NA MWANDISHI WETU
SERIKALI imewaagiza wakandarasi wanaotekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, madaraja na viwanja vya ndege kuhakikisha wanaendelea na utekelezaji wa miradi hiyo ili ikamilike kwa viwango na kwa muda uliopangwa.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akifafanua jambo kwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Queen Sendinga, wakati wakikagua hatua za ujenzi wa barabara ya Ntendo-Kizungu (kilomita 25) kwa kiwango cha lami mkoani humo.
Agizo hilo limetolewa mkoani Rukwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof.Makame Mbarawa, wakati akikagua utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya Ntendo-Muze-Kilyamatundu yenye urefu wa kilomita 179 awamu ya kwanza inayoanzia Ntendo-Kizungu (kilomita 25) kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Waziri amesisitiza kuwa, kuhusu suala la malipo Serikali inatambua na itaendelea kuhakikisha inakamalisha taratibu za malipo mara tu baada ya wakandarasi kuwasilisha hati za madai.
Muonekano wa sehemu ya ujenzi wa barabara ya Ntendo-Kizungu (kilomita 25) kwa kiwango cha lami mkoani Rukwa. Ujenzi wa barabara hiyo unatekelezwa na Kampuni ya China Geo-Engineering Corporation kwa gharama ya shilingi bilioni 45.299 kwa muda wa miezi 18.
"Serikali inapokea madai ya wakandarasi na kuna taratibu za uhakiki ilizojiwekea ili kujiridhisha hivyo TANROADS endeleni kuwasimamia wakandarasi wote nchini tuikamilishe miradi,"amesisitiza Prof.Mbarawa.
Aidha, amesema hivi karibuni Serikali itaweka historia kwa kusaini mikataba ya EPC+F ya ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 2,000 kwa ajili ya kuunganisha mikoa yote kwa kiwango cha lami.
Awali akitoa taarifa ya mradi, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS),Mhandisi Rogatus Mativila, ameeleza mkataba wa ujenzi wa mradi huo umetolewa kwa Kampuni ya China Geo-Cooperation ya nchini China ambapo mkataba ulisainiwa Machi 29, 2022 na mradi ulianza Juni 6,2022 kwa muda wa miezi 18 pamoja na miezi 12 ya matazamio.
Kuhusu utekelezaji wa mradi huo, Meneja wa TANROADS,Mkoa wa Rukwa,Mhandisi Mgeni Mwanga, amesema mradi huo utajumuisha ujenzi wa makalvati makubwa 17 na makalvati madogo 43 ambapo hadi sasa makalvati makubwa 4 yamekamilika na 9 ujenzi unaendelea huku makalvati madogo 5 yamekamilika na yaliyobakia yanaendelea.
Kazi zikiendelea za ujenzi wa moja ya makalvati katika barabara ya Ntendo-Kizungu (kilomita 25) inayojengwa kwa kiwango cha lami mkoani Rukwa.
Ameongeza kuwa, kwa ujumla utekelezaji wa barabara hiyo umefikia asilimia 23 na mradi unatarajiwa kukamilika mwezi Disemba, 2023.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Queen Sendinga amesema kuwa, barabara hiyo ni muhimu sana kwani inapita kwenye maeneo yenye fursa mbalimbali za kiuchumi kama vile kilimo, ufugaji, uvuvi, uchimbaji wa madini (makaa ya mawe) na uchimbaji wa gesi.
"Hii barabara ikikamilika tutakuwa na usafiri wa uhakika wa bidhaa na mazao yetu tunayolima kutoka katika Bonde la Ziwa Rukwa hadi kufkia Sumbawanga mjini ambako ndiko soko la bidhaa zinazozalishwa linapatikana,"amefafanua Mkuu huyo wa mkoa.
Naye Mbunge wa Jimbo la Sumbawanga Mjini, Aeshi Hillary ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa kipaumbele miradi ya ujenzi inayoendelea katika jimbo lake na mkoa kwa ujumla.
Mbunge wa Jimbo la Sumbawanga Mjini, Mhe.Aeshi Hillary, akizungumza jambo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, wakati wakikagua hatua za ujenzi wa barabara ya Ntendo-Kizungu (kilomita 25) kwa kiwango cha lami mkoani Rukwa.(Picha na WUU).
Amesema, wasafiri wa mazao na bidhaa wamekuwa wakipata adha ya usafirishaji kwani barabara hiyo inapita kwenye miinuko na kona kali hali ambayo inasababisha magari makubwa kuzunguka kupitia miji ya Majimoto-Kibaoni-Katete-Kizi hadi Sumbawanga umbali wa takribani kilomita 230 ukilinganisha na kilomita 37 za kupitia hapa Ntendo-Muze kama hali ya barabara ikikamilika.
Barabara ya Ntendo-Muze-Kilyamatundu (kilomita 179) ni moja ya barabara muhimu inayounganisha mikoa ya Songwe, Rukwa, Katavi kupitia Bonde la Ziwa Rukwa.