduni za nje. Kuna baadhi wanapigwa na mmomonyoko wa maadili wengi wanaingia kwenye uhalifu, wanavuta madawa ya kulevya, wanakuwa wezi na wala rushwa wanakuja kukutana sasa na masuala ya kuingizwa kwenye vitendo hivi visivyo na staha katika makuzi yao ya kijinsia.
"Sasa hapa mtu akishafika hapa kumtoa inakuwa gharama kubwa maana yake ameshaingia huko na ameharibika na safari yake inaweza kuharibika. Niwaombe msiingie huko kwa sababu ya hela, magomvi ya wazazi kwa sababu yoyote."

Ukatili unatisha

Mheshimiwa Waziri Dkt.Gwajima amefafanua kuwa, licha ya jitihada mbalimbali ambazo zinafanywa na Srikali kwa kushirikiana na wadau bado matuko ya ukatili wa kijinsia ni mengi.

"Ndugu washiriki matukio ya ukatili wa kijinsia ni mengi, takwimu za Jeshi la Polisi mwaka 2022 kuanzia Januari hadi Desemba kwa watoto matukio yalikuwa 12,163, mwaka 2021 yalikuwa matukio 11,499. Kwa hiyo bado tuko kwenye maelfu na tunaona ni kama yemeongezeka matukio 669 hayo ni machache wengi hawasemi.

"Waliokuwa wanasema ilikuwa asilimia 12 tu, kwa hiyo tunapoona yanaongezeka ni mifumo imeimarika na watu wanathubutu wanatoka wanasema sasa usiogope kwamba yanaongezeka yapo na data zipo na pia yanachangiwa na nguvu za mitandao na wengine hawajasema wanakatiliwa wanasema samehe saba mara sabini.
"Kumbe wanatengeneza roho ya ukatili, kwa hiyo wanaye mkatili anakuja kuwakatili katika haya 12,163 waliobakwa ni 6,335, mwaka jana 5,810 lakini ukigawanya asilimia 60 yanatokea nyumbani aliko baba,mama, mjomba, binamu, na mdogo wako tena penye maendeleo watoto wanachumba chao cha kulala ndio wanakatiliwa sana.

"Wageni wakija walale na mjomba wao au binamu yao au baba yao mdogo ndiko yanakotengenezwa, ulawiti 1,557. ukumbuke hizi ni takwimu ambazo zimeripotiwa sasa.

"Wengi hawajaripoti wameficha, sasa wewe ni yatima umefanyiwa hicho kitu halafu umetunzwa mle unaenda kumshitaki nani, taarifa yenyewe ya habari hujawahi kusikia wanasikiliza wao unaenda kumwambia nani.

"Kwa hiyo yanafanyika nyumbani kwa asilimia 60 tunawafikiaje? Mambo yanafichwa kama hayatokei kwako yanatokea kwa jirani. Mtoke hapa mkawe mabalozi kwa jamii mkaielimishe jamii juu ya madhara haya yanatokea nyumbani.
"Wewe mtoto usifiche unapofanyiwa haya, wengine wanafanikiwa na kufika mbali wametokea katika madhira hayo wanageuka na kuwafanyia wengine kwa sababu walifanyiwa hayo kwa hiyo tunapita kwenye mnyororo ambao wamepita mkienda mtusaidie kuyasema hayo. ndugu zangu hili la ukatili wa kwenye mtandao UNICEF (Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa) kwa kushirikiana na Serikali yetu tukafanya utafiti hali ikoje kwenye mitandao.

"Mwaka 2022 tukabaini asilimia 67 ya watoto walio kati ya umri wa miaka 12-17 wanatumia simu, unatumia simu akili yako ndogo unapekua inakupeleka unakutana na vitu vinavyokuzidi uwezo unaona vitu vya ajabu. 

"Unatumia kompyuta na matokeo yake asilimia nne ya watoto hao wanaotumia mitandao hiyo wamewahi kufanyiwa ukatili wa vitendo vya kingono na kisaikolojia hili ni tatizo. Mtoto anakuwa anavipata vifaa hivi kutoka kwa wazazi au ndugu wa karibu na hivyo kuongeza wigo wa watoto kufanyiwa ukatili.

"Anajifunza anataka akajaribishe, anajaribisha kwa nani kwa wadogo zake, nanyi mnapokwenda kwenu kuna wadogo zenu mkawaambie wazazi wasiwape simu watoto, takwimu zinasema watoto wanaotumia hii mitandao kati ya miaka 12-17 ni asilimia nne wamefanyiwa ukatili. Mentality inaposhika anayaona ya kawaida. 

"Mila na desturi bado zinawakabili watoto wetu na kuwahangaisha ukiangalia mwaka 2015/2016 kwenye taarifa ya utafiti wa afya na uzazi na mtoto na viashiria vya malaria hapa kuna masuala ya ukeketaji, mtakutana nayo mnakwenda kwenye dunia ambayo mtaambiwa hii ni mila, mila ambayo itakuacha umepata maumivu, magonjwa, ulemavu, umepoteza damu safari na ndoto yako zimeishia hapo," amesema Waziri Dkt.Gwajima.

Waziri apongeza

Wakati huo huo, Mheshimiwa Waziri Dkt.Gwajima amezipongeza taasisi za dini nchini ikiwemo Kanisa Katoliki katika utoaji wa huduma za afya na elimu kwa watoto bila ubaguzi wa kiimani. 
"Hongereni aana Kanisa Katoliki. Serikali inafarijika sana kuona shule zinazomilikiwa na taasisi za dini nchini, binafsi zinaungana na serikali katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu hususani lengo namba nne la kuendeleza elimu bora kwa watoto, lakini pamoja na mikataba ya kikanda na kimataifa ya haki na ukuzaji wa mtoto ambayo nchi imesaini na kuridhia kwa maana kwamba hatuendi peke yetu tunakwenda na Dunia yote.

"Nimefurahi kusikia wastani wa wanafunzi 230 wanaomaliza kidato cha sita hapa St.Joseph Cathedral High School kila mwaka wanafunzi hawa wanakuwa na sifa za kuendelea na masomo ya elimu ya juu. 

"Nimesikia daraja la kwanza la pili hapa na mmeongoza mashindano mengi ya mitihani kama mlivyosema wenyewe hakika mnatisha sana.
"Sasa kutisha huku nimeambiwa huko vyuoni pia wanawasifia sasa mkaendeleze utisho huo hasa kwenye Dunia ya sasa ambayo tunatafuta watu watakaotisha kwa ucha Mungu sio kwa madivisheni tu. Na ninyi sina shaka nina imani tutaanzisha kombe la wanaotisha kwa maadili tuwashindanishe huko vyuo vikuu.

"Ninaimani hii inatokana na jitihada zenu wanafunzi wenyewe katika kujisomea, walimu kutoa mafunzo yenye tija na tabia njema na maadili kwa watoto wetu. Ni ngumu kufanikisha jambo hili iwapo hakuna mawasiliano na umoja.

"Huu umoja unaotoka kwa walimu kwenda kwa wazazi ni kiungo kikubwa kinachofanya usikivu na uadilifu maana mnawapigia wazazi kutoka nyumbani kwao na kuangalia wayaendeleze yale mnayofundisha hili kwa kweli ni la kuigwa sina uhakika liko shule ngapi hapa Tanzania, lakini mimi kama Waziri mwenye dhamana ya Watoto nitawasiliana na wenzangu wa elimu nione wapi panalega lega ili hii experience hii iende kote hongereni sana.

"Naomba muendeleze ushirikiano huu na malezi bora ili kuzalisha kizazi chenye kumcha Mungu na chenye maadili yanayofaa katika taifa letu,"amesisitiza Waziri Dkt.Gwajima.

Wanafunzi wafunguka

Wakisoma risala kwa niaba ya wanafunzi wenzao, wanafunzi Kersten Mbuligwe na Nancy Kitena wamesema,kutokana na shule yao ya St.Joseph Cathedral High School kujitahidi kuweka mazingira mazuri ya kujifunzia, changamoto za ndani hazikuwa nyingi. 
"Lakini tangu kumaliza mitihani yetu ya taifa hadi sasa tumeishi kwenye jamii zetu tumekutana na changamoto. Changamoto hizo ni kama upatikanaji wa vitambulisho vya taifa ambavyo vimekuwa na mchakato mkubwa wa upatikanaji jambo ambalo limesababisha wahitimu kushindwa kukamilisha mchakato wa chuo ikiwemo mikopo.

"Lakini changamoto ya pili ni changamoto ya upatikanaji wa mikopo kwani mchakato ni mrefu ambao pia huhitaji fedha nyingi.

Kuhusu maadili

Wanafunzi hao kwa niaba ya wenzao wamesema kuwa, "Pia pamekuwa na changamoto ya mmomonyoko wa maadili kwa vijana nchini mwetu hasa utandawazi umechangia kuleta maovu kama makundi yanayohamasisha mapenzi ya jinsia moja hasa kwa vijana na watoto.

"Ndugu mgeni rasmi ili kukabiliana na vitendo hivi ni lazima wazazi na walezi warudi katika msingi wa malezi shirikishi ili kushirikiana kuwalea watoto katika msingi bora na maadili mema.

"Viongozi wa dini pia wafundishe malezi bora na kuwalea watoto na vijana katika misingi. Serikali pia inawajibu wa kuweka sheria kali dhidi ya mapenzi ya jinsia moja ili kuyakomesha.
"Vijana wanapaswa kupewa semina na mafunzo mbalimbali ya kuwaandaa vyema, lakini pia wahitimu warahisishiwe upatikanaji wa vitambulisho vya taifa ili kiwezesha shughuli zao na maandalizi ya kujiunga na vyuo pamoja na kuwapatia wahitimu mikopo."

Shukurani

"Ndugu mgeni rasmi tunapenda kukushukuru kwa kuhudhuria sherehe yetu na pia tunaushukuru uongozi wa shule, walimu na wafanyakazi wasio walimu, wazazi na walezi kwa mchango wao wote katika kufanikisha hatua hii.

"Mmetupatia elimu na ujuzi katika kukabiliana na dunia ya sasa hata kupata mafanikio, Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki St.Joseph Cathedral High School.

"Shule yetu imekuwa ikitoa huduma ya elimu tangu mwaka 2010 ikiwa na michepuo mbalimbali. Shule inafanya hivyo ikiwa na malengo ya kuandaa viongozi wawajibikaji na kujitahidi kufikia ubora wa viwango vya juu. 

"Sambamba na malengo hayo ni kauli mbiu ya shule kukuza vijana wenye fadhila na waaminifu pia tunachokifanya ni kwa ajili ya Mungu na taifa letu."
Wamesema, wanafunzi 230 ambao wanahitimu kidato cha sita mwaka huu walipokelewa St.Joseph Cathedral High School walipokelewa shuleni hapo Machi 18, 2021 wakianza masomo ya kidato cha tano katika michepuo tofauti tofauti. 

"Tunashukuru Mungu leo Mei 20, 2023 tunafanya mahafali ikiwa ni ishara ya kuhitimu ngazi hii ya elimu kwenda ngazi nyingine."

Pia wamesema, katika safari yao ya miaka miwili shuleni yapo mengi ambayo wamekutana nayo mengine ya kuwatia moyo na mengine ni changamoto. 

"Mwanzo wa safari yetu tulijiwekea malengo ya kufaulu kwa kiwango cha juu na nidhamu sambamba na malengo hayo tulitumia njia mbalimbali ikiwemo ushirikiano baina yetu sisi kwa sisi na walimu, viongozi wa shule pia na wazazi na walezi ili kuweza kupata ufaulu.

"Tulitilia mkazo suala la utii hata kujikita kuomba sana kwa Mungu kupitia mtakatifu Yoseph msimamizi wa shule kwani tunaamini kwamba bila Mwenyezi Mungu hakuna tunaloweza kulifanya likafanikiwa.

"Katika kukamilisha malengo yetu, walimu na viongozi wa shule wamekuwa na mchango mkubwa moyo kwa kujitolea bila kuchoka walionao walimu wetu ambao wametufundisha na kututia moyo. 

"Shule pia imejitahidi kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya kujifunza ikiwemo madarasa mazuri, vitabu vya kutosha, maktaba ya kujisomea, chakula bora, malazi na hata kutupatia afya afya na nguvu ya kusoma yote haya tunasema Asante.

"Utayari wa wahitimu hawa kujifunza pamoja na usikivu na nidhamu yao vimeweza kufanya safari ya miaka miwili kuwa ya amani na utulivu kitu ambacho tunaamini kimetufanya kutoka hapa tukiwa na ufaulu wa kiwango cha juu.
"Pamoja na masuala ya elimu shule imekuwa chachu ya kutuandaa sisi kuwa viongozi wazuri wa baadae kama yasemavyo maono ya shule 'kuandaa viongozi waadilifu'.

"Mara kwa mara wahitimu wamepewa semina za elimu na maadili ili kupanda mbegu ya maadili mema shule imefundisha uwajibikaji na kuamini viongozi ambao huchaguliwa kwa njia ya kidemokrasia shuleni hapa kuweza kuongoza wenzao bila uwepo wa walimu au walezi na hivyo kujenga utamaduni wa uwajibikaji, utendaji kazi kwenye msukumo kutoka ndani ya nafsi.

"Safari yetu imekuwa ya mafanikio ambapo tunamshukuru Mungu sana kutujali kitaaluma tumeweza kufanya mitihani mingi ya ndani na nje ya shule ambayo ilitujenga na kutupa uimara tumeweza kufanya mitihani kama MOCK, mitihani ya umoja wa shule za Kikatoliki Dar es Salaaam na Pwani na mitihani mingine ya ushirika ambayo yote tuliweza kufaulu kwa daraja la kwanza, la pili na wachache daraja la tatu.

"Tuliweza kushiriki katika mashindano ya taifa ya midahalo na kutoa muongeaji bora kwa mkoa wetu kwa ujumla, tulishiriki mashindano ya uandishi wa insha yanayoandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania na kushinda nafasi ya kwanza. 

"Na katika mashindano ya insha ya Manispaa pia tulishika nafasi ya kwanza, lakini pia katika mashindano ya ubunifu wa sayansi ya Young Scientists Tanzania na kushinda nafasi ya pili na mengine mengi.

"Tofauti na taaluma tuliunda vikundi vya sanaa kuendeleza vipaji vyetu. Ambavyo tulifanya kupitia utaratibu wa klabu ambazo hufanyika hapa shuleni. Tuliandaa vikundi vya maonesho kama vikundi vya uchoraji na kadhalika. 
"Shule haikutupatia elimu ya darasani tu, bali pia mafundisho ya uhalisia wa maisha na namna ya kuishi vyema na watu. Tunahimizwa sana juu ya umoja, upendo na moyo wa kujitolea kwa ajili ya wengine. Kutokana na mafundisho hayo tuliweza pia mara kwa mara kufanya matendo ya huruma hapa shuleni tarehe 10 mwezi wa 9 kila mwaka.

"Tulitembela vituo vya wahitaji wakiwemo wazee pamoja na watoto. Sisi wahitimu tumeendelea kuwa na moyo huo huo hata hivi tunavyoongea tumefanya matendo ya huruma baada ya kumaliza mitihani yaetu ya Taifa na tunaahidi kuendelea na moyo huo huo na tunawasihi waliobaki wazidi kufanya hivyo,"wamefafanua wanafunzi Kersten Mbuligwe na Nancy Kitena kwa niaba ya wenzao.

Mkuu wa Shule

Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya St.Joseph Cathedral High School,Sr. Theodeta Faustin ameiomba Serikali kutazama upya namna ya kunusuru malezi kwa vijana na watoto nchini.
"Ndugu mgeni rasmi, kwa ufupi kabisa hali ya mmomonyoko wa maadili usipotazamwa upya ni hasara sana kwa taifa na kizazi kijacho. Mara nyingi tabia au mwenendo ukipotea maana yake kila kitu kimepotea huwezi kupata chochote wala afya nzuri wala mahitaji yako ya msingi.

"Naomba nitoe wito kwa wazazi kwamba, malezi bora ni mhimili wa maisha ya mtoto kama unataka ufanye uwekezaji kwa mtoto wako leo mjenge katika malezi bora lazima uwe na muda na mwanao unampa nasaha za kidini, mafundisho ya kiroho kama neno la Mungu lisemavyo kuwa mlee mwanao katika njia impasayo naye hataiacha hata atakapokuwa mzee Methali 22:6.

"Kwa watoto wetu wa kidato cha sita tumesemezana sana kwa miaka miwili, tunaamini masemezano hayo yamekuwa mbegu njema katika kuwasaidia kwenye safari yenu ya maisha tukumbuke huu ni wakati wa kutathmini juu ya nidhamu binafsi self despline hili ni nguzo muhimu sana katika maisha ya mwanadamu.

"Ukifika chuo kikuu ukamsahau Mungu, sauti ya wazazi na walezi ukaingia kwenye makundi mabaya hata kama utamaliza chuo kikuu ukiwa na daraja la kwanza utabaki na masononeko makubwa sana moyoni. Tunaamini hilo halitatokea kwenu.

"Sisi tunawapenda sana tutaendelea kuwaombea na kuwaweka mioyoni mwetu, malezi yetu ya miaka miwili naomba pia myaweke kwenye mstari wa Biblia, 'mwanangu yasikilize mafundisho ya baba yako wala usiache sheria ya mama yako ndipo utakapokwenda katika njia yako salama wala mguu wako hautajikwaa, Methali 3:23."

Mkuu huyo wa Shule ya St.Joseph Cathedral High School amefafanua kuwa,shule hiyo ambayo ipo chini ya Mtakatifu Yoseph zilianzishwa kwa lengo maalumu la kutoa elimu bora ngazi zote kuanzia chekechea,msingi,sekondari na kidato cha tano na sita ambayo ndio wanaadhimisha mahafali yake leo.

"Kwa sababu hiyo ni matumaini yetu wahitimu wa shule zetu wanatambua kwamba muda wao wa kusoma katika shule zetu sio muda tu wa kukua na kutambulika. 

"Bali tunategemea watambulike kokote wanakokwenda kwa matendo uadilifu yanayowafanya wawe tofauti kabisa na wengine. 

"Hivyo wanatakiwa waoneshe maisha yao na tunu zetu za msingi ambazo zitawaonesha kila siku na tunaziishi ambazo ni kumcha Mungu, uwajibikaji, kufanya kazi kwa bidii, ukweli, uadilifu utunzaji wa muda, heshima binafsi na kwa wengine,"amefafanua Mkuu wa shule hiyo,Sr. Theodeta Faustin.

Idadi ya Wanafunzi

Mkuu huiyo wa shule amebainisha kuwa, kati ya wahitimu hao 230 wasichana 83 na wavulana 147 ambao ni wahitimu waliolelewa vizuri katika bidii, nidhamu na taaluma.

"Wahitimu hawa wapo katika michepuo ya Sayansi,Biashara na Sanaa kama ifuatavyo ECA,PGM, HGE, HGL, HKL, CBG, CBM na EGM, haya ni mahafali ya 12 ya kidato cha sita.

"Mahafali yetu ya kwanza yalikuwa mwaka 2012 kwa miaka 12 sasa wanafunzi wanahitimu kidato cha sita kila mwaka ni kati ya 230 hadi 250 kila mwaka tunamshukuru Mungu sana licha ya wingi wao wote wanafaulu sana katika ufaulu wa daraja la kwanza, la pili na baadhi yao wachache daraja la tatu.

"Lakini wote wenye sifa za kujiunga na elimu ya juu. Kama hiyo haitoshi tumekuwa tukipata taarifa ya matokeo mazuri wanapokuwa vyuo vikuu.
"Msingi wa malezi bora wananaopata shuleni unawajengea uwezo wa kujimudu na kujiongoza katika hatua mbalimbali za maisha yao ambayo yanatokana na nidhamu ambayo tumekuwa tukiwasisitiza kama walimu na walezi wao.

Kuhusu malezi

"Ndugu mgeni rasmi licha ya mafanikio hayo changamoto ni nyingi katika utoaji wa elimu kwa sasa. Kwanza tunaipongeza Serikali kwa kuanza mchakato wa uboreshaji wa elimu kwa namna ambavyo makundi mbalimbali ya wadau yameshirikishwa katika kutoa maoni.

"Kwa kuwa wewe ni mtendaji mkuu katika wizara hii muhimu inayohusu familia na malezi yapo mambo ambayo kama walimu na walezi tunakutana nayo kila siku na tunaomba tukushirikishe kwani kwa uwezo wako unaweza kufanya kitu.

"Kuhusu malezi kwa miaka ya hivi karibuni kumeibuka kwa wimbi kubwa la kumomonyoka kwa maadili katika jamii yetu kuanzia watoto wadogo hadi watu wazima, kumekuwa na kilio kikubwa kwenye jamii kila mmoja akimlaumu mwingine sisi ambao ni walimu tunakutana nayo na hali hii imekuwa ikileta changamoto katika ufundishaji.

"Tunaona kwamba changamoto hii inachangiwa sana na kulega lega kwa taasisi ya familia, zipo familia nyingi zinazoonekana baba na mama wako pamoja, lakini sivyo. Lakini pia wazazi wengine wametengana kabisa kila mmoja na maisha yake, wazazi kugombana mbele ya watoto wanakuwa wapo katikati na hawana mifano mizuri katika maisha yao.
"Madhara ya mtoto anayekulia katika mazingira haya ni makubwa kwake kiutu na kijamii ndio maana kwenye jamii yetu tumekuwa na watoto na vijana waliokengeuka sana, wote tunajua kwamba msingi wa malezi bora unawekwa na wazazi nyumbani, shuleni tunaendeleza tu kumwagilia maji mbegu hii ambayo inakuwa imepandwa na wazazi.

"Kwa sasa ukweli huo umebaki kwenye fikra kwa kuwa mtoto anafika shuleni anategemea kufundishwa masomo na pia yale ambayo wazazi wameacha na kwa kidato cha tano na sita mambo ni mengi, lakini pia wapo wazazi ambao kwa sababu mbalimbali za kimaisha hawana muda kabisa na watoto wao.

"Wanawapatia watoto vifaa vya kielektroniki wakiwa wadogo sana, sio jambo la kushangaza leo kuona mtoto wa miaka sita akiwa na simu na anaweza kufuatilia yaliyoko kwenye mitandao ya kijamii. 
"Tunajua wote kwamba kifaa kama simu licha ya kuwa na faida kubwa kwenye jamii, lakini pia matumizi mabaya ya simu yamesababisha mmomonyoko wa maadili katika jamii yetu licha ya kujua ukweli huo badi wazazi huwapatia watoto simu.Maudhui wanayoyapata kwenye simu yanaharibu ubongo wao mchanga."

Ushauri

"Ushauri wetu kwa serikali ni kuona namna ya kusaidia suala lihusulo kutazama upya sheria zinazohusu talaka kwa kuwa kama tulivyosema awali kuparanganyika kwa wazazi kuna athari kubwa. 
"Sheria ya talaka inamsaidiaje mtoto baada ya talaka kwamba ni nani anajua mtoto ataishije baada ya talaka, tatizo sio kupata pesa au mali, nani anamlinda mtoto huyo dhidi ya nyuma ya jamii. Pia, Serikali ione namna ya kushirikiana na mashirika ya dini katika kunusuru hali ya familia leo.

"Suala la matumizi ya simu katika umri mdogo litazamwe upya na kuwekewa sheria, Serikali ione nini cha kufanya kuokoa watoto walio katika umri mdogo sana wanaopewa simu na watoto wao.

"Ili kusaidia tunashauri pia kuanzishwa kwa somo la maadili shuleni kuanzia elimu ya awali, ukitazama mitaala yetu kama hakuna somo litakalomsaidia mtoto kujua tunu za msingi, kwani somo hili litasaidia kukuza kizazi chenye elimu na maadili.

"Tunajua mabadiliko tunayoyataka hayaji kwa ghafla, tunajua kwamba yanahitaji uwekezaji mkubwa. Lakini sisi tulio walezi wa watoto tunaamini kwamba hatujachelewa.

Watoto wa kiume

"Ndugu mgeni rasmi kumekuwa na changamoto kwa malezi ya mtoto wa kiume, hivi sasa miaka ya hivi karibuni kumeanza kutokea kwa vijana wanyonge na wanaopenda kuonewa huruma, wasiojiamini na wanyonge sisi tulio kwenye elimu tunaona mabadiliko haya yanakuja kwa kasi kubwa.
"Maadiko matakatifu mathalani Biblia inamuonesha mwanaune kama mlinzi na nguzo ya familia hofu yetu ni kubwa juu ya hali hiii, tunajiuliza familia zitalindwa na nani kama nguzo ya familia tunaamini kwamba tatizo hilo kwa kiasi kikubwa limesababishwa na ombwe la wazazi ambao ni wababa wanashindwa kuwajenga kama tunavyosisitiza malezi na ulinzi kwa mtoto wa kike.

"Tunapaswa kubadilika pia na kuanza upya kufanya hivyo kwa watoto wa kiume. Bila kuweka malezi ambayo ni balance itakuwa ni changamoto kubwa kusimamisha familia,"amefafanua Mkuu wa Shule ya St.Joseph Cathedral High School,Sr. Theodeta Faustin.

Wazazi wanasemaje?

Akizungumza kwa niaba ya wazazi,Mbunge wa Jimbo la Muleba Kusini, Dkt.Oscar Ishengoma Kikoyo amewataka wazazi kuedelea kuwalea watoto hao katika maadili mema ili waweze kuzifikia ndoto zao maishani.

"Msidhani kwamba wamemaliza basi yamekwisha, ndiyo kazi imeanza. Walikuwa wanalelewa na sheria na kanuni wanapokwenda chuo kikuu kule ni uwanja wa fujo. Hakuna sheria tena, hakuna kengele ni wewe mwenyewe unaweza ukaamua uingie darasani au usiingie au ufuate sheria."

"Wazazi lazima tuendelee kuwalea hawa watoto kwa maadili mema, nimewaona vijana wengi mimi nafundisha International Transport Laws pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nawaona wakati mwingine naangalia vijana nasema kweli hawa walidhamiria kuja chuo ama walisukumwa kuja chuo?.

"Lakini wale vijana mnaomaliza niwaambie kazi ndio inaanza hapa mlikuwa mnasukumwa kule unakwenda kujisukuma wewe mwenyewe, wazazi tuendelee kuwaombea vijana wetu huko wanakokwenda wasije wakarudi nyuma kwa sababu ya uhuru watakaoukuta huko.
"Ndio maana shule hii ninaiamini mtoto wa kwanza alipomaliza,nikaleta wa pili na wa tatu na Mungu akijalia nitaleta wa nne kwa sababu ninaiamini kwa malezi yake mazuri tunashukuru kwa kazi kubwa ambayo mnaifanya mkuu wa shule najua uwajibikaji wako hapa hakuna mzaha mzaha, naomba muendelee kukaza kamba wembe uwe ule ule na wazazi muendelee kukaza kamba." 

Maadili

"Wazazi tumekuwa tukiwaharibu watoto sisi wenyewe kwa malezi ambayo hayafai kabisa sijui tunakwenda wapi.Ni changamoto kubwa sana tuliyonayo wakati huu na kipindi hiki kupelekea mmomonyoko wa maadili hasa consumerlism, hii ni hali ambayo unatumia pesa kwa sababu mzazi anakupa pesa, au mzazi anatumia kwa sababu ana kipato unaweza ukanunua chochote unachotaka.
"Lakini sisi enzi zetu sisi hatukuwa nayo, hivyo tuendelee kuwalea watoto wetu katika maadili mema,"amefafanua Mheshimwa Dkt.Kikoyo kwa niaba ya wazazi shuleni hapo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news