Iringa msitembee usiku

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI imewatahadharisha wananchi mkoani Iringa kuacha kutembea usiku ili kuepukana na madhara ya kuvamiwa na Simba walioingia katika makazi ya watu.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) ameyasema hayo Juni 26, 2023 jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe.Grace Tendega aliyetaka kujua nini mkakati wa Serikali wa kuhakikisha wananchi wananchi wa Iringa wanaishi kwa uhuru kutokana na changamoto ya Uvamizi wa Simba.

“Niendelee kutoa elimu kupitia Bunge hili kwamba wakati huu ambapo tunawasaka hawa Simba wananchi wawe na tahadhari ya kutotembea usiku lakini pia wenye mifugo wawashe mioto kuzunguka maeneo ya mifugo ili kuepusha Simba wasisogee katika maeneo yao,” Mhe. Masanja amesisitiza.

Kufuatia hatua hiyo Mhe.Masanja amesema Serikali tayari imeshapeleka helikopta inayozunguka usiku na mchana kuhakikisha Simba hao wanapatikana na kurudishwa katika maeneo yao ili kuhakikisha maisha ya Watanzania yanalindwa kwa gharama yoyote

Kuhusu mikakati ya Serikali ya kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu, Mhe. Masanja amesema Serikali inatekeleza Mkakati wa kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu wa mwaka 2020 – 2024 ambapo Wizara inatoa elimu juu ya kujikinga na wanyamapori wakali na waharibifu; inajenga vituo vya askari wanyamapori ili kusogeza huduma karibu na wananchi; kuwafunga mikanda (GPS collars) tembo; na kuanzisha timu maalum (Rapid response Teams).

Pia, Serikali inaendelea kuwashirikisha wananchi kwa kutoa mafunzo kwa Askari wa Vijiji (VGS) ili kuongeza nguvu ya kudhibiti tembo katika maeneo ya wananchi.

Aidha, amesema Serikali imeshaweka mipango ya kujenga fensi ya umeme katika baadhi ya maeneo ili kupunguza athari ya wanyama wakali na waharibifu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news