NA GODFREY NNKO
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imebaini kuwa kuna baadhi ya taasisi, kampuni na watu binafsi wanaojihusisha na biashara ya kutoa mikopo bila ya kuwa na leseni, jambo ambalo ni kinyume na Kifungu cha 16(1) cha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa leo Juni 21,2023 na Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba.
"Aidha, taasisi, kampunina mtu binafsi wasio na leseni hawaruhusiwi kufanya biashara ya kukopesha.
"Kufuatia kifungu cha 16(2)(a) cha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018, hatua zitakazochukuliwa kwa ukiukaji wa Sheria hiyo ni pamoja na faini isiyopungua Shilingi Milioni 20 au kifungo kisichopungua miaka miwili,"imefafanua sehemu ya taarifa hiyo ya Gavana wa BoT.
Pia,Benki Kuu ya Tanzania imewakumbusha watoa huduma ndogo za fedha waliokwisha kupata leseni kufuata sheria, kanuni na miongozo inayotolewa na Benki Kuu ya Tanzania ikiwemo kuwapa wakopaji mikataba, kuonesha riba ya mkopo kama ilivyopitishwa kwenye sera ya mkopo, gharama nyingine zote wanazotoza, na riba kukokotolewa kwa mwezi na sio kwa siku.
"Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuwaasa wananchi kuepuka kukopa au kufanya biashara na taasisi, kampuni au mtu binafsi ambao hawana leseni.
"Aidha, orodha ya taasisi, kampuni na watu binafsi wenye leseni za biashara ya kukopesha zilizotolewa na Benki Kuu ya Tanzania inapatikana kwenye tovuti ya Benki Kuu ambayo ni www.bot.go.tz na kwenye matawi yake yote.
"Kwa taarifa zaidi tafadhali wasiliana na: Kurugenzi ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha Idara ya Usimamizi wa Taasisi za Huduma Ndogo za Fedha Benki Kuu ya Tanzania,2 Mtaa wa Mirambo, S.L.P 2939 Dar es Salaam Simu Na. +255-22-223-5585; Barua Pepe: info@bot.go.tz or botcommunications@bot.go.tz," imeongeza taarifa hiyo ya Gavana wa BoT.