Kila siku ni asante,tunachotaka ni ubora

NA LWAGA MWAMBANDE

KLABU na timu mbalimbali za soka nchini Tanzania zimeendelea kufanya maboresho kwa ajili ya kujiandaa na msimu ujao wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, huku maboresho hayo yakienda sambamba na kuwashukuru baadhi ya nyota wao.

Shukurani hizo ambazo zinatolewa kwa nyakati tofauti tangu msimu wa Ligi Kuu ya NBC ufikie tamati, wengi wetu tumeshuhudia namna ambavyo nyota hao wanaagwa, makocha wanaagwa na kuvunja mikataba huku wakitazama nyota wengine ambao wanaamini wataongeza thamani msimu ujao.

Tumeshuhudia,tayari Klabu ya Simba imeachana na kiungo mshambuliaji Mnigeria, Nelson Esor-Bulunwo Okwa baada ya msimu mmoja tangu asajiliwe kutoka Rivers United ya kwao.

Pamoja na kusajiliwa mwanzoni mwa msimu, lakini Okwa alipelekwa kwa mkopo Ihefu SC ya Mbeya ambako alimalizia msimu.

Okwa anakuwa mchezaji wa nne kuoneshwa mlango wa kutokea Simba SC baada ya beki rai wa Ivory Coast, Mohamed Ouattara, kiungo Mnigeria Víctor Akpan na winga Mghana, Augustine Okrah.

Aidha, Simba imeachana na makocha wake wawili wa Fiziki, Kelvin Mandla Ndlomo na Fareed Cassiem, wote raia wa Afrika Kusini na kocha wa makipa, Mmorocco, Zakaria Chlouha na kocha wake wa timu yake ya wanawake, raia wa Uganda, Charles Lukula.

Katika hatua nyingine, Klabu ya Yanga imetangaza kuachana na winga Mghana, Bernard Morrison baada ya msimu mmoja tangu arejee kutoka kwa mahasimu wao, Simba SC.

Morrison alijiunga na Yanga kwa mara ya kwanza katika dirisha dogo mwaka 2020 akitokea DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na mwishoni mwa msimu akahamia kwa mahasimu, Simba ambako alicheza hadi Julai, mwaka jana aliporejea Yanga SC.

Morrison anakuwa mchezaji wa nne kuondoka baada ya kiungo Feisal Salum aliyeuzwa Azam FC, mawinga wengine, Mkongo Tuisila Kisinda na mzawa, Dickson Ambundo.

Vile vile, tayari Yanga SC imeachana na Kocha wake Mkuu, Mtunisia Nasredeen Nabi na Kocha wa makipa, Mbrazil Milton Nienov.

Wakati huo huo, kwa upande wa Azam FC,mlinda mlango chipukizi Wilbol Maseke Changarawe amekuwa mchezaji wa sita kutemwa kwenye kikosi cha Azam FC baada ya kumalizika kwa msimu wa 2022-2023.

Maseke anaungana na beki Bruce Kangwa raia wa Zimbabwe,Kenneth Muguna raia wa Kenya na mshambuliaji Rodgers Kola kutoka Zambia na wazawa wenzake, Ismail Aziz na Cleophace Mkandala.

Azam FC pia imeachana na makocha wake wanne, aliyekuwa Kaimu Kocha Mkuu, Kali Ongala, Msaidizi wake, Aggrey Morris, Kocha wa Makipa, Mspaniola Dani Cadena na kocha wa Fiziki, Mtunisia Dkt.Moadh Hiraoui. 
 
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, licha ya hatua ambazo zinachukuliwa na klabu pamoja na timu hizo wanachotaka mashabiki wa soka Tanzania ni ubora wa mpira uwanjani na kupaisha soka la Tanzania. Endelea;

1.Us’ende kimya asante, kumenoga hizi timu,
Kila siku ni asante, wale waliohitimu,
Waondoshwa kama Conte, kwa muda wamejihimu,
Tunachokitaka sisi, pira bora uwanjani.

2.Pengine ni timu tatu, asante sasa ni gemu,
Ni wengi sio watatu, na wao hawana hamu,
Tutaja jiuliza tu, ule ujao msimu,
Tunachokitaka sisi, soka bora uwanjani.

3.Tatizo lake asante, ni kama kwenda kuzimu,
Hawapoteagi wote, hurudi kama mizimu,
Nafasi acha wapate, wanacheza washutumu,
Tunachokitaka sisi, soka bora uwanjani.

4.Hawa ambao waagwa, kama wamemeza sumu,
Viatu huko hupigwa, zinapokutana timu,
Ni kama wamevurugwa, kisasi kwao chadumu,
Tunachokitaka sisi, soka bora uwanjani.

5.Tunahesabuhesabu, wanatoswa wanadamu,
Hazitolewi sababu, asante kama karamu,
Huo mwema uratibu, wapeni zetu salamu,
Tunachokitaka sisi, soka bora uwanjani.

6.Hasa kwa kimataifa, huku kutamba tudumu,
Tafuteni maarifa, makundi nne zitimu,
Tukayalete maafa, kwa zile zingine timu,
Tunachokitaka sisi, soka bora uwanjani.

7.Asante zagawanyika, kwenye hizihizi timu,
Huku mwali aachika, kwingine wanamzumu,
Ni sherehe waalika, twendeni kula karamu,
Tunachokitaka sisi, soka bora uwanjani.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news