NA ADELADIUS MAKWEGA
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini, Saidi Yakub tarehe 2 Juni, 2023 akiwa Kwimba-Mwanza amesema kuwa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya kinaelekea kuwa cha Kimataifa kwani sasa Serikali imepanga kukitangaza zaidi ili wanachuo kutoka mataifa mengine katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati wajiunge nacho.
“Kwa takwimu tulizo nazo, Tanzania tangu uhuru imewasomesha wataalamu wa michezo wanaokaribia 2000 ambapo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimetoa wataalamu 704 na Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya kimetoa wataalamu 701, na juhudi ya kuyafikia malengo hayo ya kimataifa zinaendelea.”
Akizungumza mbele ya Katibu Mkuu Yakub, Mkuu wa Chuo cha Maedeleo ya Michezo Malya ndugu Richard Mganga alizitaja changamoto kadhaa zinazokikabili chuo chake zikiwamo uhaba wa wakufunzi na hali duni ya miundo mbinu huku changamoto hizo zikifanana na zile zilizotolewa na Rais wa Serikali ya Wanachuo Baptist Kapinga.
“Tunaomba serikali yetu tukufu ilifanyie kazi suala la walimu wanaosoma kozi za michezo maana sasa wanakabiliwa na kushushwa madaraja wanapokuwa maafisa michezo wanapochaguliwa katika nafasi hizo wakirudi katika Halmashauri wanazofanyia kazi.”
Akilijibu hilo Katibu Mkuu Yakub alisema,“Hilo serikali imeliona, kwa sababu Rais Samia Suluhu Hassan amewapandisha madaraja watumishi wa umma nchi nzima alafu tena mtumishi huyo huyo anatumia muda wake kufanya mafunzo alafu akirudi kazini inakuwaje ashushwe cheo kwa kukitumikia cheo alichokisomea? "Tumekubaliana, wizara ninayoiongoza, wizara ya Utumishi na TAMISEMI tutakaa pamoja kulipatia ufumbuzi jambo hilo.”
Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wa Chuo hicho Kaimu mwenyekiti wa wafanyakazi Mohammed Mwinduchi alimuomba Katibu MKuu Yakub kuwapatia basi linaloweza kuwasaidia kushiriki mafunzo mbalimbali nje ya chuo hicho, huku Katibu Mkuu Yakub akitoa uhakika kuwa pale chuo wanapohitaji usafiri huo wizara itawapatia basi kutoka Dodoma lakini hapo mbeleni wizara inaweka utaratibu wa kununua basi jipya.
Kabla ya Katibu Mkuu Yakub kuzungumza na umma huu wa wasomi hao wa michezo katika viwanja vya ndani vya viunga vya chuo hiki , Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini Ali Mayay Tembele alimshukuru mno Katibu Mkuu Yakub kwa kuwa jirani naye kutembelea taasisi ambayo ipo chini ya Sekta ya Maendeleo ya Michezo nchini na hilo linaonesha namna uongozi wake ulivyo na maono ya mbali.
Katibu Mkuu Yakub aliwasili chuoni hapo saa 4.25 ya asubuhi na kupanda Mti Maji (MDODOMA) wa kutembelea maeneo mbali ya chuo hiki ikiwamo mabweni,miradi ya ujenzi wa majengo kadhaa madarasa, kumbi za michezo na nyumba za watumishi akijionea hali halisi ilivyo.