NA MWANDISHI WETU
TAASISI ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group imefunga mashine mbili za kisasa za kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiogram – ECHO) kwaajili ya kuboresha huduma za matibabu ya moyo kwa wagonjwa wanaotibiwa katika hospitali hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group, Dkt.Tulizo Shemu alisema mashine hizo za kisasa zinauwezo wa kubaini matatizo ya moyo ya ndani ambayo mtu anayo tofauti na ilivyo kwa mashine zingine.
Dkt. Shemu ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema kuwepo kwa mashine hizo katika Hospitali ya JKCI Dar Group kutasaidia watu wengi wa wilaya ya Temeke na maeneo ya jirani kupata huduma ya matibabu ya moyo kwa wingi pasipo kutumia muda mrefu.

Dkt. Shemu alisema tangu Novemba 14 mwaka jana Serikali ilipokabidhi hospitali ya Dar Group kwa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) idadi ya wagonjwa wanaotibiwa magonjwa ya moyo imekuwa ikiongezeka, kwasasa wanaona wagonjwa 30 hadi 40 kwa siku, pia kliniki za moyo ziko kila siku na huduma inatolewa saa 24 ukilinganisha na hapo nyuma ambapo kliniki za moyo zilikuwa zinatolewa mara mbili kwa wiki siku za Jumanne na Alhamisi.
Alisema katika Hospitali hiyo pia wanatoa huduma za matibabu kwa magonjwa mengine tofauti na moyo ambapo huduma zimezidi kuimarika kwa kuongeza idadi ya madaktari bingwa, kununua vifaa vya kisasa, kuimarisha huduma ya dharura, kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa wataalamu wa afya na kuhakikisha dawa zote muhimu zinapatikana.

“Mashine hizi zinauwezo mkubwa wa kufanya kazi zinaweza kupima watu hamsini hadi sitini kwa siku na mbali na kupima moyo zinapima mishipa ya damu kuona kama inapitisha damu vizuri au la, zinapima mfumo wa tumbo, mkojo na uzazi”, alisema Hamisi.
Kwa upande wake Nassoro Tangulu ambaye ni mgonjwa anayetibiwa katika Hospitali ya JKCI–Dar Group alishukuru uwepo wa hospitali hiyo ambayo imewasaidia kupata huduma mbalimbali za matibabu yakiwemo ya moyo.
“Mimi na familia yangu tunatibiwa katika Hospitali hii nilikuwa nakuja hapa kwaajili ya matibabu ya shingo na mgongo lakini sasa hivi ninatibiwa moyo, ninaamini uwepo wa mashine hizi utasaidia wananchi wenye matatizo ya moyo na mengine kupata huduma nzuri na kwa wakati bila kutumia muda mrefu,”alisema.
