NA MWANDISHI WETU
WAF Dodoma
WAZIRI wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu leo amekutana na Balozi wa Cuba nchini Tanzania Mhe. Yordenis Vera na kujadilia mambo mbalimbali yanayohusu Sekta ya Afya kati ya nchi hizo mbili, ikiwemo swala la upatikaji wa madaktari wa huduma za utengamao kwa watoto.

“Tumeshatoa Madaktari 30 hapa Tanzania na tupo tayari kuwaongeza kadiri ya uhitaji lakini pia kwa upande wa Dawa tunazozalisha nchini Cuba ni zile ambazo zitamsaidia mgonjwa wa Kisukari akizitumia vizuri basi inaokoa kukatwa kwa kiungo chochote cha mgonjwa,”amesema Mhe. Vera.
Waziri Ummy akimkaribisha Balozi wa Cuba nchini Tanzania ametoa shukrani kwa Balozi huyo kwa kuleta Madaktari 30 nchini lakini pia ameomba nafasi ya kuwapeleka Madaktari wa Tanzania nchini Cuba ili waweze kujifunza zaidi kwa vitendo.
Katika mazungumzo yao pia wamezungumzia juu ya kuendelea kuimarisha huduma za mama na mtoto, huduma kwa watoto wanaozaliwa na ulemavu, huduma za utengamao pamoja na kuendelea kutoa wataalamu nchini Cuba kuja Tanzania kwa lengo la kuendelea kushirikiana baina ya nchi hizo mbili.
Mwisho, Waziri Ummy ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano Kwa Balozi huyo Mhe. Yordenis Vera ili kuendeleza Ushirikiano baina ya Tanzania na Cuba kwa lengo la kuwasaidia Watanzania pamoja na Sekta ya afya kwa ujumla.