HILI TATIZO LA DOLA LIKO KOTE DUNIANI

NA LWAGA MWAMBANDE

JUNI 12, 2023 Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa semina kwa waheshimiwa wabunge jijini Dodoma kuhusu mwenendo wa uchumi wa Dunia, athari za mwenendo huo kwenye upatikanaji wa fedha za kigeni, na hatua zinazochukuliwa na Benki Kuu kukabiliana na hali ya fedha za kigeni nchini.

Semina hiyo, chini ya uenyekiti wa Naibu Spika,Mheshimiwa Musa Azzan Zungu ilifanyika katika Ukumbi wa Pius Msekwa na Ujumbe wa Benki Kuu uliongozwa na Gavana, Bw.Emmanuel Tutuba na wasilisho kufanywa na Mkurugenzi wa Utafiti na Sera za Uchumi, Dkt.Suleiman Missango.

Katika wasilisho hizo imeelezwa kwamba kuanzia mwaka 2022 hadi hivi sasa, mwenendo wa uchumi wa Dunia umekuwa sio wa kuridhisha kutokana na kukabiliwa athari za UVIKO-19, vita ya Urusi na Ukraine na mabadiliko ya tabianchi.

Changamoto hizo zimeathiri mwenendo wa uchumi nchi mbalimbali, ikiwemo Tanzania na kwamba serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kukabiliana na changamoto zilizojitokeza.

Dkt.Missango alisema athari za mwenendo wa uchumi wa dunia kwa fedha za kigeni nchini ni pamoja na kuongezeka kwa nakisi ya urari wa malipo kwa asilimia 127.3 katika kipindi cha mwaka mmoja hadi Disemba 2022 kutoka mwaka 2021 na nakisi ya urari wa malipo ni hasi kwa kiasi cha dola bilioni 5.4 kutoka dola bilioni 2.4 mwaka 2022.

Kutokana na hali hiyo, alisema tangu mwaka 2022, fedha za kigeni nchini zimekuwa zikipungua kutokana na kupungua kwa fedha za kigeni kutoka vyanzo mbalimbali kutokana na sera zilizochukuliwa na Benki Kuu za nchi zilizoendelea, uwekezaji katika masoko ya fedha kuelekea nchini Marekani na hivyo kusababisha kupungua kwa mikopo na misaada kutoka nchi za nje.

Aidha, ongezeko la bei za bidhaa katika soko la dunia, hususani mwaka 2022, kama za mafuta, chakula na mbolea, kugharamia miradi ya maendeleo na kulipa madeni ya nje, kumechangia pia kupungua kwa fedha za kigeni

Hatua zinazochukuliwa na Benki Kuu kukabili hali hiyo ni pamoja na kuendelea kuuza dola milioni mbili kila siku katika soko, kununua dhahabu yenye thamani ya dola milioni 280 kwa mwaka, sawa na tani sita ili kukuza akiba ya fedha za kigeni. Mpaka sasa imeshanunua kilo 418 kutoka kwa Serikali.

Hatua zingine ni kupata fedha za kigeni kutoka kwa mabenki ya ndani na nje kwa njia ya currency swap, kuuza akiba ya Kwacha za Zambia zilizopo kwenye akaunti ya Benki Kuu ya Tanzania iliyopo Benki Kuu ya Zambia, kuendelea kutekeleza sera ya fedha inayolenga kupunguza ukwasi wa shilingi kwenye uchumi.

Pia, kutoa leseni za maduka ya kubadilisha fedha za kigeni katika maeneo mengi nchini ili kuongeza fedha za kigeni kwenye mzunguko rasmi.

Aidha, hivi karibuni Benki Kuu imetoa sekula kwa mabenki ambayo imeanza kutumika Juni Mosi, 2023 yenye lengo la kudhibiti fedha za kigeni.

Matarajio ni kuanza kuongezeka kwa akiba ya fedha za kigeni kutokana na kwamba bei za bidhaa katika soko la dunia, hususani mafuta, zinaendelea kushuka hivyo mahitaji ya fedha za kigeni yatapungua.

Aidha, kipindi cha Julai hadi Septemba ni msimu wa utalii na mauzo ya mazao ya biashara, hivyo inatarajiwa kwamba upatikanaji wa fedha za kigeni utaongezeka.

Pamoja na hatua na hali hiyo, wananchi wamehimizwa kuongeza matumizi ya bidhaa zinazozalishwa hapa nchini na kutumia fedha za kigeni zilizopo kwa uangalifu kwa kuagiza bidhaa ambazo ni muhimu na zisizozalishwa hapa nchini, hasa katika kipindi hiki ambacho nchi inakabiliana na changamoto hii ya dunia. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anabainisha kuwa, hili tatizo la dola, liko kote duniani. Endelea;

1.Hili tatizo la dola, liko kote duniani,
Tunafukuzia dola, kwa ile yake thamani,
Biashara pata dola, pesa kubwa duniani,
Changamoto hizi zote, ndizo twapambana nazo.

2.Athari za matukio, yalokuja duniani,
Ni sababu kubwa hio, dunia i taabuni,
UVIKO athari hio, yatutesa duniani,
Changamoto hizi zote, ndizo twapambana nazo.

3.Urusi na Ukraine, nchi zilizo vitani,
Ndiyo athari nyingine, kotekote duniani,
Tanzania na kwingine, athari hadi jikoni,
Changamoto hizi zote, ndizo twapambana nazo.

4.Vita vimetufumbua, macho na masikioni,
Ndio sasa twatambua, mahitaji duniani,
Kumbe tukiyachambua, hatuna kitu nyumbani,
Changamoto hizi zote, ndizo twapambana nazo.

5.Nishati kwa wingi huko, iko nyingi visimani,
Urusi ni nyingi huko, yasambazwa duniani,
Tokana na vita huko, ugavi uko shidani,
Changamoto hizi zote, ndizo twapambana nazo.

6.Ngano kwa wala mikate, kinara ni Ukraini,
Walime ngano walete, sisi tuko furahani,
Sasa na shida wapate, kwa vile wako vitani,
Changamoto hizi zote, ndizo twapambana nazo.

7.Na hii tabianchi, inatamba duniani,
Ardhi kuweka uchi, miti ni ya msituni,
Tusikae kwa makochi, sote twendeni kazini,
Changamoto hizi zote, ndizo twapambana nazo.

8.Ukame wa kukithiri, tetemeko duniani,
Imekuwa ni hatari, zatukuta maishani,
Ugavi wawa ni shari, bidhaa za viwandani,
Changamoto hizi zote, ndizo twapambana nazo.

9.Hali hii kukabili, hatua ziko kazini,
Tena twazidi jadili, yasitufike shingoni,
Tuukubali ukweli, hali ngumu duniani,
Changamoto hizi zote, ndizo twapambana nazo.

10.Kwanza sote twahimizwa, tulio hapa nchini,
Ni vizuri kuzoezwa, kutumia vya nyumbani,
Mahitaji tapunguzwa, ya dola ya Marekani,
Changamoto hizi zote, ndizo twapambana nazo.

11.Uzalishaji kuzidi, wa hapa kwetu nyumbani,
Tuiongeze akidi, mauzo ughaibuni,
Tutaongeza idadi, dola zetu mifukoni,
Changamoto hizi zote, ndizo twapambana nazo.

12.Hivi njiti kiberiti, ni za fedha za kigeni?
Wakati tunayo miti, tuzichonge viwandani?
Tunajipiga kifuti, kwa matumizi mageni,
Changamoto hizi zote, ndizo twapambana nazo.

13.Vyote tuviagizavyo, ni vya lazima nyumbani?
Mbona vingine tunavyo, tusitumie kwanini?
Kwa hali ilivyo sivyo, dola ngumu duniani,
Changamoto hizi zote, ndizo twapambana nazo.

14.Hizi fedha za kigeni, muhimu sana nyumbani,
Kwa bidhaa za kigeni, zisokuwepo nyumbani,
Ni bora kama madini, tukiwa nazo ghalani,
Changamoto hizi zote, ndizo twapambana nazo.

15.Wewe wahitaji dola, hizi fedha za kigeni,
Usinunue chakula, tuzalishacho nyumbani,
Na mashati yenye kola, tushonayo viwandani,
Changamoto hizi zote, ndizo twapambana nazo.

16.Hiki kipindi mpito, kotekote duniani,
Ndiyo tunatoa wito, sote tubaki makini,
Na tusiwe tumbo joto, hatujafika shidani,
Changamoto hizi zote, ndizo twapambana nazo.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news