NA MWANDISHI WETU
WMJJWM,DODOMA
SERIKALI inaendelea kushirikiana na taasisi za kisayansi nchini zinazofanya tafiti mbalimbali na kuja Majawabu ya kisayansi yanayowezesha kupata suluhu za kuinua uzalishaji na vipato vya makundi maalum.
Akifungua Mafunzo ya utengenezaji wa Vijarida sera vitakavyotatua changamoto za Makundi Maalum, Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu ameelezea ni namna gani Sayansi na teknolojia inaweza kutumika katika kusaidia kupata majawabu yenye ushahidi ili kusaidia makundi maalum.
“Matarajio yetu juu ya kikao kazi hiki ni Makubwa kwani tunatarajia majawabu yenye ushahidi na yanatokelezeka ili kupata njia nzuri zaidi za kusaidia Makundi Maalum katika kuinua hali yao ya kiuchumi,"amesema Dkt.Jingu.
Amesema, mazingira yanaruhusu kuja na majawabu yenye ushahidi kwani miundo mbinu ipo na imesambaa nchini ikiwemo barabara, nishati, taasisi binafsi na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa idara ya Makundi Maalum kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Juma Samwel amesema, Serikali inapambana kuhakikisha wafanyabiashara ndogondogo wanakua kiuchumi.
“Tunatamani Makundi haya maalum yaweze kurahisishiwa mazingira ya kufanyia kazi kwa kushirikishwa kwa ukaribu katika masuala yanayowahusu lakini pia mamlaka husika na yanayowagusa wazalishaji hawa wadogo kufanya nao kazi kwa ukaribu ili kurahisisha uzalishaji wao kwa mfano Latra kuweza kuongeza ukaribu nao ikiwemo kuwaelemisha juu ya masuala mbalimbali.”