DCEA:Ukikutwa na dawa za kulevya iwe nyumbani, kwenye gari unakamatwa na mali zote zinataifishwa

NA GODFREY NNKO

KAMISHNA Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo amesema kuwa, sheria inasema iwapo ukikutwa na aina zozote za dawa za kulevya bila kujali ni mali yako au ya mtu mwingine inakutambua kwamba wewe ndiye muhusika.
Hayo ameyabainisha leo Juni 21, 2023 kupitia mahojiano ya moja kwa moja na kipindi cha Clouds 360 cha Clouds TV ambapo ametoa ufafanuzi wa mbinu zinazotumiwa na wafanyabiashara wa dawa za kulevya hususani raia wa kigeni kuwatumia wanawake wa kitanzania kufanikisha biashara zao.

Aidha, ameeleza namna Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ilivyojipanga katika kuhakikisha biashara ya dawa za kulevya inatokomea nchini.

"Tunapozifungua dawa za kulevya mbele yake au mashaidi, wanaanza kusema , hatukujua ndani kulikuwa kuna nini, hatukujua kama kulikuwa na dawa za kulevya, lakini sheria inasema ukikutwa na dawa za kulevya wewe ndiye muhusika wa dawa za kulevya na dawa za kulevya zikiwa ndani.

"Hata nyumba ambayo imekutwa imehifadhiwa dawa za kulevya, pia inakuwa inaingia kwenye kesi, na mwisho wa siku, inataifishwa ikiwa dawa za kulevya zimekutwa kwenye gari, hilo gari na lenyewe linaingia kwenye kesi na mwisho wa siku baada ya kesi, linataifishwa linakuwa mali ya Serikali.

"Kwa hiyo mara nyingi ndiyo maana tunawaasa wadada hao kwamba mara zote wawe makini na wapenzi wanaokuwa nao, lakini wawe makini kupokea vifurushi ambavyo hawajui ndani kuna nini, na katika operesheni hii tuliyoifanya hizo kilo 200.5 tulizozikamata katika kipindi hiki cha muda mfupi.

"Asilimia 90 ya dawa zote tulizokamata nyingi, zilikuwa zinahifadhiwa na wadada, hawa wadada tayari tumeshawakamata na tayari wengi wao wameshafikishwa mahakamani na wengine wapo magerezani. Wengi (wageni hao) wanaingia kwamba wanakuja kufanya biashara,"amebainisha Kamishna Jenerali Aretas Lyimo.

Pia, Kamishna Jenerali Aretas Lyimo amewataka wananchi kuwa makini na mizigo wanayopewa kubeba au kuhifadhi pasipo kujua ndani yake kuna nini. 

"Wanawake wanatakiwa kuwa makini zaidi kwani katika baadhi ya matukio, wamekuwa wakitumiwa na wapenzi wao hasa raia wa kigeni kusafirisha na kupokea mizigo wasiyoijua na wakati mwingine mizigo hiyo huwa na dawa za kulevya na hivyo hujikuta matatani."
Kamishna Jenerali Aretas Lyimo amefafanua kuwa, Kifungu cha 15 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kinaeleza kwamba, ni kosa kusafirisha dawa za kulevya, na mtu yoyote akithibitika kutenda kosa hilo atawajibishwa kisheria ikiwa ni pamoja na kifungo kisichopungua miaka 30 au kifungo cha maisha gerezani.

Wakati huo huo, Kamishna Jenerali Aretas Lyimo amesema, Serikali imejipanga ipasavyo kuhakikisha inamaliza tatizo la dawa za kulevya kwa ustawi wa jamii. 

Amesema, kutokana na kuwepo madhara makubwa ya kiuchumi, kijamii na kisaikolojia yanayotokana na matumizi ya dawa za kulevya, ni vema wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali kwa kuwafichua wote wanaojihusisha na matumizi na biashara ya dawa za kulevya.

"Ni ili kwa pamoja tuweze kulikomboa taifa kutoka katika janga hili.Aidha, katika kuhakikisha biashara na matumizi ya dawa za kulevya yanatokomea nchini. Mamlaka imejikita katika utoaji wa elimu juu ya tatizo la dawa za kulevya kwa jamii. 

"Ili kupanua wigo wa utoaji elimu,mamlaka imeingia makubaliano na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kutumia klabu zao zilizokwisha anzishwa kwenye shule na vyuo kutoa elimu juu ya tatizo la dawa za kulevya. Hivyo, elimu ya kupambana na rushwa na dawa za kulevya itatolewa kupitia klabu hizo,"amefafanua Kamishna Jenerali Aretas Lyimo.

Kwa upande mwingine, Kamishna Jenerali Aretas Lyimo ametumia mahojiano hayo kuwaalika wananchi wa Mkoa wa Arusha na mikoa ya jirani kushiriki katika maadhimisho ya siku ya kupiga vita dawa za kulevya ambayo yataanza Juni 23 na kilele chake ni Juni 25, 2023.

Amesema, katika maadhimisho hayo ambayo yatafanyika jijini Arusha katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mgeni rasmi siku ya kilele atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan. Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni “Tuzingatie Utu na Kuboresha Huduma za Kinga na Tiba” .

Ukamataji

Juni 19, 2023 Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo aliwaeleza waandishi wa habara jijini Dar es Salaam kuwa, mamlaka hiyo kwa kushirikiana na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama ilifanya operesheni katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Kilimanjaro na Arusha na kufanikiwa kukamata dawa za kulevya aina mbalimbali.

Miongoni mwa dawa hizo ni heroin kilogramu 200.5, bangi kavu iliyokuwa tayari kusafirishwa gunia 978, bangi mbichi gunia 5,465, bangi iliyosindikwa (skanka) kilogramu 1.5, methamphetamine gramu 531.43,heroin kete 3,878, cocaine kete 138, mililita 3,840 za dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Pethidine pamoja na kuteketeza ekari 1,093 za mashamba ya bangi. 

Aidha, alibainisha kuwa, mamlaka hiyo kwa kushirikiana na Bodi ya Kimataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya (INCB) Mamlaka imezuia kuingia nchini jumla ya kilogramu 1,507.46 za kemikali bashirifu ambazo zingeweza kutumika kutengenezea dawa za kulevya.

Ukamataji huo uliofanyika kuanzia Machi 25, 2023 hadi Juni 19 2023 unahusisha watuhumiwa 109 wakiwemo raia watatu wa kigeni. 

Alisema, baadhi ya watuhumiwa wamefikishwa mahakamani na wengine wanatarajiwa kufikishwa mahakamani taratibu za kisheria zitakapokamilika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news