Waziri Dkt.Gwajima azindua programu ya kuwawezesha wanawake

NA MWANDISHI WETU
WMJJWM, Dodoma

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amezindua Programu ya Jinsia ya ANAWEZA itakayowawezesha wanawake kiuchumi na kushiriki katika nafasi mbalimbali za uongozi kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango leo Mei 31, 2023. 
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothh Gwajima akibonyeza kitufe kuashiria uzinduzi wa Programu ya kuwainua wanawake kiuchumi "ANAWEZA" kwa niaba ya Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango katika hafla iliyofanyika jijini Dodoma Mei 31, 2023. Kushoto ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Riziki Pembe.

Akizungumza kwa niaba ya Mhe. Dkt. Mpango wakati wa uzinduzi huo, Waziri Dkt. Gwajima amesema Programu hiyo itakayogharimu fedha za Kimarekani milioni 7.5 kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC), inaendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 , mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano, Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya 2050, Sera ya Maendeleo na Jinsia ya 2000 na Sera ya Jinsia ya 2016 ya Zanzibar.
"Uzinduzi wa Programu hii inayolenga kumkomboa mwanamke kiuchumi, imekuja kwa wakati muafaka ambapo Tanzania ipo katika jitihada za kumkomboa na kumuinua mwanamke kiuchumi. Tanzania ni mojawapo ya Mataifa yanayotekeleza malengo ya Jukwaa la Kimataifa ya Kukuza usawa wa Kijinsia. Katika hili Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kinara wa utekelezaji wa Jukwaa hili hususan kuhusu Haki na Usawa wa Kiuchumi."
Waziri Dkt. Gwajima ameongeza pia, pamoja na kuwa Wanawake ni tegemeo kubwa katika Taifa, wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mila na destruri zenye madhara, elimu duni, ukosefu wa mitaji na stadi za ujasiriamali ambapo Serikali imechukua hatua ya kuboresha kipato na kuondoa umaskini kwa wanawake na wanaume nchini.

Akizitaja baadhi ya hatua hizo, amesema ni pamoja na fursa za mikopo ikiwemo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Mamlaka za Serikali za Mitaa, Mikopo ya Mfuko wa Maendeleo wa Wanawake na kupitia madirisha mahsusi kwenye Benki mbalimbali.
Amesema hatua nyingine ni uanzishwaji wa majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi katika mikoa yote Tanzania Bara ambapo wanawake wameendelea kupata taarifa na fusa za kiuchumi.

Aidha, Dkt. Gwajima amebainisha kwamba programu hiyo inayotekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali na Sekta binafsi lengo ni ifikiapo mwaka 2026 hali ya Wanawake iwe imebadilika kwa kiasi kikubwa. 
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Mary Senyamule amesema umefika wakati wanawake wanatakiwa kuthubutu wenyewe bila kusukumwa kushiriki katika nafasi mbalimbali, hivyo programu hii itakuwa chachu ya kuwabadilisha fikra zao.
Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Riziki Pembe amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini mchango wa wanawake kutokana na uwezo walionao katika uongozi kwenye nyanja zote.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri (ATE) Sussane Ndomba ambapo Programu hiyo itatekelezwa chini ya Chama hicho, amebainisha kwamba Chama hicho kinajali usawa wa kijinsia hasa mahala pa kazi na tangu mwaka 2016 chama hicho kimekuwa na programu ya mafunzo kwa wanawake 274 hadi sasa.
Akieleza lengo la mradi huo utakaotekelezwa kwa miaka 5, Mkurugenzi wa Shirika la Fedha la Kimataifa IFC Kanda ya Afrika Mashariki Jumoke Jagun Dokunmu amesema usawa wa kijinsia utafikiwa iwapo kutakuwa na usawa wa kiuchumi kati ya wanawake na wanaume, ili wanawake waweze kushiriki vema nafasi za uongozi.
Nao Baadhi ya wanawake walioshiriki uzinduzi huo wameiomba Serikali na IFC kuhakikisha programu hiyo inawanufaisha walengwa na kuwatoa hatua walizopo na kufikia malengo yao

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news