DCEA yateketeza bangi magunia 731, hekari 308 ndani ya siku mbili Arusha

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini Tanzania (DCEA) imefanya operesheni kwa siku mbili mfululizo katika vijiji vya Kisimiri Juu na Lesinoni wilayani Arumeru mkoani Arusha na kukamata magunia 731 ya bangi kavu pamoja na kuteketeza hekari 308 za mashamba ya bangi mbichi.
Kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, sura ya 95, kilimo na biashara ya bangi katika Taifa letu ni kosa la jinai. Kwa hiyo, kujihusisha kwa namna yoyote na bangi (kulima, kuuza, kuhifadhi, kutumia, kuichakata, nk) ni kosa la jinai na adhabu yake inafikia hadi kifungo cha maisha jela.

Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amebainisha leo Juni 2, 2023 kuwa, katika Kijiji cha Kisimiri Juu,DCEA ilikamata magunia 482 na kutekeleza hekari 101 za mashamba ya bangi.

Aidha, katika Kijiji cha Lesinoni mamlaka hiyo ilikamata magunia 249 ya bangi kavu na kuteketeza hekari 207 ambapo jumla ya watuhumiwa tisa wamekamatwa na dawa hizo za kulevya.

Kamishna Jenerali Lyimo amefafanua kuwa, ukamataji huo umefanyika Mei 31 hadi Juni Mosi, mwaka huu kufuatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan la kufanya operesheni nchi nzima.

Lengo ni kuhakikisha dawa za kulevya zinatokomezwa nchini. Aidha, kwa mujibu wa Kamishna Jenerali Lyimo, operesheni hizo zimefanyika siku moja baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera na Bunge), Mheshimiwa Jenista Mhagama (Mb) kutoa taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya nchini kwa mwaka 2022 ambayo alitaja mikoa ya Arusha, Iringa,Morogoro na Manyara kujihusisha na kilimo cha bangi kwa kiasi kikubwa.

Amefafanua kuwa, DCEA kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama nchini inaendelea kufanya operesheni za mara kwa mara katika maeneo yote nchini ili kuhakikisha kilimo cha bangi, mirungi na dawa zingine za kulevya zinatokomezwa kabisa na wananchi kujikita katika kilimo cha mazao mbadala ya biashara na chakula.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

  1. Nafikiri kuna haja ya kufikiri njia mbadala ya kuwasaidia watu wanaojihusisha na kilimo/biashara hii. Ni kiasi kikubwa sana hiki.

    ReplyDelete
Previous Post Next Post

International news