Chamwino watakiwa kuzingatia lishe bora

NA DENNIS GONDWE

WANANCHI wa Kata ya Chamwino wametakiwa kuzingatia lishe bora ili kujikinga na udumavu na magonjwa ili wawe na afya njema itakayowawezesha kuzalisha mali. 
Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu Mganga mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Situ Muhunzi alipokuwa akiongea na mamia ya wananchi wa Kata ya Chamwino waliojitokeza katika maadhimisho ya siku ya Afya na Lishe iliyofanyika katika viwanja vya Wajenzi jijini Dodoma. 

Muhunzi alisema “lishe bora ni muhimu kwa maisha ya mwanadamu. Awali Afisa Lishe wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma alitueleza makundi matano ya vyakula yaani wanga, protini, mbogamboga, matunda, mafuta na asali ili kujikinga na udumavu na magonjwa mengine. Kwa Mkoa wa Dodoma bado udumavu upo kwa asilimia 30.7 na miaka mitatu nyuma tulikuwa asilimia 37.” 

Afya na lishe ni muhimu kwa wananchi wote, endeleeni kutumia kutuo cha kutolea huduma za Afya cha Chamwino ili kupata elimu ya lishe na huduma nyingine za afya na tiba. “Na leo hapa tumeleta huduma mbalimbali za kuchungaza hali ya lishe, virusi vya Ukimwi na kupata vitamin A kwa watoto na kufuatilia mapishi ya chakula lishe kilichokuwa kinaandaliwa hapa uwanjani,” alisema. 
Akiongelea afya na lishe, alisema kuwa vinaenda sambamba na ufanyaji wa mazoezi. “Mazoezi ni muhimu katika kujenga na kuboresha afya za wananchi wa Kata ya Chamwino na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa ujumla. Mazoezi yanatukinga na magonjwa yasiyoambukiza ambayo yameibuka kwa wimbi kubwa katika siku hizi. Hivyo, ni muhimu kwa wananchi kufanya mazoezi kama ambavyo tumefanya leo,” alisema Muhunzi. 

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Chamwino, Jumanne Ngede alisema kuwa suala la afya na lishe ni muhimu kusisitizwa katika jamii. 

“Nikushukuru sana Kaimu Mganga mkuu wa Halmashauri ya Jiji na timu yako kwa kuja kutoa elimu katika kata yetu. Afya na lishe ni muhimu na lina maslahi mapana kwa kata yetu na halmashauri yetu. Nitumie nafasi hii kuwaalika tena katika Kata ya Chamwino kuja kutoa elimu ili tuweze kuwasaidia wananchi wetu kutokomeza changamoto zote zitokanazo na lishe duni,” alisema Ngede. 

Aidha, aliwataka wananchi wa kata hiyo kuzingatia elimu watakayopewa katika maadhimisho hayo. “Ndugu zangu maendeleo yanategemea sana afya njema na lishe bora. Bahati nzuri hapa umewekwa na utaratibu wa kufanya mazoezi. Niwaombe tuwe na utamaduni wa kufanya mazoezi, usiishie siku ya leo tu bali wananchi tuwe na tabia ya kufanya mazoezi kila siku ili tuimarishe kinga ya miili yetu,” alisisitiza Ngede.
Maadhimsiho ya Siku ya Afya na Lishe katika Kaya ya Chamwino yaliongozwa na kaulimbiu isemayo “Lishe bora kwa ustawi wa afya zetu na maendeleo ya kata yetu.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news