Jaji Imani Daud Aboud kutoka Tanzania achaguliwa tena kuwa Rais

NA DIRAMAKINI

MHESHIMIWA Jaji Imani Daud Aboud kutoka Tanzania amechaguliwa tena kuwa Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kwa muhula wa pili wa miaka miwili na wa mwisho.

Ni katika uchaguzi uliofanyika Juni 12, 2023 wakati wa ufunguzi wa Kikao cha kawaida cha 69 cha Mahakama hiyo ya Afrika, kinachoendelea kwenye Makao makuu ya Mahakama hiyo mjini Arusha.

Katika kikao hicho, Mheshimiwa Jaji Sacko Modibo kutoka Mali amechaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Mahakama.

Akitoa shukrani zake, Jaji Imani aliwashukuru Majaji wenzake kwa kumchagua kwa mara nyingine, tena kwa kauli moja, na kwa imani waliyoonyesha kwa uongozi wake.

“Nimefurahishwa sana na imani mliyo nayo kwangu Majaji wenzangu, na nawashukuru kwa dhatiu kabisa,”amesema.

Jaji Imani ambaye kabla ya kuchaguliwa kwa mara ya kwanza kushika wadhifa huo katika Mahakama hiyo, alikuwa ni Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Divisheni ya Kazi.


Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Haki za Watu ni mahakama iliyoanzishwa na nchi za Kiafrika ili kuhakikisha ulinzi wa haki za binadamu na watu katika Afrika.

Mahakama hiyo ilianza shughuli zake rasmi 2006 jijini Addis Ababa, Ethiopia na baada ya mwaka mmoja ikahamia kwenye kiti chake cha kudumu jijini Arusha ambapo mahakama hiyo inaundwa na majaji 11, raia wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika.

Mahakama inatarajia kutoa maamuzi tisa kesho, kuanzia saa 10:00 (Saa za Afrika Mashariki). Kikao cha maamuzi hayo kitarushwa moja kwa moja kwenye mtandao.

Unaweza kufiuatilia kwa Kiingereza: https://www.youtube.com/user/africancourt/live, na Kifaransa: https://www.youtube.com/@courafricaine/live

Katika Kikao hicho cha 69, Majaji wataitisha Kongamano la siku tatu kuanzia tarehe 14 hadi 16 Juni mjini Dodoma, mji mkuu mpya wa Tanzania, kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa Mahakama na kuboresha ulinzi wa haki za binadamu katika bara zima la Afrika. “Kongamano hilo litawezesha kuratibu na kuchanganua mbinu bora za kufanya kazi," aliongeza

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news