NA DIRAMAKINI
KATIBU wa Chama cha Wanawake Wajane Tanzania (CCWWT) Taifa, Sabrina Tenganamba amendelea kuwahamasisha wanawake wajane nchini kujiunga na chama hicho ili kuweza kukusanya nguvu itakayowawezesha kukabiliana na changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo katika maisha yao.
Amesema, kupitia CCWWT wataweza kuthaminiwa na kuheshimika ndani ya jamii kwani wapo mstari wa mbele kutoa elimu kwa jamii kuhusu wajane ili waweze kutambulika na hatimaye kuthaminiwa ikiwemo kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazowakabili.
Wito huo unakuja ikiwa ni siku chache zimepita baada ya wajane nchini kupitia chama hicho kuiomba Serikali kuwapatia msaada wa kisheria ili kupata haki zao na kusaidiwa huduma ya afya ya akili ili kudhibiti msongo wa mawazo.
Tenganamba alitoa wito huo Juni 23, 2023 jijini Mbeya alipokuwa akiwasilisha risala mbele ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Wajane Duniani.
Alieleza changamoto wanazokumbana nazo wajane kuwa ni pamoja na kusingiziwa kuwauwa waume zao na kunyang'anywa haki zao za mirathi hivyo, wengi kukabiliwa na umaskini mkubwa na kupelekea msongo wa mawazo hata wengine kujiua.
"Lakini pia tunaomba Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) ahakiki kumbukumbu za ndoa, kwani changamoto nyingine zinaletwa na wanaume kuwa na ndoa zilizosajiliwa zaidi ya moja hivyo kuleta shida wakati wa mirathi,"amesema Sabrina.
Aidha, wajane wameomba waunganishwe na mifumo ya benki ili wanufaike na fursa za kiuchumi na kufanya uzalishaji.
Akijibu changamoto hizo, Waziri Mhe.Dkt.Gwajima amesema Serikali itaimarisha zaidi uratibu wa masuala ya wajane na kusimamia Sheria ya Msaada wa Kisheria Na. 1 ya mwaka 2017 kuhakikisha wajane wanapata haki zao.
"Taasisi 125 za kutoa huduma za msaada wa kisheria zimetambuliwa na Wasaidizi wa Kisheria 3,721 wamesajiliwa kote nchini ambapo, mwaka 2021/22 kesi 277 za mirathi ya wajane zilitolewa hukumu ya ushindi,"amesema Waziri Dkt.Gwajima.
Katika kuwaelimisha wajane juu ya fursa za kiuchumi, Dkt.Gwajima ameelekeza uandaliwe mkutano wa Chama cha Wajane na Watendaji wote kupitia mtandao wa kidigitali ili kujadili changamoto zote na kuziwekea mkakati mapema Julai, mwaka huu