NA GODFREY NNKO
KAMISHNA Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), Aretas Lyimo ameguswa na salamu ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Kisimiri Juu iliyopo wilayani Arumeru mkoani Arusha ambayo inashabihiana na juhudi za mamlaka hiyo katika kudhibiti dawa za kulevya nchini.
...Najivunia kuzaliwa Tanzania, nchi yenye amani na upendo... "Marahaba, hamjambo? Nimefurahia sana salamu yenu, nchi yenye amani,na upendo nchi salama.
"Salamu nzuri sana, nchi yenye amani na upendo na sisi tumekuja hapa kuhakikisha usalama wa nchi unakuwepo,lakini amani na upendo unaendelea kutawala, sawa.
"Mimi ninaitwa Lyimo ni Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, dawa za kulevya si mnazifahamu?.
...ndiyo...moja wapo ya dawa za kulevya hebu nitajieni, dawa za kulevya moja tu,..bangi, kuna mwingine anajua nyingine, wewe, pombe ambayo ni gongo? Ndiyo,mwingine sikara (sigara)...,
"Kwa hiyo bangi ni moja wapo ya dawa za kulevya ambazo zinaharibu akili za mwanadamu, anayetumia bangi anasababisha fujo, anayetumia bangi anakuwa na matatizo ya akili, anayetumia bangi hawezi kuleta amani, sawa?
Ndiyo..., lakini anayetumia bangi anasababisha uhalifu, kwa hiyo hii salamu yenu hapa ya kwamba nchi yenye amani, upendo, nchi ya amani haiwezi kuwepo hiyo nchi ya amani kama dawa za kulevya zipo nchini.
"Kwa hiyo ninyi wanafunzi mtusaidie pia kuhakikisha kwamba tunapiga vita dawa za kulevya ikiwemo bangi. Sasa na huku Kisimiri Juu huku ni watu ambao wanalima bangi sana, si ndiyo...ndiyooo...wazazi wengi wanalima bangi, si ndiyo, ndiyooo...kwa hiyo lazima tuhakikishe tunaikataa bangi,si ndiyo?
Ndiyooo... kwa sababu bangi haileti amani, bangi haileti utulivu, bangi haileti maendeleo na sisi tunataka ninyi mkue, mpate maendeleo, si ndiyo?
Ndiyooo...msome vizuri mfaulu mfaulu ili na ninyi mpate kuja kuwa viongozi wa Taifa hili la Tanzania, si ndiyo? Ndiyooo...,wangapi wanataka kuja kuwa Rais (wote), vizuri sana, wangapi wanataka kuja kuwa wabunge (wote), wangapi wanataka kuja kuwa mawaziri (wote),
"Wangapi wanataka kuja kuwa walimu (wote), wangapi nao wanataka kuja kuwa Kamishna Jenerali wa Dawa za Kulevya (wote), vizuri sana, kwa hiyo ili sasa muweze kufika huko lazima tuhakikishe dawa za kulevya hazipo nchini, maana ukitumia dawa za kulevya hauwezi kuja kuwa mbunge, ukitumia dawa za kulevya hauwezi kuja kuwa mwalimu kwa sababu akili yako inaharibika, si ndiyo?
Ndiyoo..., kwa hiyo tuwashauri wazazi wetu waache kulima bangi, sawa? Ndiyooo..., tuwashauri wazazi wetu waache kulima bangi, tuwashauri wazazi wetu wabadilishe kilimo walime mazao ya chakula na mazao mengine ya biashara,lakini wasilime bangi kwa sababu bangi inaharibu watoto, bangi inaharibu Taifa, bangi inaharibu usalama wa nchi,"amesisitiza kwa kina Kamishna Jenerali wa DCEA,Aretas Lyimo.
Shuleni
Mmoja wa walimu Shule ya Msingi Kisimiri Juu, amewataka wanafunzi hao kusimama badala ya Serikali. "Kwa hiyo msimame badala ya Serikali, mtakavyorudi nyumbani waambieni wazazi sasa walime mazao mengine mbadala ya bangi.
"Mazao gani mengine mnaweza mkayalima?Mahindi, maharage, mihogo, kilimo cha mboga mboga pia walime, sawa? Ndiyoo,"amesisitiza Mwalimu huyo na kuungwa mkono na wanafunzi.
Jitihada
Ili kuhakikisha dawa za kulevya zinatokomewa hapa nchini Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imeendelea kufanya jitihada mbalimbali kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama wakiwemo wananchi ambapo hivi karibuni imefanya operesheni kwa siku mbili mfululizo katika vijiji vya Kisimiri Juu na Lesinoni wilayani Arumeru mkoani Arusha na kukamata magunia 731 ya bangi kavu pamoja na kuteketeza hekari 308 za mashamba ya bangi mbichi.
Kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, sura ya 95, kilimo na biashara ya bangi katika Taifa letu ni kosa la jinai. Kwa hiyo, kujihusisha kwa namna yoyote na bangi (kulima, kuuza, kuhifadhi, kutumia, kuichakata au kwa namna nyingine yoyote ile) ni kosa la jinai na adhabu yake inafikia hadi kifungo cha maisha jela.
Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo alibainisha Juni 2, 2023 kuwa, katika Kijiji cha Kisimiri Juu,DCEA ilikamata magunia 482 na kutekeleza hekari 101 za mashamba ya bangi.
Aidha, katika Kijiji cha Lesinoni mamlaka hiyo ilikamata magunia 249 ya bangi kavu na kuteketeza hekari 207 ambapo jumla ya watuhumiwa tisa wamekamatwa na dawa hizo za kulevya.
Kamishna Jenerali Lyimo amefafanua kuwa, ukamataji huo umefanyika Mei 31 hadi Juni Mosi, mwaka huu kufuatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan la kufanya operesheni nchi nzima.
Lengo ni kuhakikisha dawa za kulevya zinatokomezwa nchini. Aidha, kwa mujibu wa Kamishna Jenerali Lyimo, operesheni hizo zilifanyika siku moja baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera na Bunge), Mheshimiwa Jenista Mhagama (Mb) kutoa taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya nchini kwa mwaka 2022 ambayo alitaja mikoa ya Arusha, Iringa,Morogoro na Manyara kujihusisha na kilimo cha bangi kwa kiasi kikubwa.
Amefafanua kuwa, DCEA kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama nchini inaendelea kufanya operesheni za mara kwa mara katika maeneo yote nchini ili kuhakikisha kilimo cha bangi, mirungi na dawa zingine za kulevya zinatokomezwa kabisa na wananchi kujikita katika kilimo cha mazao mbadala ya biashara na chakula.
DCEA na TAKUKURU
Mei 26, 2023 Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) zilisaini hati ya Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi hizi hususani katika kuzuia vitendo vya rushwa na dawa za kulevya hapa nchini kupitia vilabu vilivyopo katika shule za msingi, sekondari hadi vyuoni.
Makubalianao hayo yalisainiwa na Mkurugenzi wa TAKUKURU, CP. Salum Hamduni na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Aretas Lyimo katika ofisi ya TAKUKURU makao makuu jijini Dodoma.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari, CP. Salum Hamduni alisema, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupamban na Dawa za Kulevya na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa wamekubaliana kutumia rasilimali walizonazo kuwahamasisha wanafunzi, vijana na jamii kwa ujumla kutoshiriki vitendo vya rushwa na biashara haramu ya dawa za kulevya pamoja na kuchukua hatua stahiki za kukabiliana na mambo hayo.
‘‘Tuna matarajio makubwa baaada ya kusaini makubaliano haya kwani nguvu yetu ya kudhibiti dawa za kulevya na rushwa itaongezeka na kufanya jamii ya watanzania kuwa salama,’’ alisema CP. Hamduni.
Aidha, aliwaasa wanahabari kutumia vyombo vya habari kuunga mkono juhudi hiziokwa kuwahamasisha wananchi kushiriki katika kutokomeza vitendo vya rushwa na matumizi ya dawa za kulevya.
Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), Aretas Lyimo aLIsema anafuraha kusaini MoU ambayo inawaunganisha TAKUKURU na DCEA katika kushirikiana kikazi kutoa elimu shuleni na jamii kwa ujumla juu ya madhara ya dawa za kulevya na rushwa kwa jamii kwani makosa haya yanauhusiano wa karibu na yanahitaji suluhu ya pamoja.
"Muungano huu ni muhimu kwani utasaidia kufanya matumizi sahihi ya rasilimali chache tulizonazo kutatua matatizo mawili kwa pamoja,’’alisema.
Pia alisema makosa yanayoshughulikiwa na taasisi hizo mbili ni makosa ya kupangwa na vita dhidi ya makosa haya yanaupinzani kwenye jamii kwani yanaleta faida kwa wanayoyatekelezea hivyo kupitia ushirikiano huu na elimu itakayotolewa, vijana watajengewa hali ya uzalendo na kuijenga jamii kuchukia matendo ya rushwa na dawa za kulevya hivyo kuibua chachu ya maendeleo kwa Taifa.
Pamoja na hayo, kamishna Jenerali Lyimo alionesha nia ya dhati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kupingana na rushwa na dawa za kulevya kwa kusema, ‘‘Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ana dhamira ya dhati ya kuongoza jamii isiyo na rushwa wala dawa za kulevya, na kupitia makubaliano yaliyofanyika yataleta tija kwa jamii na kutimiza azma ya Mhe. Rais ya kuwa na jamii bora, ya wachapakazi, jamii ya wazalendo na jamii ya kulisukuma taifa mbele kupata maendeleo.
"Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inaahidi kushirikiana kikamilifu katika kuisimamia na kuimarisha vita dhidi ya rushwa na dawa za kulevya, na tutaendelea kushirikiana kuhakikisha jamii inaelewa madhara ya Rushwa na Dawa za kulevya. Tumeamua kuwekeza nguvu kubwa katika kuzuia kuliko kukamata maana kukamata kunakuja pale ambapo nguvu ya kuzuia imeshindikana,"alisema Kamishna Jenerali Lyimo.
Kuhusu DCEA
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ilianzishwa chini ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015. Sheria hii iliifuta Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya. Kuanzishwa kwa Mamlaka Kulitokana na mapungufu yaliyokuwepo katika mfumo wa udhibiti wa dawa za kulevya.
Mapungufu hayo yalikuwa ni pamoja na Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya iliyoanzishwa na Sheria ya ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995 kukosa nguvu ya kisheria ya kupeleleza, kufanya uchunguzi na kukamata wahalifu wa dawa za kulevya.
Kutokana na mapungufu hayo, Baraza la Mawaziri katika kikao chake cha tarehe 8 Novemba, 2007 (Waraka Na 60/2007) liliagiza, kurekebisha au kufuta Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995, ili kukidhi matakwa na changamoto za udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya.
Baraza la Mawaziri liliagiza kuundwa kwa chombo cha kupambana na dawa za kulevya chenye uwezo kiutendaji kwa kukipa mamlaka ya ukamataji, upekuzi na upelelezi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola ili kuongeza ufanisi wa udhibiti wa dawa za kulevya nchini.
Kufuatia agizo hilo, tarehe 24/03/2015 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga na kupitisha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015 na kuanza kutumika rasmi tarehe 15 Septemba, 2015 kupitia tangazo la Serikali namba 407 (GN NO.407/2015).
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ilianza kutekeleza majukumu yake kikamilifu tarehe 17 Februari, 2017 baada Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kumteua Kamishna Jenerali.
Tags
DCEA
DCEA Tanzania
Habari
Kataa Dawa za Kulevya na Timiza Ndoto Zako
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)
Nafuatilia sana Tume hii ya mamlaka ya udhibiti na kupambana na dawa za kulevya Tanzania ukweli munafanya kazi vizuri chini ya Kamishna Jenerali Hongereni sana
ReplyDelete