Jela miaka 30 kwa kusafirisha kilo 38.84 za bangi wilayani Bagamoyo

NA DIRAMAKINI

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kibaha mkoani Pwani imemhukumu Abubakar Mbanje kutumikia kifungo cha miaka 30 jela baada ya kukutwa na hatia ya kusafirisha kilo 38.84 za dawa za kulevya aina ya bangi.

Hukumu hiyo imesomwa jana na Hakimu Mkazi Salumu Ally baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote na kuthibitisha pasipo shaka kuwa mshtakiwa ana hatia.

Awali ilidaiwa kuwa Mei 19, 2022, mshtakiwa alikamatwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) eneo la Bandari bubu, mji mpya Wilaya ya Bagamoyo akisafirisha bangi hiyo kwa njia ya pikipiki.

Sheria inasemaje?

Kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, sura ya 95, kilimo na biashara ya bangi katika Taifa letu ni Kosa la Jinai.

Kwa hiyo, kujihusisha kwa namna yoyote na bangi (kulima, kuuza, kuhifadhi, kutumia, kuichakata, nk) ni Kosa la Jinai na adhabu yake inafikia hadi kifungo cha maisha jela. JELA.

BANGI NI NINI?

Aidha, kwa mujibu wa DCEA, bangi ni aina ya dawa ya kulevya inayotokana na mmea unaoitwa “Cannabis sativa” ambao hustawi na hutumika kwa wingi hapa nchini na duniani kote.

Bangi huathiri ubongo na kubadili jinsi tunavyotafsiri uhalisia wa vitu. Majani na maua ya mmea huo hukaushwa na hutumiwa kama kilevi peke yake au kwa kuchanganywa na dawa zingine.

Mara nyingi bangi imekuwa ni kati ya dawa ya awali kutumiwa, ambapo watumiaji wengi huanza matumizi wakiwa na umri mdogo hivyo kuwa katika hatari zaidi kiafya, kijamii na kiuchumi.

Aidha, watumiaji wengi wa bangi huishia kutumia dawa nyingine hapo baadae kama heroin na cocaine. Hivyo, bangi hutumika kama njia ya kuingia katika matumizi ya dawa nyingine za kulevya.

Majina mengine ya bangi yanayotumika mitaani ni kama msuba, dope, nyasi, majani, mche, kitu, blanti, mboga, sigara kubwa, ndumu, msokoto, ganja, nk.

 MADHARA YA BANGI

  • Bangi huamsha magonjwa ya akili hususani, ‘depression’, ‘anxiety’ ‘psychosis’na ‘schizophrenia’
  • Moshi wa bangi huzalisha lami na kemikali mbalimbali ambazo zinaweza kusababisha kansa ya mapafu
  • Bangi huathiri mifumo ya fahamu na kumfanya mtumiaji awe kwenye hali ya njozi ambapo ataona na kusikia vitu tofauti na uhalisia. Hali hii inachangia kupunguza stamina ya mtumiaji na kusababisha ajali, uharibifu wa mali pamoja na kushusha ufanisi wa kazi.
  • Baadhi ya watumiaji hupata wasiwasi mkubwa mara wavutapo na kuwahisi vibaya watu wanaowazunguka kuwa wanataka kuwadhuru au kuhisi wanajua kuwa wamevuta bangi. Wasiwasi huweza kumfanya mtumiaji amshambulie mtu na kumdhuru bila hatia
  • Mara baada ya kutumia bangi mapigo ya moyo huongezeka na mishipa ya damu kupanuka na hata kusababisha kiharusi.
  • Uvutaji wa bangi huweza kusababisha kikohozi sugu, kukosa pumzi, vidonda vya koo na pumu
  • Mtumiaji wa bangi hukosa mwamko wa maendeleo akijihisi ni mwenye maendeleo makubwa wakati anaishi maisha duni kabisa.
  • Matumizi ya bangi huchochea mmomonyoko wa maadili kutokana na ongezeko la vitendo vya uhalifu ikiwemo wizi, utapeli na ukatili wa kijinsia katika jamii.
  • Bangi husababisha utegemezi, huvuruga mahusiano ya kifamilia pamoja na upotevu wa ajira kwa mtumiaji. Matokeo ya kuvurugika mahusiano ni pamoja na kuwepo kwa migogoro isiyoisha, kutelekeza wenza na watoto, kuvunjika kwa ndoa, kutokuwa na ajira, ongezeko la watoto wa mitaani na biashara ya ngono.


Matumizi ya bangi huchochea matumizi ya dawa nyingine za kulevya kwa namna mbili; kwanza kwa kuchanganya bangi na dawa nyingine za kulevya au kwa kuhamia kwenye dawa zingine kama heroin na cocaine. Hali hii huongeza madhara kwa mtumiaji na hata wakati mwingine husababisha vifo.

Kilimo haramu cha bangi mara nyingi hufanyika kwenye vyanzo vya maji, misituni na milimani ambapo miti hukatwa au kuchomwa moto na kusababisha kutoweka kwa baadhi ya viumbe hai na uoto wa asili, kukauka kwa vyanzo vya maji, mmomonyoko wa udongo na hatimaye ukame. Uharibifu huu umejidhihirisha katika safu za milima ya Uluguru, Usambara, Udzungwa na maeneo ya Arumeru.

Kushamiri kwa kilimo haramu cha bangi, kunaweza kusababisha uhaba wa mazao ya chakula na hivyo kupelekea kupanda bei ya vyakula na hata janga la njaa.

Kutokana na athari za matumizi na kilimo haramu cha bangi, Taifa linaingia gharama kubwa katika kukabiliana na tatizo hili, ikiwemo utoaji wa elimu mashuleni na katika jamii, matibabu ya maradhi mbalimbali, uteketezaji mashamba na udhibiti wa biashara haramu ya bangi.

Bangi huchangia kuongezeka kwa umasikini kwa mtumiaji, jamii na taifa kwa ujumla na kupelekea kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news