NA MWANDISHI WETU
KIJIJI cha Chandama wilayani Chemba mkoani Dodoma ni miongoni mwa vijiji vilivyopatiwa fedha na Serikali kiasi cha shilingi milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati.
Akiwasalimia wakazi wa Chandama katika ziara ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi ambaye hii leo yuko wilayani Chemba, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amesema fedha hizo zimeendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya.
"Wilaya ya Chemba imepatiwa fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 14 kwa ajili ya miradi ya maendeo ikiwa ni pamoja na afya, elimu, miundombinu, nishati na maji.
"Pia tuna miradi mikubwa miwili ya kimkakati ambayo ni ujenzi wa barabara kati ya Singida na Manyara na ujenzi wa bwawa la Farkwa ambalo kukamilika kwake kutasaidia upatikanaji wa maji ya uhakika," Senyamule amesisitiza.
Senyamule pia ametumia hadhara hiyo kukemea vikali vitendo vya unyanyasaji wa kijiinsia vinavyofanywa na baadhi ya wanaume katika Kijiji cha Chandama na kuonya kuwa hatua kali za kisheria zitachukiwa dhidi ya wote watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Daniel Chongolo kwa nyakati tofauti ametoa msukumo katika suala la elimu kwa kuhimiza jamii kuacha mila potofu za kutoelimisha watoto wa kike na kiume.
"Acheni kuwaozesha watoto mapema, acheni kuwapeleka mijini kufanya kazi za ndani, simamieni mila, desturi na maadili yetu ya kitanzania. Wazazi timizeni wajibu wenu. Acheni kulea watoto kama mayai, biskuti ama boksi,"Chongolo amekemea.
Ziara ya ndugu Daniel Chongolo mkoani Dodoma imeingia siku ya sita hii akiwa Chemba kukagua miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na miradi ya Afya, Elimu, miundombinu, nishati na maji.