NA MWANDISHI WETU
NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt.Grace Magembe ametoa wito kwa wananchi kuwa na desturi ya kufanya mazoezi mara kwa mara ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.
Dkt.Magembe amesema hayo leo Juni 11,2023 jijini Dodoma katika mbio za mashindano ya nne ya tamasha la riadha la Makao makuu lijulikanalo kama “Capital City Marathon katika viwanja vya Chimwaga Chuo Kikuu cha Dodoma.
Dkt.Magembe amesema ni muhimu kila Mtanzania kuona umuhimu wa kufanya mazoezi kwa ajili ya kujikinga na magonjwa mbalimbali yasiyoambukiza ikiwemo matatizo ya Moyo,Shinikizo la juu la damu.
“Kwa upande wa afya mazoezi ni zaidi tu ya mazoezi, ni Tib ana Kinga dhidi ya Magonjwa mbalimbali kama vile magonjwa ya Moyo, Shinikizo la Juu la Damu, Figo,Saratani,yote haya yanasababishwa na mienendo yetu ya tabia jinsi tunavyoishi hatufanyi mazoezi,tunakula chakula kingi kuliko mwili ambavyo unahitaji, unapofanya mazoezi unapunguza uwezekano wa kupata magonjwa haya,”amesema Dkt.Magembe.Aidha, Dkt.Magembe amesema Wizara ya Afya itaendelea kushirikiana na Wizara zingine kuwa na siku maalum ya mazoezi kwa watumishi angalau mara moja kwa mwezi katika mji wa Serikali Mtumba ili kuendelea kuimarisha afya za Watumishi katika kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Magonjwa yasiyoambukiza(NCD) kutoka Wizara ya Afya Dkt.Omary Ubuguyu amesema katika ulimwengu wa sasa kuna wimbi kubwa la vijana hawafanyi mazoezi kutokana na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia hivyo ni muhimu kila mmoja kuwajibika kufanya mazoezi.
“Mazoezi yanaimarisha mwili kwa kuondoa msongo wa mawazo ni muhimu kila mmoja kufanya mazoezi,”amesema.
Mratibu wa Capital City Marathon ambaye pia Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni inayojishughulisha na michezo ya Dodoma Sports Nsolo Mlozi ametumia fursa hiyo kuishukuru Wizara ya Afya pamoja na wadau wengine katika kuhamasisha mazoezi huku mmoja wa washiriki wa mbio hizo ambaye Shukuru Mbota akitoa wito kwa watu wengine kuendelea kuwa na desturi ya kushiriki bila kujali hali walizonazo kwani hata wenye ulemavu wana uwezo mkubwa.
Makundi ya walioshiriki mbio hizo ni pamoja na wakimbiaji wa kilometa 21,kilometa 10 na makundi maalum.