KATIBU MKUU UTUMISHI ATAKA MALALAMIKO NA MAONI YA WANANCHI KUJIBIWA KWA WAKATI KUPITIA MIFUMO YA KIDIGITALI

NAMWANDISHI WETU

KATIBU Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi amewataka Wakuu wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa Taasisi za Umma kushughulikia kwa wakati malalamiko na maoni ya Wananchi kupitia mifumo ya kidigitali ya e-mrejesho na e-uhamisho ili kuleta tija iliyokusudiwa.
Bw. Mkomi ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo ya matumizi na uendeshaji wa mfumo wa kutumia, kupokea na kufuatilia malalamiko, mapendekezo, maulizo na pongezi (e-mrejesho) na mfumo wa e-Uhamisho kwa Wakuu hao wa Idara.

Amesema licha ya kuundwa kwa mifumo hiyo kama hakutakuwa na uwajibikaji wa kufanyia kazi maoni na malalamiko yaliyowasilishwa na wananchi hao kutakuwa hakuna maana ya kuwa na mifumo hiyo.
"Mtakapokuwa mnachelewa kujibu malalamiko ya wananchi, wananchi hao wataandika barua kwangu huku wakielekeza barua hiyo ionwe na Katibu Mkuu Kiongozi ambaye ni Mkuu wa Watumishi wote pamoja na kwa Waziri Mkuu, hatutaki kufika huko jibuni kwa wakati," Bw. Mkomi amesisitiza.

Kufuatia hatua hiyo, Bw. Mkomi amesema anataka kuona Maafisa watakaochaguliwa kusimamia mifumo hiyo wanawajibika ipasavyo ikiwemo kuhakikisha malalamiko ya wananchi yanajibiwa kwa haraka huku akisisitiza suala la usiri.

Ameongeza kuwa, endapo mfumo wa e-mrejesho utatumika ipasavyo utasaidia Taasisi za Serikali kuboresha huduma zinazotolewa kwa wananchi kwani mrejesho ambao utakuwa ukitolewa utasaidia katika kufanya maamuzi yanayoendana na hali halisi.

Amefafanua kuwa, mfumo wa e-mrejesho umesanifiwa kwa namna ambayo unaongeza uwazi, uwajibikaji na usiri kwa kuwa ni mfumo unaowezesha viongozi kuona kwa jinsi gani malalamiko au maoni yanavyoshughulikiwa.

Akizungumzia mfumo wa e-uhamisho, Katibu Mkuu Mkomi amesema, mfumo huo utakuwa wa wazi na utasaidia Watumishi kuomba nafasi ya kuhama au kuhamia mahali ambako kuna uhitaji wa watumishi na si vinginevyo.
Awali, Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Maadili kutoka Ofisi ya Rais - UTUMISHI, Bi. Leila Mavika amesema kutumika kwa mfumo wa e-mrejesho kutasaidia Serikali kuongeza uwajibikaji kwa watumishi wa umma katika kuwahudumia wananchi.

Aidha, ameongeza kuwa taarifa mbalimbali zitakazopatikana katika mifumo hiyo itasaidia kuongeza utendaji kazi Serikalini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news