ALIVYOTUHESHIMISHA, BORA KUMWIMBA SHIRIMA

NA LWAGA MWAMBANDE

HIVI karibuni Mbunge wa Rombo mkoani Kilimanjaro,Mheshimiwa Profesa Adolf Mkenda ametoa taarifa fupi yenye fundisho kubwa kuhusu namna ambavyo mtu ambaye anapambania ndoto yake anavyoweza kuyaendea malengo yake kwa haraka.

Ni wakati akizungumzia maisha ya Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Shirika la Ndege la Precision Air,Michael Ngaleku Shirima ambaye amesema ameacha historia nzuri kwa Taifa kwa kuwa alikuwa mtu asiyekata tamaa,mwenye bidii na mpambanaji licha ya changamoto mbalimbali alizopitia wakati wa kuyatafuta maisha.

Mzee Shirima ambaye alikuwa na umri wa miaka 80 mzaliwa wa Rombo mkoani Kilimanjaro alifariki dunia Juni 9,2023 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam alikokuwa amelazwa tangu Juni 8, mwaka huu.

Profesa Mkenda ambaye pia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, alisema kitabu alichoandika Mzee Shirima na kukizindua mwaka 2022 alichokipa jina la On My Father's Wings (An Entrepreneurial Journey of Finding Humility, Resiliency, and a Lasting Legacy) kinaelezea historia ya maisha yake na uamuzi mgumu aliochukua wa kujiuzulu Shirika la Ndege la Tanzania (Air Tanzania) mwaka 1979.

"Niliwahi kumuuliza ni kwa nini aliacha kazi Air Tanzania, aliniletea barua zake kwa nini alitaka kujiuzulu na mpaka leo nina nakala yake, alivyoona shirika linayumba na kuwatahadharisha kwamba litakufa wakiendelea vivyo hivyo, hawakumsikiliza, hivyo akaamua kujiuzulu.

"Alipofika nyumbani mke wake alishtuka sana, lakini wakati huo walikuwa wanakaa nyumba ya Serikali, alikuwa hana kazi, ikabidi aondoke akatafute mahali pa kujishikiza yeye na familia yake, baadaye alianza kufanya biashara ya kuuza nyama choma kidogo kidogo.

“Alitafuta mkopo akaanza kununua mafuta ya pamba na alipata lori akaanza kuchukua mafuta kutoka Mwanza kuja kuuza Moshi. Wakati anafanya biashara hiyo akagundua Mwanza kuna ujenzi mwingi, lakini mbao zipo upande wa Moshi, akawa anachukua mbao Moshi na kupeleka Mwanza na kurudi na mafuta, alifanya kazi ngumu,"alibainisha Prof.Mkenda kama alivyokaririwa na Mwananchi.

Mheshimiwa Profesa Mkenda aliendelea kufafanua kuwa, Shirima wakati wa uhai wake kipindi hicho kwa kushirikiana na mtu mwingine aliyemtaja kwa jina la Kisinani walianza biashara ya kupeleka kahawa nje ya nchi na siku moja rafiki yake huyo alimwambia kuna mtu anahitaji ndege ndogo kwa ajili ya kufanya kazi shambani.

"Hivyo akaanza na ndege ndogo ya kukodi, baadaye akanunua nyingine, ndivyo alivyoendelea mpaka alipofikia leo," alisema Profesa Mkenda.

Alisema atamkumbuka Shirima kwa namna alivyokuwa mtu wa dini na hata alipofikwa na changamoto za biashara alikuwa akifunga siku tisa akiomba.

Pia, Prof. Mkenda anasema mzee Shirima ni mfano wa kuigwa ndani ya Tanzania na Afrika nzima, kutokana na tabia yake ya upole na uungwana.

Amesema, maisha yake ni mfano mzuri wa kuigwa kwani alikuwa ni mtu wa kujitolea katika jamii na kwamba katika Wilaya ya Rombo ambako ndiko alipozaliwa amefanya mambo makubwa ikiwemo kuanzisha kituo cha watoto yatima na hivi karibu alikuwa anajenga zahanati kwa ajili ya watoto yatima. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, Mzee Shirima amewaheshimisha Watanzania. Endelea;


1.Ameondoka Shirima, vema kumwimba Shirima,
Kazi yake yasimama, inayotupa heshima,
Yake yote tukipima, kweli aliishi vyema,
Alivyotuheshimisha, na ajengewe mnara.

2.Precision ndege yetu, kwa kweli yafanya vyema,
Miaka lukuki petu, shirika lilivyovuma,
Mahitaji yale yetu, kujibu ilisimama,
Alivyotuheshimisha, na ajengewe mnara.

3.Kuna muda hapa kwetu, tupokuwa lelemama,
Precision ndege zetu, kazi hazikutuama,
Kwa zile safari zetu, walai hatukukwama,
Alivyotuheshimisha, na ajengewe mnara.

4.Kuna muda Tanzania, safari likuwa homa,
Angani kuangalia, likuwa kukwamakwama,
Precision kuingia, mambo yakawa ni mema,
Alivyotuheshima, na ajengewe mnara.

5.Mepita mingi miaka, Precision yasimama,
Wengine shaenda chaka, shirika lafanya vyema,
Shirima anahusika, utendaji wake mwema,
Alivyotuheshimisha, na ajengewe mnara.

6.Tunao Watanzania, ambao wafanya vyema,
Yao tunajivunia, yanatufanya kuvuma,
Shirima nakutajia, ni kinara asimama,
Alivyotuheshimisha, na ajengewe mnara.

7.Kwa uchumi Tanzania, Precision ni njema,
Watalii waingia, pesa za kigeni njema,
Kote wanakufikia, hata kupata mlima,
Alivyotuheshimisha, na ajengewe mnara.

8.Toka zamani za kule, hata sasa iko vyema,
Yapaa huku na kule, kote twafika salama,
Zaidi ajali ile, vinginevyo kote kwema,
Alivyotuheshimisha, na ajengewe mnara.

9.Atatajwatajwa wapi, mzalendo huyu mwema,
Ataeleweka vipi, bila kumsemasema?
Watu wajifunze wapi, wasimjue Shirima?
Alivyotuheshimisha, na ajengewe mnara.

10.Pole tunawapatia, kwa msiba wa Shirima,
Huyu ni Mtanzania, alotutendea mema,
Yuko kwa historia, jina litazidi vuma,
Alivyotuheshimisha, na ajengewe mnara.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news