NA MWANDISHI WETU
SERIKALI itaendelea kuhakikisha watoto wote wanapata huduma za msingi kupitia vituo vya kulea watoto nchi nzima kwa kushirikiana na wadau wote.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akijadili jambo na Balozi wa China nchini Tanzania Mhe. Chen Mingjian kabla ya hafla maalum ya "Gusa moyo wa watoto" iliyofanyika katika kituo cha kulea watoto cha Ijango Zaidia Orphanage kilichopo Sinza Madukani, Wilaya ya Ubungo mkoa wa Dar es Salaam Mei 28, 2023.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameyasema hayo wakati wa hafla ya "Gusa Moyo wa Watoto" , iliyoandaliwa na Ubalozi wa Jamhuri ya watu wa China, katika kituo cha kulea watoto cha Ijango Zaidia Orphanage, Sinza Wilaya ya Ubungo mkoa wa Dar es Salaam Mei 28, 2023.
Waziri Dkt. Gwajima amesema amefarijika na mpango mzuri uliofanywa na mke wa Rais wa China kugusa mioyo ya watoto wa Kitanzania.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na watoto na wafanyakazi wa kituo cha kulea watoto cha Ijango Zaidia, mtaa wa Sinza, Wilaya ya Ubungo katika hafla maalum ya "Gusa Moyo wa watoto" watoto Mei 28, 2023.
"Kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan napenda kusema Wizara hii inaungana na maono haya ya wenza wanawake wa Marais na kuyashusha nchi nzima, tutaratibu mfumo mzima kwa kila anayeguswa kuwasaidia Yatima popote alipo kujua anapita njia gani kuwafikia watoto wote," amesema Waziri Dkt. Gwajima.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akipokea mahitaji mbalimbali kutoka kwa Balozi wa Chini nchini Tanzania Mhe. Chen Mingjian na kukabidhi kwa Mmiliki wa kituo cha kulea watoto cha Zaidia Orphanage Zaidia Hassan Mei 28, 2023, mahitaji hayo yametolewa na Mke wa Rais wa China Profesa Peng Liyuan kwa lengo la kusaidia watoto wa Tanzania katika hafla maalum ya "Gusa Moyo wa Watoto".
Akizungumza pia kwa niaba ya Mke wa Rais wa Zanzibar na mwanzilishi Taasisi ya Maisha Bora Zanzibar Mhe. Mama Mariam Mwinyi, Waziri Dkt. Gwajima ametoa rai kwa Wadau kuuenzi mpango huo ulioanzishwa na Mke wa Rais wa China Mhe. Profesa Peng Liyuan na kuufanya kuwa endelevu.
"Lengo la mpango huu ni kusaidia watoto waliokosa fursa barani Afrika kuwa na maisha bora ya baadaye," amesema Dkt. Gwajima.
Balozi wa China nchini Tanzania Mhe. Chen Mingjian akizungumza na watoto na wafanyakazi wa kituo cha watoto cha Ijango Zaidia kilichopo Sinza, wilaya ya Ubungo, mkoani Dar es Salaam wakati wa hafla maalum ya "Gusa Moyo wa Watoto", Mei 28, 2023.
Kwa upande wake Balozi wa China nchini Tanzania mhe. Chen Mingjian amesema katika kuadhimisha miaka 60 ya ushirikiano wa Madaktari wa China na Serikali ya Tanzania Jamhuri ya watu wa China imetoa mahitai mbalimbali ili kusaidia maisha bora kwa watoto wa Kitanzania.
Ameongeza kwamba kupitia ushirikiano huo, tayari wagonjwa 20 elfu wa Kitanzania wametibiwa kwa China kuongeza nguvu katika eneo la wataalamu na Hospitali.
Awali akizungumza katika tukio hilo, mmiliki wa kitio cha Zaidia Orphanage, Zaidia Hassan amebainisha kuwa kituo hicho kina watoto 52 hadi sasa ambapo kimeshafanikiwa kuwaunganisha watoto 80 na familia zao.
Mmiliki wa kituo cha kulea watoto cha Ijango Zaidia Orphanage Zaidia Hassan kilichopo Sinza Madukani, wilaya ya Ubungo Mkoani Dar es Salaam akieleza jambo katika hafla maalum ya kusaidia watoto iliyoandaliwa na Ubalozi wa China nchini Mei 28, 2023.(Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WMJJWM).
"Tunawaandaa watoto wetu kisaikolojia kuanzia miaka 14 kuwa wakishafikisha umri wa miaka 18 wanatakiwa kutoka kwenye kituo, baadhi yao wamesoma na wanajitgemea," amesema Zaidia.
Ameishukuru pia Serikali kwa ushirikiano katika vituo vya kulea watoto kupitia Maafisa Ustawi wa Jamii.
Katika tukio hilo, Waziri Gwajima amekabidhi mahitaji mbalimbali kwa ajili ya watoto ikiwemo vifaa vya masomo na vya michezo.