HEKARI 16 ZATENGWA UJENZI WA HOSPITALI YA MKOA WILAYANI UKEREWE

NA MWANDISHI WETU
WAF-Ukerewe

ZAIDI ya hekari 16 zimetengwa katika Wilaya ya Ukerewe, Kata ya Bulamba Kijiji cha Bukindo kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali yenye hadhi ya Mkoa itakayosogeza karibu upatikanaji wa hudumu bora za afya. 
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu mara baada ya kukagua eneo la hekari 16 ambapo patajengwa Hospitali yenye hadhi ya Mkoa.

“Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe ambayo ilitarajiwa kuwa ya Mkoa kwa sasa itaendelea kuwa Hospitali ya Wilaya ambapo Hospitali ya Mkoa itajengwa Katika Kata ya Bulamba kijiji hiki cha Bukindo,” amefafanua Waziri Ummy.

Waziri Ummy amesema kwa kushirikiana na wataalam wake ameridhishwa na eneo hilo na sasa hatua ya uchoraji wa ramani unaanza ili kuwezesha kujua thamani ya ujenzi huo ambapo ujenzi wa Hospitali hiyo unatarajia kuanza mapema iwezekanavyo.

“Hospitali hii itakayojengwa hapa itakuwa chachu katika utoaji wa huduma bora za afya ikiwemo za upasuaji, magonjwa ya wanawake na uzazi pamoja na utolewaji wa huduma za magonjwa ya watoto,”amesema waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy amewataka wananchi hao wa Wilaya ya Ukerewe kutoa ushirikiano pindi ujenzi huo utakapoanza hadi ukimalizika kwakuwa watapata fursa ya kufanya kazi za ujenzi lakini pia wenye uwezo wajenge nyumba kwakuwa kutakuwepo na watumishi zaidi ya 50 katika hospitali hiyo. 

“Ndugu zangu Wana-Ukerewe nawaomba sana mtoe ushirikiano pindi ujenzi huu utakapoanza hadi kukamilika kwake, tutoe ushirikiano kwa watumishi wa afya wakituambia tujenge vyoo bora tujenge ili tuweze kujikinga na magonjwa ya milipuko kama kipindupindu lakini pia tuwapeleke watoto kupata chanjo,”amesema Waziri Ummy.

Pia, Waziri Ummy amesema sababu ya kujengwa kwa hospitali hiyo ni maamuzi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan baada ya kuona changamoto wanayoipata wananchi wa Ukerewe. 

“Baada ya Mhe. Rais kusikia kilio cha Wana-Ukerewe amefanya maamuzi bora ya kuwaletea hospitali hii ambayo itakua ni ghorofa mbili, hii haijawahi kutokeani kwa sababu ya mapenzi yake kwenu,”amesema Waziri Ummy.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Mhe. Hassan Bomboko ameomba kuongezewa Madaktari, Daktari Bigwa, wataalamu wa afya kwakuwa uhitaji ni mkubwa katika eneo hilo.

“Lakini pia nikushukuru sana Mhe. Waziri kwa kuja kufanya ziara hapa na kumpelekea kilio chetu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na hakika mmetuheshimisha kutujengea hospitali na kwa kuwa itakua suluhisho la chamgamoto za upatikanaji wa huduma za afy,”amesema Mhe. Bomboko.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news