Agizo la Waziri Mkuu lamleta mwanafunzi aliyepotea ndani ya saa 24

NA DIRAMAKINI

SIKU moja baada ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa kumuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera na Kamati ya Usalama ya Mkoa huo wafanye uchunguzi zaidi na kwa haraka kuhusiana na tukio la kupotea kwa binti Esther Noah Mwanyiru ambaye alikuwa akisoma shule ya Sekondari ya Panda Hill mkoani humo, RC Homera na timu yake wameanza kazi.

RC Homera amesema, kama kuna mtu yupo na mwanafunzi huyo wa kidato cha tano aliyepotea Mei 18, 2023 ni vizuri akamuachia au kama yupo sehemu yoyote ni vizuri wananchi wakitoa ushirikiano ili apatikane.

Ameyabainisha hayo leo Juni 23, 2023 wakati akizungumza kupitia Clouds360 ya Clouds TV huku akisema, kupotea kwa mtoto huyo ni maumivu makubwa kwa familia.

“Chukulia mtoto wako amepotea na hajulikani alipo utajisikiaje? Sisi ni viongozi, lakini ni wazazi pia tunajisikia maumivu sana na leo tutakuwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa ili kujua tumefika hatua gani.

“Pia tutawasilisha taarifa kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye alitoa maagizo kwamba huyu mwanafunzi atafutwe ili ajulikane alipo na alinipigia na kunitumia meseji kwamba baada ya taarifa kukamilika nimtumie taarifa ofisini kwake.

“Jitihada mbalimbali zilifanyika ikiwa na pamoja na kuwahoji walimu wa shule,wanafunzi,marafiki wa Ester na jumbe zote alizokuwa akiandika zilizoachwa na mwanafunzi huyo zimechukuliwa na kupelekwa kwenye maabara kwa ajili ya uchunguzi ili kubaini kama ni jumbe za mwanafunzi huyo aliandika mwenyewe au la!."

Hayo yanajiri ikiwa Alhamisi ya Juni 22, 2023 Waziri Mkuu alitoa agizo la uchunguzi huo baada ya kupokea clip yenye maelezo ya mzazi wa binti huyo ambaye alikuwa akisoma kidato cha tano, tahsusi ya PCB kwenye shule hiyo.

Katika clip hiyo, Mama yake Esther anadai kwamba yeye na mume wake waliitwa na uongozi wa shule hiyo na kujulishwa kwamba Esther hajaonekana tangu asubuhi ya Mei 18, 2023 na kwamba hadi sasa zimepita siku zaidi ya 20 wamekuwa wakimtafuta binti yao kila mahali lakini hakuna dalili za kumpata.

Mama Esther anadai kuwa, Esther aliacha ujumbe wa maandishi akiwaaga rafiki zake na kuomba Mwalimu Jimmy aache kuwafanyia wanafunzi wengine kitendo alichomfayia yeye kwani kimesababisha maisha yake kuwa magumu

“Naomba umfikishie salamu Mwalimu Jimmy, mwambie ameyafanya maisha yangu kuwa magumu sana hapa shuleni. Asiendelee kuwafanyia wanafunzi wengine kama alivyoyafanya maisha yangu mimi kuwa magumu,” alisema mama yake Esther akisoma sehemu ya ujumbe huo.
Amepatikana

Hata hivyo,taarifa za hivi punde ni kuwa Ester Noah Mwanyiru aliyepotea amepatikana katika maeneo ya Ifisi jijini Mbeya.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, muda huu kuna mahojiano yanakamilishwa Kituo cha Polisi ili akabidhiwe kwa wazazi. 
 
Taarifa mpya
 
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 23,2023 mkoani hapa, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema, chumba alichokutwa binti huyo huko maeneo ya Ifisi Mbalizi kinamilikiwa na Azurati Mohamed ambapo baada ya mahojiano alidai binti huyo alikabidhiwa na mmoja wa mteja wake.

“Amepatikana akiwa hai maeneo ya Ifisi mji mdogo wa Mbalizi akiwa katika chumba cha mwanamke mmoja ambaye ni muuza mkaa kwenye nyumba ya kupanga ya Azurati Mohamed, alikabidhiwa na mtu mmoja ambaye ni mteja wake wa mkaa,”amesema.

Amesema, mteja huyo anajulikana kwa jina la Baba Geofrey na kwamba baada ya makabidhiano hayo alisema amemwaribu mwanafunzi huyo, hivyo akae naye siku mbili akimtafutia sehemu ya kumpangia.

Jeshi la Polisi mkoani humo kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi lilipomuuliza binti huyo iwapo anahitaji kwenda shule, alidai yupo tayari isipokuwa apelekwe shule nyingine.

“Nikipelekwa shule nyingine nitakuwa tayari kuingia darasani kusoma ila siyo shule niliyokuwa nasoma na naomba walimu wabadilike,”amesema.

Hata hivyo mkuu wa mkoa huo ameahidi kumpeleka kwenye shule yeyote aendelee kusoma. RC Homela ameeleza kuwa, katika vipimo vya awali walivyofanya havijaonesha kama anaujauzito, na wanatarajia kufanya vipimo vingine.

“Ikibainika kwamba anaujauzito itatakiwa abaki nyumbani hadi ajifungue kisha arudi shuleni kuendelea na masomo,”amesema. RC Homela amesema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ikiwamo kumtafuta Baba Geofrey.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news