NA GODFREY NNKO
WAHARIRI wa vyombo vya habari wameombwa kutumia kalamu na vyombo vyao vya habari kuwakumbusha wakurugenzi na wamiliki wa makampuni nchini kuendelea kuwasilisha taarifa za Wamiliki Manufaa kwa wakati ili kuwa na uwazi na uwajibikaji katika kampuni husika.
Hayo yamebainishwa Juni 8, 2023 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam kupitia kikao kazi kati ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na wahariri mbalimbali wa vyombo vya habari nchini.
Mgeni rasmi katika kikao kazi hicho ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatius Balile amefafanua kuwa,vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuweza kulisukuma jambo hilo ili walengwa waweze kutimiza wajibu wao ikiwa ni takwa la kisheria.
"BRELA imezingatia umuhimu wetu kama wadau muhimu na kuamua kutuandalia warsha hii. Na baada ya kutoka hapa tutakuwa tumepata uelewa mpana zaidi kuhusiana na dhana ya umiliki manufaa.
"BRELA imekuwa ikishirikiana na wahariri hususani kwenye shughuli zake zinazohusu utendaji kazi wake wa kila siku na pale tunapokuwa na jambo jipya la kimkakati tumekuwa tukiwashirikisha wahariri.
"Hii ni pamoja na kupeana taarifa na kupokea marekebisho au maboresho mbalimbali yanayoendelea ya kisheria na kimfumo ili kuhakikisha tunakuwa na uelewa wa kutosha kwenye habari tunazozipeleka kwa wananchi ili kuboresha mazingira ya biashara hapa nchini,"amefafanua Balile.
Ameendelea kufafanua kuwa, "Leo tumefika tena mbele yenu kutoa mafunzo na ufafanuzi zaidi ya maboresho yanayoendelea kwenye sheria, kanuni na miongozo mbalimbali ya miongozo hii ya huduma za usajili wa kampuni hususani mabadiliko ya mwaka 2022 na kanuni zake.
"Niwakumbushe tu kwamba, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha marekebisho ya sheria na kanuni sura namba 212 kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wa taarifa za umiliki manufaa katika kampuni zote ambazo zimeshasajiliwa na zinazoendelea kusajiliwa ili kuboresha mazingira ya uwekezaji, kuzuia ukwepaji kodi, pamoja na utakatishaji wa fedha haramu na kufadhili vitendo vya kigaidi."
Balile amefafanua kuwa,pia mwaka 2022 kanuni ya umiliki manufaa katika kampuni zilipitishwa na kuanza kutumika rasmi mwaka huo huo.
"Na leo imeonekana ni vyema BRELA tukae nanyi sio kwa lengo la kuwafundisha, bali kuelekezana maendelezo hayo kusudi muwe mabalozi wazuri kwa wananchi ambao wanategemea kupata taarifa sahihi kupitia vyombo vya habari.
"BRELA imeshaanza utekelezaji wa ukusanyaji na utunzaji wa taarifa za umilki manufaa mwaka huu. Takwimu zinaonesha kwamba kampuni nyingi bado hazijawasilisha taarifa za umiliki manufaa bado uelewa ni mdogo.
"Kwa hiyo kwa kuzingatia umuhimu wenu kama njia ya kuwafikishia wananchi taarifa sahihi tumeandaa warsha hii mahususi kwa ajili ya kupeana uzoefu na uelewa pamoja na kuifikishia taarifa jamii.
"Tunategemea baada ya hii ninyi wadau wetu muhimu kupata elimu ya kutosha mtasaidia Watanzania kuwakumbusha juu ya muda, taratibu na umuhimu wa uwasilishaji wa taarifa za umiliki manufaa katika kampuni kwa mujibu wa sheria."
Kupitia kikao kazi hicho, washiriki walipata nafasi ya kuwa na mjadala mpana na kuwasilisha mawasilisho mbalimbali, kupokea maoni, maswali na kuyatolea majibu kwa lengo la kuelewa kwa undani dhana hiyo katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara hapa nchini.
"Aidha, kama ilivyo mara zote mmekuwa mkishirikiana na BRELA na taasisi zingine za Serikali zinazosimamia urasimishaji wa biashara ni mategemeo yangu pia warsha hii itaibua michango mizuri na uelewa wa pamoja ambao utasaidia kufanikisha zoezi hili kwa manufaa ya biashara,uwekezaji na sisi wananchi wote kwa ujumla,"amefafanua Balile.
BRELA
Naye Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Andrew Mkapa amesema, wahariri wa vyombo vya habari na vyombo vya habari vyenyewe kwa ujumla ni wadau wao muhimu, kwani ndio nyenzo kubwa inayotegemewa katika kufikisha taarifa mbalimbali kwa jamii.
"Kutokana na hali hiyo, BRELA inatambua nafasi ya vyombo vya habari ni kiungo muhimu na chachu katika eneo la uhamasishaji na urasimishaji wa biashara nchini."
Amesema, BRELA mara kwa mara imekuwa ikiwashirikisha wanahabari hususani wahariri kwenye shughuli zake mbalimbali zinazohusu utendaji kazi wa kila siku ikiwemo marekebisho na maboresho mbalimbali yanayoendelea ya kisheria.
"Lakini vile vile ya kimifumo na hii yote ni katika harakati za kuhakikisha kuwa wananchi wanapata taarifa sahihi na kwa wakati.
"Taarifa ambazo zinahusu mabadiliko hayo yakiwa na lengo la kuboresha huduma zinazotolewa na BRELA ili hatimaye wapate unafuu na urahisi wa kuzitumia huduma hizo katika kufanya biashara hapa nchini."
Katika kikao kazi hicho baina ya BRELA na wahariri, watumishi wa wakala huo wamewaongoza na kuwapitisha katika mada walizoziandaa kuhusiana na dhana ya umiliki manufaa ambayo ni mpya na imeibuka katika masuala ya makampuni na sheria za fedha.
"Tutawasikia wataalamu watupe elimu hiyo na sisi tunapoelimisha umma kwa kuwa ni zana mpya waweze kuwa na ufahamu kwa kina kuhusu hili suala.
"BRELA imeona kuna umuhimu mkubwa wa kutoa elimu hii kwa kuwashirikisha wadau kutoka kwenye sekta ya habari kwa mfano baada ya marekebisho ya sheria ya makampuni yaliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na baada ya kupitishwa kuna kanuni za hilo suala la umiliki manufaa, hivyo imeonekana ni muhimu sana kuwafikishia wananchi na hasa wale wanaomiliki makampuni au wanaokusudia kuanzisha makampuni kuwafikishia taarifa hizi.
"Hivyo lengo la warsha hili kwa wahariri ni kuwaelezea juu ya mabadiliko hayo na marekebisho hayo ya sheria ambazo tunazungumza ili kuwa na uelewa wa pamoja utakaowezesha umma wote kushiriki kikamilifu na kwa ufasaha na kuelimisha wengine au umma juu ya dhana nzima ya suala hili la umilki manufaa,"amefafanua Kaimu Mkurugenzi Mtendaji huyo.
Kuhusu wao
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ilianzishwa chini ya Sheria ya Wakala za Serikali Na. 30 ya Mwaka 1997 na kuzinduliwa rasmi Desemba 3, 1999 chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara (kwa sasa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara).
Majukumu ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ni kama yalivyoainishwa kwenye Waraka wa Uanzishwaji (establishment order) Na. 38 ya Tangazo la Serikali na. 294 la tarehe 08/10/1999.
Majukumu ya Msingi ya BRELA ni kusajili kampuni (The Companies Act, Cap. 212), kusajili Majina ya Biashara (The Business Names (Registration) Act, Cap. 213 R.E. 2002),kusajili Alama za Biashara na Huduma (The Trade and Service Marks Act, Cap. 326 R.E. 2002).
Aidha, majukumu mengine ni kutoa Hataza (The Patents (Registration) Act, Cap. 217 R.E. 2002),kutoa Leseni za Viwanda (The National Industries (Licensing and Registration) Act, Cap 46 R.E. 2002) na kutoa Leseni za Biashara Kundi "A" (The Business Licensing Act Cap. 208 R.E. 2002)
Isdor Mkindi kutoka Idara ya Usajili amefafanua kuwa, wahariri na vyombo vya habari vina mchango mkubwa kwani kupitia taarifa zao zitawawezesha wananchi kuhuisha taarifa za makampuni na kuendelea kurasimisha biashara zao kote nchini.
"Kuijua BRELA ni muhimu sana, kwanza sisi ni wakala wa Serikali, tunafanya kazi kwa niaba ya Serikali, tuna mamlaka si kamili kabisa, ukichukua BRELA na TANESCO, tofauti yetu ni kwamba sisi tuna mamlaka, karibia yote lakini siyo yote, mengine amebakia nayo wizara na Serikali. Tupo chini ya Wizara ya Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara.".
"Sasa, kwa nini ninyi,mna umuhimu mkubwa sana angalau tunaweza kuwaeleza kwa maneno manne, wanahabari ni watu muhimu sana kwetu kwa sababu mtakumbuka kwamba sasa hivi sisi, hatupokei karatasi wala hatupokei hela, tupo kidigitali toka 2018.
"Huduma zetu zote zipo mtandaoni,sasa wafanyabiashara si wale tu ambao walikwisha sajili biashara zao,ni hata wale ambao hawajasajili na ambao hata hawana mpango wa kusajili biashara zao, lakini tunapaswa kuwafikia ili waweze kusajili. Nani afanye kazi hiyo, hatutaweza ndiyo maana wanahabari wanakuja, wanakuwa ni watu muhimu katika wakati wowote.
"Ninyi ni watu muhimu lazima tuhabarishwe, tuelimishwe ili tufahamu Dunia inataka nini, sasa media, ni mwalimu wetu mkuu, hilo hatuna ubishi nalo ndiyo maana mko hapa, tunatarajia wale wateja wetu au wale wateja watarajiwa wapate taarifa sahihi ili waweze kufanya uamuzi sahihi, sasa ninyi mnatakiwa mfanye kazi ya kuharakisha, tunachokizaa kiweze kuwafikia wananchi wetu.
"Wananchi wote, wana imani kubwa sana na vyombo vya habari,hivyo mna umuhimu mkubwa sana kwetu,"amefafanua Mkindi.
Aidha, Mkindi amebainisha kuwa, BRELA wanaamini kazi wahariri wanazofanya na wao wanafanya na Serikali, hivyo wazifanye kwa uadilifu mkubwa, na kutumia rasilimali zao zote ili kuhakikisha yanapatikana matokeo bora kwa ustawi wa Taifa.
Rweyemamu
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Makampuni na Majina ya Biashara kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Meinrad Rweyemamu amesema kuwa, vyombo vya habari ni muhimu katika kuelimisha umma ikiwemo wadau pamoja na huduma zinazotolewa na BRELA.
“Kila kampuni inapaswa kuwasilisha majina ya wanufaika wake baada ya siku 30 kusajiliwa, nchi nyingine wanafanya siku hiyo hiyo ya usajili lakini sisi walau tumeweka siku 30 baada ya kusajiliwa.
“Kutofanya hivyo utalazimika kulipa faini. Sheria hii imeanza kutumika baada ya marekebisho ya sheria ya Kampuni Sura 212, mwaka 2022 na ndipo ilipotambulisha dhana ya Mmiliki Manufaa,” amesema.
Sheria ya Kampuni Sura 212 ilifanyiwa marekebisho kupitia Sheria ya Fedha, 2020 kwa kuleta dhana ya Umiliki Manufaa wa Kampuni.
Marekebisho hayo yalienda sambamba na utungwaji wa Kanuni za Wamiliki Manufaa za mwaka 2021 ambazo zinatumika katika kusimamia zoezi la ukusanyaji, uwasilishaji na utoaji wa taarifa za wamiliki manufaa wa kampuni nchini.
Rweyemamu amesema kuwa, kampuni zina umuhimu mkubwa katika kuchangia uchumi wa nchi, ingawa uzoefu umeonesha kwamba kampuni nyingine zinatumika vibaya katika kufanya vitendo vya uhalifu ikiwa ni pamoja na utakatishaji wa fedha haramu, ukwepaji wa kodi, kufadhili vitendo vya ugaidi na vitendo vya rushwa.
Pia amesema, kutokana na hali hiyo amesema, Benki ya Dunia na taasisi nyingine za Kimataifa zinazojihusisha na masuala ya kusaidia biashara zimejitolea kwa njia moja au nyingine kuleta mabadiliko kwa kuanzisha dhana hiyo ya wamiliki manufaa.
Kaimu Mkurugenzi huyo amefafanua kuwa, Tanzania ni moja ya nchi ambazo zipo chini ya Eastern and Southern Anti-Money Laundering Group ( ESAMLAG) ambapo lengo kuu la ESAMLAG ni kuhakikisha kuwa mapendekezo 40 ya Financial Action Task Force yanafanyiwa kazi.
Amesema,moja kati ya mapendekezo hayo ni kuhakikisha nchi inaanzisha daftari la Wamiliki Manufaa wa kampuni na kuhakikisha vyombo vya uchunguzi vinapata taarifa za wamiliki manufaa kwa wakati. Amesema, kwa sasa Tanzania imewekwa katika orodha ya kijivu.
FATF ni nini?
Kikosi Kazi cha Kifedha (FATF) ni shirika la kiserikali linalofuatilia utoroshaji wa fedha duniani na mwelekeo wa ufadhili wa kigaidi.
FATF hushirikiana na nchi wanachama na mashirika ya kikanda ili kuunda mfumo wa kisheria, udhibiti na uendeshaji wa kupambana na vitisho hivyo.
Kama sehemu ya juhudi zake, FATF hudumisha Orodha Nyeusi (Black List), inayojulikana rasmi kama Mamlaka ya Hatari Kuu chini ya Wito wa Hatua, na Orodha ya Kijivu (Grey List).
Orodha ya kijivu inajumuisha nchi ambazo zimejitolea kushughulikia mapungufu ya kimkakati katika mifumo yao ya Kupambana na Utakatishaji Fedha/Kukabiliana na Ufadhili wa Ugaidi (AML/CTF).
Kwa kuzingatia hatari inayowezekana ya udhibiti inayohusishwa na nchi ambazo haziudumii viwango vya utiifu vya kimataifa, taasisi za fedha zinapaswa kufahamu kuhusu orodha nyeusi ya FATF na nchi zilizo na orodha ya kijivu na kile ambacho jina hilo linahusisha.
Orodha Nyeusi ya FATF ni nini?
Orodha nyeusi ya FATF (wakati mwingine hujulikana kama orodha nyeusi ya OECD), hii ni orodha ya nchi ambazo shirika linazingatia,serikali husika haina ushirika katika juhudi za kimataifa za kupambana na utakatishai fedha na ufadhili wa ugaidi.
Kwa kutoa orodha hiyo, FATF huwa inatarajia kuhimiza nchi kuboresha kanuni zao za udhibiti na kuanzisha seti ya kimataifa ya viwango na kanuni za AML/CTF na kanuni ambazo nchi zilizoorodheshwa nyeusi zinaweza kukabiliwa na vikwazo vya kiuchumi na hatua zingine za kukataza kutoka nchi wanachama wa FATF na mashirika ya kimataifa.
Orodha nyeusi ni hati hai iliyotolewa na kusahihishwa mara kwa mara katika ripoti rasmi za FATF. Nchi huongezwa na kuondolewa kwenye orodha nyeusi huku kanuni zao za udhibiti za AML na CFT zikirekebishwa ili kufikia viwango vinavyohusika vya FATF.
Aidha, orodha nyeusi ya kwanza ya FATF ilitolewa mwaka 2000 ikihusisha nchi 15. Tangu wakati huo, orodha zimechapishwa kama sehemu ya taarifa na ripoti rasmi za FATF kila mwaka na wakati mwingine mara mbili kwa mwaka.
Kufikia Februari 2023, Korea Kaskazini, Jamhuri ya Kiislam Iran na Myanmar zilijumuishwa kwenye orodha nyeusi ya FATF.
FATF inataja mapungufu makubwa katika tawala za AML/CTF za nchi zilizoorodheshwa nyeusi na kupendekeza nchi zingine zichukue tahadhari kali zinapofanya biashara na makampuni yaliyo katika maeneo hayo ya kisheria.
Ingawa FATF imetoa wito kwa nchi wanachama wake kutumia hatua madhubuti za kukabiliana katika shughuli zozote za kibiashara na Korea Kaskazini, Iran, na Myanmar, imebainisha dhamira ya awali ya Iran katika kuboresha udhibiti wake wa AML/CTF.
Pia, FATF imeweka hatua za kuondolewa kwa Iran kwenye orodha, ikijumuisha hitaji la kuidhinisha Mikataba ya Palermo and Terrorist Financing Conventions.
Ingawa haina mamlaka ya uchunguzi wa moja kwa moja, FATF hufuatilia mifumo ya kimataifa ya AML/CFT kwa karibu ili kufahamisha maudhui ya orodha zake nyeusi.
Baadhi ya waangalizi wamekosoa neno "zisizo za ushirika" kuhusu nchi zilizo kwenye orodha nyeusi, wakisema kwamba baadhi ya nchi zilizoorodheshwa nyeusi zinaweza, badala ya kutenda kinyume na mazoea bora ya kimataifa, zisiwe na miundombinu ya udhibiti au rasilimali za kutunga Sheria ya AML ya FATF.
Je! Orodha ya Kijivu ya FATF ni nini?
Orodha ya kijivu ya FATF, inayojulikana rasmi kama Mamlaka Chini ya Kuongezeka kwa Ufuatiliaji, inajumuisha nchi zilizo na mapungufu katika mifumo yao ya AML/CTF.
Kama orodha nyeusi, orodha ya kijivu iliundwa mwaka 2000 na inasahihishwa mara kwa mara. Nchi zilizowekwa kwenye orodha ya kijivu zinakabiliwa na kuongezeka kwa ufuatiliaji na lazima zifanye kazi na FATF ili kuboresha taratibu zao.
Ili kufanya hivyo, FATF inazitathmini moja kwa moja au kutumia mashirika ya kieneo ya mtindo wa FATF (FSRBs) kuripoti maendeleo yao kuelekea malengo yao ya AML/CTF.
Ingawa uainishaji wa orodha ya kijivu sio wa kuadhibu kama orodha nyeusi, nchi zilizo kwenye orodha bado zinaweza kukabiliwa na vikwazo vya kiuchumi kutoka kwa taasisi kama Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia na kupata athari mbaya kwenye biashara.
Orodha ya kijivu inasahihisishwa mara kwa mara nchi mpya zinapoongezwa au nchi zinazokamilisha mipango yao ya utekelezaji zinavyoondolewa.
Aidha, kufikia Februari 2023, orodha ya kijivu ya FATF ilijumuisha nchi za;
Albania,
Barbados
Burkina Faso
Cayman Islands
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Haiti
Jamaica
Jordan
Mali
Malta
Mozambique
Nigeria
Panama
Philippines
Senegal
South Africa
South Sudan
Syria
Tanzania
Turkey
Uganda
United Arab Emirates
Yemen
Nyongeza za karibuni
FATF huendelea kukagua utendaji wa AML/CTF wa nchi wanachama wake ili kupima upatanishi wao na mwongozo wake wa udhibiti. FATF hivi karibuni imeongeza nchi zifuatazo kwenye orodha ya kijivu ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
FATF iliongeza Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwenye orodha ya kijivu mnamo Oktoba 2022. Uamuzi huo ulifanywa kwa sababu ya kutokuwepo kwa maendeleo ya kutosha ya nchi kuhusu mapendekezo yaliyowekwa katika ripoti ya ya hivi karibuni ya DRC ya Tathmini ya Pamoja (MER).
Aidha,FATF imesema DRC lazima ishughulikie kikamilifu mapungufu ya kimkakati yaliyotambuliwa kwa kutekeleza mpango kazi uliopendekezwa kufikia 2025.
Taifa lingine ni Jordan ambapo kufuatia MER mnamo 2019, Jordan ilijitolea kushughulikia mapungufu katika sheria zake za utakatishaji wa pesa za ndani na ufadhili wa ugaidi.
Mnamo Oktoba 2021, FATF iliamua kuwa Jordan haikufanya maendeleo ya kutosha kuelekea malengo hayo, na iliongezwa kwenye orodha ya kijivu.
FATF iliongeza Mali kwenye orodha ya kijivu mnamo Oktoba 2021. Kama vile Jordan, nyongeza ya Mali kwenye orodha ya kijivu ilichochewa na ukosefu wa maendeleo ya kufikia malengo katika MER yake ya 2019. FATF ililenga hasa hatari katika nchi zinazohusiana na ufadhili wa ugaidi.
Kufuatia MER ya mwaka 2021, Msumbiji iliweka dhamira ya hali ya juu ya kisiasa kushughulikia mapungufu katika kanuni zake za utakatishaji fedha za ndani na ufadhili wa ugaidi.
Wakati FATF ilibainisha kuwa nchi ilikuwa imepiga hatua katika baadhi ya hatua zilizopendekezwa na MER, maendeleo ya kutosha hayakuwa yamepatikana, na kusababisha Msumbiji kuongezwa kwenye orodha ya kijivu mnamo Oktoba 2022.
Mnamo Februari 2020, Myanmar ilijitolea kushughulikia mapungufu ya kimkakati yaliyoangaziwa katika MER ya 2018 ya nchi hiyo. Hata hivyo, mpango wa utekelezaji wa Myanmar uliisha muda wake Septemba 2021, na hakuna maendeleo makubwa yaliyofanywa.
Pia, mnamo Juni 2022, FATF iliitaka sana Myanmar kukamilisha mpango wake wa utekelezaji ifikapo Oktoba 2022. Kwa sababu ya kuendelea kukosekana kwa maendeleo na mambo mengi ya nchi bado hayajashughulikiwa zaidi ya tarehe ya mwisho ya mpango wa utekelezaji, FATF iliongeza Myanmar kwenye orodha nyeusi mnamo Oktoba 2022.
Hapo awali Nigeria iliongezwa kwenye orodha ya kijivu mwaka wa 2007 kutokana na mianya mbalimbali katika mfumo wake wa sheria na udhibiti.
Hata hivyo, iliondolewa kwenye orodha iliyoongezeka ya ufuatiliaji mnamo Oktoba 2013 kufuatia nchi kutekeleza kikamilifu mpango wake wa utekelezaji uliokubaliwa na pande zote mbili.
Mnamo Februari 2023, Nigeria iliongezwa tena kwenye orodha ya kijivu kufuatia mapungufu ya kimkakati ya AML/CTF yaliyotambuliwa na FATF.
Wakati huo huo, FATF iliongeza Afrika Kusini kwenye orodha ya kijivu mnamo Februari 2023 kufuatia MER ya 2021 ya nchi hiyo ambayo ilielezea ukosefu wa uangalifu unaostahili, kushindwa kwa mara kwa mara kutekeleza hatua za utambuzi wa AML/CFT, na ukosefu wa mafunzo na wafanyakazi katika sekta muhimu, ikiwa ni pamoja na sheria. utekelezaji.
Aidha, kufuatia MER yake mwaka 2021, FATF inabainisha kuwa Tanzania imepiga hatua katika baadhi ya hatua zilizopendekezwa za MER kuboresha mfumo wake wa AML/CTF.
Ingawa kutokana na sababu za hatua kadhaa ambazo hazijakamilika, FATF iliiweka Tanzania kwenye orodha ya kijivu mnamo Oktoba 2022.
FATF iliongeza Uturuki kwenye orodha ya kijivu mnamo Oktoba 2021 baada ya kuamua kuwa haijafanya maendeleo ya kutosha kushughulikia masuala yaliyowekwa katika MER yake ya 2019.
FATF ilitaja wasiwasi maalum kuhusu vitisho vya ufadhili wa ugaidi kutoka kwa majirani wa Uturuki, Syria, Lebanon, Iraq, na Iran.
Pia,FATF iliongeza Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kwenye orodha ya kijivu mnamo Machi 2022 kufuatia Mkutano wa Jumla na wa Kikundi Kazi mnamo Februari 2022.
FATF iliamua kwamba ingawa UAE ilikuwa imepata maendeleo makubwa tangu tathmini yake ya 2020 kuhusu masuala yanayohusiana na utakatishaji fedha, ufadhili wa ugaidi, kutaifisha mapato ya jinai, na ushirikiano wa kimataifa, maendeleo zaidi yanahitajika ili kuhakikisha kuwa uchunguzi na mashtaka ya kesi za utakatishaji fedha ni kulingana na wasifu wa hatari wa UAE.
Uondoaji
Kama vile nchi zinaongezwa mara kwa mara kwenye orodha nyeusi na orodha ya kijivu, nchi zinazoendelea katika kushughulikia mapungufu yao ya AML/CTF huondolewa kwenye orodha. Kwa kuzingatia hilo, FATF hivi karibuni iliondoa nchi zifuatazo kutoka kwenye orodha ya kijivu.
Mnamo 2020, FATF iliongeza Mauritius kwenye orodha ya kijivu, ikitaja mapungufu katika udhibiti wake wa manufaa wa umiliki na taratibu za kutaifisha mapato ya uhalifu.
Baada ya kufuata mpango wa utekelezaji wa FATF wa kushughulikia kasoro hizo, ikijumuisha kuandaa mipango mipya ya usimamizi inayozingatia hatari na mipango ya mafunzo ya utekelezaji wa sheria, Mauritius iliondolewa kwenye orodha ya kijivu mnamo Februari 2021.
Aidha, Botswana iliongezwa kwenye orodha ya kijivu ya FATF mwaka wa 2018. Mnamo 2021, kufuatia mfululizo wa tathmini kutoka kwa Kundi la Kupambana na Utakatishaji Fedha Mashariki na Kusini mwa Afrika (ESAAMLG), Botswana ilionekana kuafikiana na mapungufu yaliyotajwa hapo awali ya AML/CTF. Hivyo, FATF iliondoa Botswana kutoka kwenye orodha ya kijivu.
Cambodia iliwekwa kwenye orodha ya kijivu mnamo Februari 2019 kutokana na masuala yanayohusu shughuli za kamari na biashara haramu ya binadamu.
Hata hivyo, kufuatia ziara ya FATF Januari 2023, shirika hilo lilibainisha maendeleo makubwa ya nchi katika kuboresha utawala wake wa AML/CFT.
Ingawa nchi itaendelea kufanya kazi na FSRB yake, Kundi la Asia/Pasifiki (APG), Cambodia haiko chini ya ufuatiliaji ulioongezeka na iliondolewa kwenye orodha ya kijivu mnamo Februari 2023.
Pia, Bahamas iliondolewa kwenye orodha ya kijivu mnamo Desemba 2020. FATF ilitaja maendeleo makubwa ya Bahama katika kuimarisha mifumo yake ya AML/CFT kufuatia mapungufu yaliyotambuliwa mwaka wa 2018.
Kama vile Bahamas, Ghana iliongezwa kwenye orodha ya kijivu mwaka wa 2018. Baada ya kukamilisha mpango wake wa kimkakati, FATF iliamua kuwa Ghana ilikuwa imefanya maendeleo ya kutosha ya AML/CTF na kuiondoa kwenye orodha ya kijivu mwaka wa 2021.
Nayo Pakistan imeonekana kwenye orodha ya kijivu ya FATF mara nyingi tangu 2008. Mnamo Juni 2022, FATF ilisema Pakistan itawekwa kwenye orodha hiyo hadi ziara ifanyike ili kuthibitisha maendeleo yake.
Mnamo Oktoba 2022, FATF ilitangaza kwamba Pakistan haitalazimika tena kufuatiliwa kutokana na maendeleo makubwa ya nchi katika kuboresha utawala wake wa AML/CTF.
Vile vile, Morocco iliwekwa kwenye orodha ya kijivu mnamo Februari 2021. Kufuatia ziara iliyofanyika kati ya 16-18 Januari 2023, FATF ilisema kuwa nchi hiyo imeshughulikia mapungufu yake ya kiufundi na haikuwa chini ya ufuatiliaji zaidi.
Baada ya kurejea kwenye orodha ya kijivu Februari 2020, FATF ilitangaza kuwa Nicaragua haikuwa chini ya ufuatiliaji zaidi kufikia Oktoba 2022.
Ingawa FATF ilipongeza Nicaragua kwa kuboresha utawala wake wa AML/CTF, tahadhari kali ilitolewa kuhusu matumizi mabaya ya viwango vya FATF vinavyosababisha kukandamizwa kwa mashirika yasiyo ya faida Nikaragua.
FATF ilihimiza Nikaragua kuhakikisha usimamizi wake wa mashirika yasiyo ya faida unategemea hatari na kulingana na viwango vya FATF.
Katika hatua nyingine, Zimbabwe iliongezwa kwenye orodha ya kijivu mwaka 2019 baada ya tathmini yake kuangazia mapungufu mbalimbali katika utekelezaji wa Viwango vya AML/CTF nchini humo.
Hivyo, kufikia Machi 2022, ripoti ya FATF ilitaja mafanikio makubwa ya Zimbabwe katika kuboresha utawala wake wa AML/CTF na ufanisi wake, na hivyo kuiondoa nchi kutoka kwenye orodha ya kijivu.
Kwa kuzingatia ongezeko la hatari ya utakatishaji fedha na ufadhili wa ugaidi ambayo nchi zilizoorodheshwa kwenye orodha nyeusi na zilizoorodheshwa kijivu zipo, mamlaka nyingi za kifedha zinahitaji makampuni kuwa na ulinzi unaofaa kulingana na AML/CTF ili kupunguza tishio hilo.
Makampuni kwa mujibu wa kikosi kazi hicho lazima yachunguze wateja dhidi ya orodha nyeusi ya FATF na orodha ya kijivu wakati wa kuingia na katika uhusiano wao wote wa kibiashara na kufuatilia miamala yao kila mara.
Ili kukagua kwa usahihi, kampuni zinapaswa kuhakikisha kuwa hatua za umakini wa wateja wao zinathibitisha makazi ya wateja wao katika, au biashara na, nchi zilizoorodheshwa.
Pia wanapaswa kuangalia kama programu yao ya ufuatiliaji wa miamala inaweza kukagua ukubwa, marudio na muundo wa miamala inayohusisha nchi zilizo hatarini zaidi ili kubaini ikiwa shughuli za uhalifu, kama vile utakatishaji fedha zinafanyika.
Hata hivyo, shughuli ya kutiliwa shaka inapogunduliwa, ni lazima kampuni ziwasilishe ripoti za shughuli zinazotiliwa shaka kwa mamlaka zinazofaa za kifedha ili kuchukua hatua za utekelezaji.