KAACHA ALAMA ZAKE, LALA SALAMA LEILA SHEIKH

NA LWAGA MWAMBANDE

TASNIA ya habari nchini Tanzania inaomboleza kifo cha mwandishi wa habari mkongwe na mmoja wa waanzilishi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Bi.Leila Sheikh ambaye alifariki ghafla usiku wa kuamkia Juni 12, 2023.

Leila Sheikh alikuwa mmoja wa wanachama waanzilishi wa TAMWA mwaka 1987, na baadaye aliandika historia ya TAMWA. Pia, alikuwa mhariri wa jarida la TAMWA, Sauti ya Siti (Sauti ya Wanawake).

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, mwanaharakati nguli na mpambanaji ameondoka katika kipindi ambacho Taifa na jamii ilikuwa inamuhitaji aweze kushiriki kikamilifu kusaidia kupasa sauti ili kusaidia kutokomeza vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa wanawake na watoto ambavyo kwa siku za karibuni vimekuwa vikishamiri mijini na vijijini. Endelea;


1.Mwanaharakati nguli, mpambanaji mfano,
Mguu sawa kamili, kwa matendo hata wino,
Haki alizijadili, tena kwa bidii mno,
Amefariki Leila, iwe chachu kwa wengine.

2.Amefariki Leila, iwe chachu kwa wengine,
Watu wote makabila, waanze jali wengine,
Hadi iwe bilabila kuwanyanyasa wengine,
Leila kitabu chake, chetu wengine kusoma.

3.Leila kitabu chake, chetu wengine kusoma,
Livyofanya mambo yake, kwa vitendo na kusema,
Akijenga hoja zake, haki iweae simama,
Wino wake ni wa chuma, hauwezi kufutika.

4.Wino wake ni wa chuma, hauwezi kufutika,
Kama TAMWA waisema, mmoja alisimika,
Hadi TAMWA kusimama, huyo alichakarika,
Kaacha alama zake, kwa hizo atakumbwa.

5.Kaacha alama zake, kwa hizo atakumbukwa,
Zile harakati zake, atazidi kutamkwa,
Na sisi hata wenzake, atazidi kuandikwa,
Yake changamoto kwetu, kwamba tutaacha nini.

6.Yake changamoto kwetu, kwamba tutaacha nini,
Katika maisha yetu, tunapigania nini,
Nini wataona kwetu, karaha au amani,
Maisha yetu kitabu, kinasomwa kitasomwa.

7.Maisha yetu kitabu, kinasomwa kitasomwa,
Twaishi tunaratibu, bila ya mtu kutumwa,
Leila chake kitabu, kimebakia kusomwa,
Andika tutakusema, kwa ubaya hata wema.

8.Andika tutakusema, kwa ubaya hata wema,
Kwa jinsi unavyosema, au kugoma kusema,
Shamba unavyolilima, mavuno yakasimama,
Leila ameondoka, tunamshukuru Mungu.

9.Leila ameondoka, Mungu tunamshukuru,
Duniani kumuweka, kupigania uhuru,
Kazi imekamilika, yake yabakia nuru,
Pole nyingi twazitoa, kwa ndugu hata jamaa.

10.Pole nyingi twazitoa, kwa ndugu hata jamaa,
Majonzi hayajapoa, kifo kwetu ni balaa,
Mungu faraja atoa, kutapoa kuchakaa,
Mungu aliyemleta, ndiye amemchukua.

11.Mungu aliyemleta, ndiye amemchukua,
Leila japo kapita, mengi ametufungua,
Tutazidi kumteta, yake tukiyachungua,
Na sisi vitabu vyetu, vyema vikawa rejea.

12.Na sisi vitabu vyema, vyema vikawa rejea,
Watu wanapovisoma, iwe njia kutokea,
Yale kwao yanagoma, wapate pa kupenyea,
Amemaliza Leila, kaacha mambo mazito.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news