YANGA YETU TANZANIA, KOFIA TWAWAVULIA

NA LWAGA MWAMBANDE

YOUNG Africans maarufu kama Yanga SC, n
i mara ya kwanza kufika fainali, lakini kwa Tanzania Simba ndiyo ilikuwa ya kwanza ilifika fainali mwaka 1993 ikashindwa na Stella Abidjan ya Ivory Coast. 

Simba ilifungwa nyumbani 2-0 na Stella Abidjan baada ya kutoka sare ugenini.

Aidha,Yanga imefikia hapa baada ya kuichapa Marumo Gallants F.C ya Afrika Kusini jumla ya mabao manne nyumbani na ugenini huku, Marumo wakipata moja la kufutia machozi.

Mei 17, 2023 wenyeji Marumo Gallants F.C ya Afrika Kusini iliwakaribisha Yanga SC katika mtanange ambao ulipigwa ndani ya Uwanja wa Royal Bafokeng nchini Afrika Kusini wakiwa na mtaji wa mabao mawili ambayo waliyapata nyumbani.

Mchezo wa kwanza uliochezwa katika Dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, Yanga SC iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 yaliyofungwa kipindi cha pili na Stephane Aziz Ki na Bernard Morison.

Kupitia mtanange huu wa marudiano, Yanga SC walianza kuandika bao la kwanza lililowekwa nyavuni na Fiston Kalala Mayele dakika ya 46 katika kipindi cha kwanza.

Ni bao la ushindi ambalo lilidumu kipindi chote cha pili ambapo kipindi cha pili,Kennedy Musonda ndani ya dakika ya 62 alivuruga kabisa mipango ya Marumo Gallants F.C baada ya kupachika bao safi huku bao la kufutia machozi la Marmo Gallants likifungwa dakika ya 91 ya mchezo huo na Ranga Chivaviro. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwmabande anasema, mafanikio haya ni makubwa na yafaa kuwatakia kila la heri Yanga SC. Endelea;


1.Yanga yetu Tanzania, kofia twawavulia,
Mlivyowafanyizia, Marumo huko walia,
Fainali kufikia, jambo la kufurahia,
Mliyoyafanya Yanga, ni sifa kwa Tanzania.

2.Nyumbani mlipania, wageni kujipigia,
Na kwao mmezidia, magoli kujifungia,
Fainali meingia, sote tunafurahia,
Mliyoyafanya Yanga, ni sifa kwa Tanzania.

3.Hayawi mmefikia, fainali kuingia,
Sote twawashangilia, wageni huko walia,
Kwenu ni historia, na shangwe kwa Tanzania,
Mliyoyafanya Yanga, ni sifa kwa Tanzania.

4.Mechi mbili zasalia, kombe kujichukulia,
Maarifa kitumia, malengo mtafikia,
Isikike Tanzania, kombe tumejitwalia,
Mliyoyafanya Yanga, ni sifa kwa Tanzania.

5.Mashabiki shangilia, pazuri mmefikia,
Wengine twaangalia, kwa mbali twatamania,
Vile ni Watanzania, mwishowe twafurahia,
Mliyoyafanya Yanga, ni sifa kwa Tanzania.

6.Imetajwa Tanzania, Yanga mlipofikia,
Kwa sisi Watanzania, kitu cha kujivunia,
Ushabiki wasalia, wa nyumbani kutania,
Mliyoyafanya Yanga, ni sifa kwa Tanzania.

7.Kiunzi kimesalia, kombe kujinyakulia,
Heri tunawatakia, kilele kukifikia,
Walakini angalia, punguza kutusagia,
Mliyoyafanya Yanga, ni sifa kwa Tanzania.

8.Mwaka huu nakwambia, kwa Yanga historia,
Makombe yanonukia, matatu mwajitwalia,
Mawili ya Tanzania, na moja linasalia,
Mliyoyafanya Yanga, ni sifa kwa Tanzania.

9.Ligi Kuu Tanzania, mmekwishajitwalia,
FA Tanzania, na hilo linanukia,
Hatrick nakwambia, matatu kijitwalia,
Mliyoyafanya Yanga, ni sifa kwa Tanzania.

10.Zile pesa za Samia, mnazidi jipatia,
Mechi mbili kumbatia, arobaini sikia,
Hongera twawapatia, zidini kufurahia,
Mliyoyafanya Yanga, ni sifa kwa Tanzania.

11.Sasa rudi Tanzania, muweze kujichimbia,
Maandalizi sawia, Alger kazi fungia,
Vizuri kitufanyia, tutazidi shangilia,
Mliyoyafanya Yanga, ni sifa kwa Tanzania.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602



Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news