HII SIKU YA MTOTO,WANATAKA MALEZI

NA LWAGA MWAMBANDE

KILA Ifikapo Juni 16 ya mwaka huwa ni maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika. Chimbuko la maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika ni tukio la mauaji ya watoto takribani 2,000 yaliyofanywa Juni 16, 1976 na askari wa utawala wa Makaburu katika Kitongoji cha Soweto nchini Afrika Kusini.

Watoto wakiwa wameshika mabango yenye jumbe mbalimbali katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika mwaka 2016.(Picha na VOA).

Mauaji hayo yalitokea wakati askari hao wanazuia maandamano ya watoto waliokuwa wanapinga mfumo wa elimu ya kibaguzi iliyokuwa inatolewa na utawala wa Makaburu.

Aidha, katika kukumbuka siku hii, Umoja wa Nchi za Afrika mnamo mwaka 1991 uliweka Azimio la kuifanya siku ya Juni 16 ya kila mwaka kuwa siku maalum ya kuwaenzi mashujaa watoto waliokufa kwa ajili ya kudai haki yao ya kuendelezwa kielimu bila ubaguzi na hivyo kuitwa Siku ya Mtoto wa Afrika.

Kuanzia hapo maadhimisho hayo yamekuwa yakifanyika kila mwaka katika nchi wanachama kwa kufanya tathmini kuhusu hali ya utoaji wa haki ya mtoto na huduma zinazohusu malezi, makuzi na maendeleo ya mtoto.

Mwaka huu wa 2023 kauli mbiu iliyoongoza maadhimisho ni “Zingatia Usalama wa Mtoto katika Ulimwengu wa Kidijitali”.

Kauli mbiu hiyo inaelekeza watoto, wazazi na wanajamii kuchukua hatua za makusudi za kutetea haki za watoto zilizoainishwa katika Sera ya Mtoto (2008) ambazo ni Haki ya Kuishi, Kuendelezwa, Kulindwa, Kushiriki na Haki ya Kutobaguliwa kwa namna yoyote akiwa nyumbani, shuleni au kwenye jamii.

Aidha, siku hii inatukumbusha wadau wote wa watoto wajibu wetu wa kumlinda mtoto dhidi ya vitendo vya ukatili, hususani ukatili unaoibuka sasa hivi ambao ni ukatili wa kwenye mitandao unaotokana na matumizi yasiyo sahihi ya vifaa vya kielektroniki kwa kuingia kwenye mitandao na kujikuta wanafanyiwa ukatili wa aina mbalimbali.

Sambamba na vitisho na kurubuniwa au kushawishiwa kuonesha au kuoneshwa maudhui ya ngono kwa njia ya picha au video, hali hiyo hupelekea hata kufanyiwa au kufanyishwa vitendo vya kingono mitandaoni. Mshairi wa kisasa,Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, malezi ya watoto ni jukumu la kila mzazi ili kumwandalia leo na kesho yake bora. Endelea;


1.Binti ya rafiki yako, huyo ni mtoto wako,
Mvulana mwana wako, huyo pia ni mwanako,
Wataka malezi yako, pia uongozi wako,
Hii siku ya mtoto, ni yule wako na wake.

2.Ukijaliwa mtoto, huyo ndiye kesho yako,
Ukimjenga mtoto, unajenga kesho yako,
Jambo hilo la mvuto, katika maisha yako.
Hii siku ya mtoto, ni yule wako na wake.

3.Ukimpeleka shule, hiyo ni faida kwako,
Ukimuwezesha ale, huo ni wajibu wako,
Jinsi anasonga mbele, wajenga taifa lako,
Hii siku ya mtoto, ni yule wako na wake.

4.Mwana usimdhulumu, hivyo siyo vema kwako,
Usimpe hali ngumu, Unaua kesho yako,
Uliko pata salamu, badili mwenendo wako,
Hii siku ya mtoto, ni yule wako na wake.

5.Kufanya kazi adili, kufundisha kazi yako,
Aelewe kwa akili, yasemavyo maandiko,
Asofanya kazi hali, hakuna madikodiko,
Hii siku ya mtoto, ni yule wako na wake.

6.Kazi si kutumikishwa, huyo ni mtoto wako,
Wala si kulazimishwa, hata kuchapwa viboko,
Ni sawa na kula rushwa, maangamizi yako,
Hii siku ya mtoto, ni yule wako na wake.

7.Mtoto huyo yatima, mama na baba hawako,
Na wewe mtu mzima, malezi jukumu lako,
Usifanye uhasama, atengwe na wana wako,
Hii siku ya mtoto, ni yule wako na wake.

8.Alivyoachiwa mali, ziko mikononi mwako,
Uzitunze kwelikweli, ni za kwake si za kwako,
Kumdhulumu muhali, usifanye hivyo kwako,
Hii siku ya mtoto, ni yule wako na wake.

9.Mali zake zizalishe, hilo ni jukumu lako,
Na shuleni mfikishe, huo ni ulezi wako,
Akue mkabidhishe, na yawepo maandiko,
Hii siku ya mtoto, ni yule wako na wake.

10.Heri ziwafike wote, watoto huko mliko,
Wazazi walezi wote, kwetu mnayo mashiko,
Tuko na ninyi popote, kwa malezi na mshiko,
Hii siku ya mtoto, ni yule wako na wake.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news