Diwani wa bando tatu, hiyo wala siyo bora

NA LWAGA MWAMBANDE

DIWANI hapa nchini ni mwakilishi wa wananchi wa kata yake, pia ni mwakilishi wao katika vikao vya Baraza la Madiwani la halmashauri anayoitumikia iwe wilaya,mji, manispaa au jiji kama ilivyoridhiwa katika Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ya mwaka 1977 sura No.292-14(1).

Aidha, diwani pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kata (WDC) kama ilivyoandikwa katika Sheria ya Serikali za mitaa No.7(31) ya mwaka 1982, iliyofanyiwa marekebisho na sheria No.6 ya mwaka 1999.

Kwa mujibu wa mabadiliko ya sheria yaliyofanywa na Sheria Na.6 ya 1999, Diwani ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kata kwa wadhifa wake.

Hakuna shaka kwamba, Diwani atatumia vikao vya kamati hiyo kuwasilisha rasmi maamuzi na mapendekezo ya kamati kwenye vikao vya halmashauri na kufikisha maamuzi ya halmashauri kwenye ngazi za chini ya Serikali za Mitaa.

Diwani pia ni mtunzi, mpitishaji, mwidhinishaji na msimamizi wa sheria ndogondogo zinazotungwa kwenye kata yake kwa ajili ya kuwaletea wananchi maendeleo kama ilivyoridhiwa katika sheria ya serikali za mitaa ya mwaka 1977 sura No.287-153(1) [mamlaka ya mji] na katika sura No.288-89 na 122(1) (d) [mamlaka ya wilaya].

Mbali na majukumu mengi aliyonayo, muhimu zaidi diwani anawajibika kuwahamasisha na kuwaelimisha wananchi kutambua umuhimu wa kulipa kodi na ushuru wa halmashauri ili waweze kupatiwa huduma bora.

Sambamba na kuhakikisha kuwa fedha za halmashauri zinakusanywa na kutumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa na kwamba matumizi hayo hayavuki bajeti iliyoidhinishwa.

Aidha, ili madiwani waweze kuwakilisha, kuwaongoza na kuwahudumia wananchi kama inavyostahili, ni budi wawe karibu na wananchi wakati wote kufahamu hali halisi ilivyo na matarajio ya wananchi kuhusiana na hali iliyopo kwa upande wa shughuli za maendeleo na utoaji wa huduma. 
 
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwmabande anasisitiza kuwa, mara zote heshima ya diwani ni makusanyo na huduma bora kwa wananchi. Endelea;

1.Diwani wa bando tatu, hiyo wala siyo bora,
Kusanya mapato yetu, ondoa yanayokera,
Utaonekana mtu, si bidhaa chotora,
Heshima ni makusanyo, huduma kwa wananchi.

2.Kwamba mtu anakuja, kama vile akuchora,
Bando tatu ana hoja, akunywesha barabara,
Na kwake wawa mteja, hiyo yaleta hasira,
Heshima ni makusanyo, huduma kwa wananchi.

3.Diwani ni kiongozi, itunze yako taswira,
Wewe iwe kazikazi, huduma bora ishara,
Hawatakuja madwanzi, kufanya yenye hasara,
Heshima ni makusanyo, huduma kwa wananchi.

4.Jukumu lenu ni kubwa, hata zaeleza sera,
Mnao umma mkubwa, na mambo mengi yakera,
Watu hawali ubwabwa, changamoto zinafura,
Heshima ni makusanyo, huduma kwa wananchi.

5.RCii Chalamila, kasema maneno bora,
Mna kura siyo kula, ondoa yanayokera,
Yote ya kumbwelambwela, safisheni barabara,
Heshima ni makusanyo, huduma kwa wananchi.

Makusanyo Serikali, yanafanya iwe bora,
Hapo inafika mbali, mipango yake kuchora,
Hata kura za halali, wajumbe hawatakera,
Heshima ni makusanyo, huduma kwa wananchi.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news