Buriani mwanahabari Leila Sheikh

NA ADELADIUS MAKWEGA

JUNI 12, 2023 Mwanakwetu alipata taarifa juu ya kifo cha mwanahabari mkongwe, Bi Leila Sheikh ambaye alikuwa mtetezi wa haki za wanawake katika vyombo habari hapa nchini.
Msiba huo ulimsitua Mwanakwetu na alipofuatilia zaidi alibaini kuwa mazishi yake ni Korogwe Tanga Juni 13, 2023 ambapo Mwanakwetu amemuagiza mkewe akashiriki mazishi ya mama huyo.

Kwa hakika Mwanakwetu ameipokea taarifa ya msiba huo kwa masikitiko makubwa, maana kwa ulimwengu wetu wa sasa watu wengi si kwamba hawajitoi kwa ajili ya watu wengine, wanafanya hivyo lakini kwa maslahi yao binafsi , tofauti na marehemu Bi Leila Sheikh ambaye aliweza kujitoa kwa maslahi makubwa ya wanahabari wanawake kwa wanaume kujenga uimara wa habari Tanzania.

Mwanakwetu anakumbuka mawasiliano ya awali baina yake na Bi Leila Sheikh ni miaka karibu 18 ambapo kufahamiana na mwanahabari huyu kulitokana na Mwanakwetu kusoma sana maandiko yake hasa juu ya wanahabari wanawake walivyokuwa wakikosa fursa nyingi katika vyombo habari kutokana tu na kuwa mwanamke .

“Wanawake wana mambo mengi, kazi hiyo mtumeni mwanaume , itafanyika vizuri.”

Haya yalikuwa maneno ya kawaida katika vyumba vya habari. Unaweza kuona sasa Mkurugenzi wa TSN Bi Tunu Abdallah kuongoza taasisi hiyo kwa sasa ni jambo la kawaida, Mwanakwetu mambo zamani hayakuwa hivyo , zipo simulizi nyingi za kusikitisha ambazo Mwanakwetu hataki kuzisema leo hii lakini mfano mmojawapo hata kwenda kuripoti Vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilikuwa ni mtihani mzito kupangiwa mwanahabari mwanamke.

Mwanakwetu alikuwa akisoma makala nyingi za Bi Leila Sheikh na mara nyingi kuzinukuu makala hizo, hapo ndipo Bi Leila Sheikh akamfahamu Mwanakwetu kwa jina na si jinsia.

Urafiki baina ya Leila Sheikh na Mwanakwetu ulikuja kwa utata ambapo mwanahabari huyu alituma ujumbe Mwanakwetu ajiunge na TAMWA, mjumbe huyo akamjibu kuwa Adeladius Makwega na mwanaume.

“Bwana nilitaka ujiunge na TAMWA, hapa nimeambiwa kumbe wewe ni baba, samahani mwanangu, ukifika Dar es Salaam nitafute tuongee.”

Tangu siku hiyo Iringa Press Club na vyama vingine vya kihabari vikawa na jirani na Mwanakwetu ambaye alikuwa Mwalimu wa Shule ya Sekondari Isimani Tarafani Iringa Vijijini na mwanachuo wa Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa.

Kuna wakati Mwanakwetu aliandika habari na makala katika Gazeti la KULIKONI juu ya Shule ya Msingi Ugele iliyopo katika Manispaa ya Iringa Mjini ambapo ilikuwa na mwalimu mmoja tu huku kaka mkuu akisaidia kufundisha wanafunzi wenzake wa darasa la kwanza, pili , tatu na la nne. Mwanakwetu alifika shuleni hapo na kupiga picha ya tukio hilo na kuandika habari na makala hiyo baada ya kujulishwa hilo na mwanahabari Mpoki Mwakapisu ambaye sasa ni Afisa Habari mkoani Iringa.

Mwanakwetu anakumbuka MISA TAN,TAMWA na Ubalozi wa Marekani Nchini Tanzania walitoa zawadi na vyeti kwa wanahabari walioandika habari za vijijini ambapo Adeladius Makwega alikuwa miongoni mwao, huku akishiriki mafunzo, akapata cheti, akapata pesa na hapo ndipo alikutana uso kwa uso na marehemu Leila Sheikh kwa mara ya kwanza

“Mwanangu mwandishi wa Iringa umekuja ? Umepata posho yako ? Umefikia wapi? Vipi Shule yako ya Ugele walipelekwa walimu? Vipi na yule kaka mkuu alifaulu mtihani wa darasa la saba?”

Mwanakwetu alijibu kuwa amefika, posho yake amepata, amefikia nyumbani kwao Mbagala na Shule ya Msingi Ugele ilipangiwa walimu wa kike wanne, huku walimu watatu wameripoti na mwalimu mmoja aliripoti na kutorudi tena kituo chake kipya cha kazi kutokana na mazingira magumu ya eneo hilo yalivyokuwa wakati huo.

Shule hii ilikuwa na mwalimu mmoja ambaye alikuwa mwanaume hivyo ujio wa walimu watatu hilo lilisaidia mno eneo hilo wakati huo.

Msomaji wangu gazeti la KULIKONI walichapisha habari na makala hayo,MISA TAN, TAMWA na Ubalozi Marekani wakatoa zawadi kwa mwandishi , hapo hapo Afisa Elimu Mkoa wa Iringa alipoona tu Makala hayo wakalifanyia kazi jambo hilo, ambalo leo hii si tatizo tena. TAMWA iliyofanya hivyo ni ya Leila Sheikh ambaye leo hii amefariki dunia.

Inawezekana watu wa Kijiji cha Ugele Iringa Mjini jambo hilo wamelisahau, lakini Mwanakwetu anatumia buriani hii kuwakumbusha hilo kuwa mama huyu amefariki dunia.

Mwanakwetu siku ya leo anasema nini?

Kwa Mwanakwetu, ndiyo kusema Bi Leila kwake ni mama yake kwa maana hata pesa ya kwanza ya kihabari aliipata kwa fursa aliyopewa nayeye.

Mwanakwetu kwa heshima zote anatoa pole kwa wananahabari wote wanaoheshimu mchango wa huyu mama, pili anatoa pole kwa TAMWA kwa kuondokewa na kiongozi wao wa zamani na tatu anatoa pole kwa ndugu na familia yake kwa kumpoteza ndugu yao aliyeliwakilisha vema jina la ukoo wao katika kutenda utu kwa binadamu wenzake.Mwanakwetu upo? Buriani Bi Leila Sheikh.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news