NA DIRAMAKINI
YANGA SC ya jijini Dar es Salaam imebisha hodi Fainali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini.
Ni kupitia mtanange wa nguvu wa kwanza wa Nusu Fainali uliopigwa Mei 10, 2023 katika Dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Kupitia mtaange huo ambao dakika 45 za kwanza zilionekana kuwa ngumu chini ya Kocha Nasredeen Nabi, Yanga SC walikitumia kipindi cha pili kuwapa maumivu Marumo Gallants.
Mburkinabe Stephane Aziz Ki alianza kuzichana nyavu dakika ya 64 na Mghana Bernard Morrison dakika ya 90 akaongeza kidonda juu ya wageni hao.
Aidha, kwa matokeo hayo Yanga SC wanatakiwa kwenda kuulinda ushindi huo kwenye mchezo ww marudiano Mei 17, 2023 utakaopigwa katika dimba la Royal Bafokeng, Phokeng, NW.
Yanga SC wakifanikiwa kuvuka hapo watakutana na mshindi wa jumla kati ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast na USM Alger ya Algeria katika fainali zitakazopigwa kati ya Mei 28 na Juni 3,2023.
Fedha za motisha
Wakati huo huo, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Balozi Dkt.Pindi Hadhara Chana alimkabidhi Nahodha wa Yanga, Bakari Nondo Mwamnyeto fedha taslimu shilingi milioni 20.
Fedha hizo ni sehemu ya zawadi ya motisha kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini ambapo kila bao lilinunuliwa ka shilingi milioni 10.
Rais apongeza
Katika hatua nyingine, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan amewapongeza klabu ya Yanga SC kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini katika mchezo wa kwanza wa Nusu Fainali dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
“Hongereni Yanga kwa ushindi katika mchezo wenu wa raundi ya kwanza ya Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho (CAF Confederation Cup)”.
“Nawatakia maandalizi mema kwa mchezo wenu wa raundi ya pili, muendelee kuiheshimisha nchi yetu. Hamasa yangu inaendelea,”amesema Mheshimiwa Rais Dkt.Samia.