NA ADELADIUS MAKWEGA
WAKRISTO wameambiwa kuwa wanawajibu wa kulitangaza na kulipeleka kwa watu neno la Mungu ambalo ni taa na mwanga wa kuonesha namna ya kuyafanya mambo ya Mungu, kila mmoja anawajibu wa kufanya utume wa kulitangaza neno hilo.
Pia, kila mmoja akumbuke kuwa siyo wote wapo tayari kulisikia neno hilo na kila anayetangaza anawajibu wa kuwa mkomavu na asiyekata tamaa.
Hayo yamesemwa Jumapli ya 12 ya Mwaka A wa Liturjia ya Kanisa, Juni 25, 2023 na Padri Samweli Masanja katika Kanisa la Bikira Maria Malkia wa Wamisionari, Parokia ya Malya, Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza.
“Kila mmoja awe tayari kukumbana na upinzani, vikwazo, dharau na shutumu na hayo yote ni kwa ajili ya lile neno.”
Akiendelea kububiri katika misa ya kwanza ya dominika hiyo, Padri Masanja alisema kuwa Yesu Kristo katika mafundisho yake anasema wazi kuwa yule anayemkiri mbele za watu nayeye atamkiri mbele ya Baba yake.
Padri Masanja aliongeza kuwa,“Kumkiri Kristo maana yake ni kujidhihirisha kwa matendo na mwenendo, kumpinga Kristo ni kuyakata yale mafundisho ya Kristo hadharani.”
Misa hii pia iliambatana nia na maombi kadhaaa, mojawapo ni, “Utuondolee woga wa kushuhudia imani yetu katika maisha ya familia na katika shughuli zetu hadharani.”
Wakati wa matangazo Padri Masanja alimualika sista mmoja kutoka Shirika la Wabenedkitine Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza ambaye alihamasisha juu ya kila mlei kushiriki katika Juma la Ukarimu litakalofanyika Agosti 2023.
Hadi misa hiyo ya iliyoanza saa 12.00 ya Asubuhi inakamilika, kwa juma zima hali ya hewa ya Malya na viunga vyake ni ya jua kali na wakati wa asubuhi kuna baridi ya hapa na pale.